Licha ya changamoto, Bodi ya Mikopo yachanua utekelezaji wa bajeti

Muktasari:

Taarifa za bodi hiyo zinaonyesha hadi Machi mwaka huu, Sh 423.5 bilioni zimetolewa kwa wanafunzi, kiwango ambacho ni zaidi ya asilimi 99 ya Sh 427.5bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mikopo.

Matarajio ya watu ni kuona kile kinachotajwa katika bajeti ndicho kinachofanyika. Vinginevyo kama ahadi hazitetekelezeka, bajeti katika macho ya walio wengi huonekana kama kiini macho.

Katika utekelezaji wa ahadi za bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imejipambanua kama taasisi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyopiga hatua ya kutia matumaini, licha ya ukweli kuwan bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji.

Bajeti ya mikopo kwa wanafunzi

Katika bajeti iliyosomwa na Waziri wa Elimu , Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako Aprili 2018 alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2018 hadi 2019, jumla ya Sh427.5 bilioni zilitengwa kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Wizara kupitia bodi hiyo ilipanga kutoa mikopo ya Sh 427 bilioni kwa wanafunzi wapatao 123,285, kati yao wakiwamo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 40,544 na wanafunzi wanaoendelea na masomo wapatao 82,741.

Mkurugenzi wa elimu, habari na mawasiliano wa bodi Omega Ngole anasema hadi kufikia Machi mwaka huu jumla ya wanafunzi 122, 775 walikuwa wamepewa mikopo ya Sh 423.5. bilioni ambayo ni zaidi ya asilimia 99.

Alisema kati ya wanafunzi hao 41,285 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 81,490 wanafunzi wanaoendelea na masomo.

“Upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wachache waliobaki unaendelea kulingana na taarifa zinazopokelewa,” anasema na kuongeza:

“Utoaji wa mikopo kwa mwaka 2018 hadi 2019 ilikuwa kwa makundi matano ya yatima ambapo jumla ya wanafunzi 1,601 sawa na asilimia 3.5 walipatiwa mkopo, wanafunzi wenye mzazi mmoja ambapo jumla ya wanafunzi 6,673 sawa na asilimia 16.1 walipatiwa mkopo.’’

Kundi jingine ni wenye ulemavu ambapo anasema jumla ya wanafunzi 759 sawa na asilimia 1.8 walipatiwa mkopo, wanafunzi 396 sawa na asilimia 0.9 wa kundi la waliofadhiliwa walipatiwa mkopo na kutoka kaya masikini wanafunzi 31,856 sawa na asilimia 77.1 walipatiwa mkopo.

Ukusanyaji mikopo

Katika eneo la ukusanyaji wa mikopo, Wizara katika hotuba ya bajeti ilipanga kuendelea na utekelezaji wa mkakati wa ukusanyaji wa mikopo iliyoiva na kujiwekea malengo ya kukusanya Sh. 157.7 bilioni.

Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019 bodi imekusanya jumla ya Sh 108 bilioni sawa na asilimia 68.5, huku Ngole akisema ukusanyaji umeimarika kutokana na jitihada mbalimbali zikiwamo kukagua waajiri, kutoa elimu kwa wanufaika na waajiri. Lakini pia anasema kumekuwapo na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.

Jitihada zaidi zahitajika

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Wiliam Ole-Nasha anasema licha ya jitihada zinazofanywa, HESLB inahitaji mikakati zaidi ya kutatua changamoto zinazoikabili ikiwamo ya baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo.

“Kuna hili tatizo la wanafunzi kukosa mikopo, nilichokiona hapa ni kwamba wanafunzi hawana elimu ya kutosha kwani wanakosea kujaza taarifa zao wakati wa kuomba mkopo, kwa hiyo toeni elimu ili kujenga uelewa,” anasema.

Aidha, anaitaka bodi hiyo kuanzisha mfumo mpya wa utoaji mikopo ambao mwanafunzi atapokea fedha moja kwa moja kutoka kwenye akaunti ya bodi ili kuondoa malalamiko ya kucheleweshewa fedha hata pale zinapokuwa tayari.

“Hili litasaidia kumaliza malalamiko ya mara kwa mara, maana mkopo unaingizwa kwenye akaunti ya chuo halafu unakuta kile chuo kinadaiwa na benki kwa hiyo pesa ikiingia wenye deni lao wanakata sasa baadaye unasikia wanafunzi wamekosa mkopo, kumbe bodi haihusiki,”anafafanua na kuongeza:

‘’Pia, kuna tatizo kwa hawa maofisa mikopo katika vyuo mbalimbali; wapo wanaojifanya miungu watu wanafanya kazi bila kufuata utaratibu, wanahusika katika ucheleweshaji wa taarifa za wanafunzi kwa makusudi kabisa kwa hiyo angalieni ni watu wa aina gani mnaowaajiri.