SHERIA BIASHARA : Mkataba unaokubalika, una sifa zake

Muktasari:

Kila inapobidi watu wanaingia kwenye makubaliano ya kutekeleza kitu fulani chenye masilahi kwao. Ili kuepuka mgogoro unaoweza kujitokeza, zipo sifa za mkataba zinazokubalika kisheria ambazo ukizizingatia hautapoteza haki zako.

Kwa mujibu wa sheria ya mikataba inayatambua makubaliano yanayofanyika kati ya mtu mmoja na mwingine yakiwa na lengo na nguvu ya kisheria.

Kuna aina mbili za mikataba ikiwamo ya maandishi na ya maneno. Katika maeneo mengine mikataba pekee inayotambulika ni ya maandishi. Wakati mwingine huwa ni ngumu kuthibitisha uwepo wa mkataba wa maneno hasa makubaliano hayo yanapokuwa hayana shahidi wa kuyathibitisha.

Sheria inasema, ili mkataba uwe halali ni lazima uwe na mambo makuu matano ambayo ni makubaliano, malipo halali, uwezo au uhalali wa kufanya mkataba, hiyari na uhalali wa jambo linalokubaliwa.

Makubaliano yanayofanywa na pande mbili kuhusu jambo fulani ambayo yaweza kuwa ni biashara, kazi au kitu kingine chochote, ni lazima yaridhiwe na kila mmoja kuwa tayari kuwajibika kisheria.

Kutokuwepo kwa nia ya kuwajibika kunayafanya makubaliano yasiwe na nguvu ya kisheria kama mikataba mingine ilivyo.

Malipo halali ni miongoni mwa vitu muhimu kuufanya mkataba utambulike na kutekelezeka kisheria. Malipo halali kisheria yaweza kuwa ni haki, faida, malipo, hasara au majukumu ambayo mtu anatakiwa kupata au kuyatekeleza kwa mujibu wa mkataba.

Hata hivyo, sheria ya mikataba inaeleza endapo kwa nia ya mtoa ahadi, aliyepewa ahadi au mtu mwingine yeyote anapokuwa ametenda au ameacha kutenda…kule kutenda au kuacha kutenda huitwa malipo halali kwa ajili ya ile ahadi iliyotolewa.

Uwezo wa kuingia kwenye mkataba humaanisha mamlaka ya kisheria ya mtu kufanya hivyo. Mtu mwenye mamlaka hayo ni lazima awe na zaidi ya miaka 18, mwenye akili timamu na mhusika katika mkataba huo.

Pamoja na sifa nyingine, ni lazima mkataba ufanywe kwa hiari kutoka pande zote mbili zenye nia ya kuingia katika makubaliano. Mkataba wowote ambao unafanyika pasipo hiari ya mhusika, ni batili.

Licha ya hiyari, mkataba wowote ni lazima ufanyike kuhusu kitu ambacho ni halali kisheria. Mahakama haiwezi kutekeleza mkataba ambao umefanyika juu ya kitu kilicho kinyume na sera za Serikali au kilicho kinyume na maadili ya jamii.