Wakulima wa pamba Itilima walilia elimu ya maofisa ugani

Wakazi wa kijiji cha Nyanchenche Kata ya Kagunga Halamshauri ya Sengerema mkoani Mwanza wakipalilia Shamba la Pamba lililolimwa kitaalamu baada ya kupata mafunzo kutoka Shirika la Dalberg linalofanya na halmashauri mbalimbali. Picha na Jesse Mikofu

Simiyu. Wakulima wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu wamesema ndani ya misimu kadhaa iliopita ya upanzi (kupanda mbegu), wamekuwa wakikosa maelekezo muhimu kutoka kwa maofisa ugani.

“Wengi wetu hapa hatuna uhakika wa zao gani linalotakiwa kupandwa kwenye baadhi ya maeneno na udongo uliopo. Hii imekuwa ni changamoto maana tayari tulikuwa tumekariri zao moja tu la pamba,” alisema mmoja wa wakulima hao, Yusuf Mutanda.

Licha ya Mkoa wa Simiyu kutegemea kilimo cha pamba, pia ufugaji wa mifugo, ng’ombe.

Kutokana na hali hiyo, wakulima wameiomba Serikali kuwaongezea maofisa ugani ili kuwasaidia kutambua mbegu mwafaka za zao hilo na aina ya udongo.

Ofisa Kilimo, Wilaya ya Itilima, Mateso Paul alisema maofisa ugani waliopo kwa sasa ni wazee na wamekaribia umri wa kustaafu, hivyo imekuwa changamoto kuwafundisha wakulima namna ya kufanya kilimo cha kisasa.

Alisema wilaya hiyo ina maofisa ugani 14 pekee ambao hawakidhi idadi ya kata 22 na vijiji 102 vilivyopo Itilima.

“Tunatarajia Serikali kuwaajiri maofisa ugani wengi ili waweze kuwasaidia wakulima ambao kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa, wanashindwa kutambua aina ya zao la kupanda kwa wakati maalumu,” alisema Mateso.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyashishi wilayani hapa, Madereke Ngolo alisema pamoja na kushindwa kutambua aina ya zao la kupanda, wakulima wengi walikosa maarifa ya kutumia maji kutoka Ziwa Victoria.

Itilima ni moja kati ya wilaya tano ambazo zinaunda Mkoa wa Simiyu. Wilaya hizo ni Meatu, Bariadi, Busega na Maswa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema zao la biashara linalolimwa mkoani humo ni pamba inayozalishwa kwa asilimia 47 ya pamba yote nchini.

Pamba hulimwa na wakulima wadogo katika mikoa 15 na wilaya 46 za Tanzania Bara na Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita, Kigoma, Kagera, Tabora na Singida ambayo hulima kwa asilimia 95.

Hivi karibuni Tanzania na Brazil ziliingia makubaliano ya kuinua kilimo cha pamba ili kiwe na tija kwa wakulima nchini.

Makubaliano ya mradi huo wa kilimo yamekuja wakati Brazil ipo katika hatua kubwa za kimageuzi ya kilimo.

Mradi wa kuinua kilimo cha pamba unaotekelezwa na Brazil nchini utajikita zaidi katika kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na uzinduzi wa utafiti umfikie mkulima ili aweze kuongeza tija.

Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa anaishukuru Serikali ya Brazil kwa utekelezaji wa mradi huo nchini unaotokana na uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.