KITABU CHA WIKI: Alichoandika Gaddafi katika kitabu cha kijani Kita

Wiki hii tukiangalie kitabu chenye mafunzo lukuki kilichoandikwa na mwandishi, mwanasiasa na rais wa zamani wa Libya Muammar Gaddaf. Kinaitwa The Green Book au Kitabu cha Kijani.

Kitabu hiki kilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1975 kikitarajiwa kusomwa na watu wote. Inavyoelezwa ni kuwa kitabu hiki ni kama vile kilishabihiana kiasi fulani na misimamo ya Mao. Kitabu kimeandikwa kwa lugha nyepesi, mifano inayoeleweka na kwa aina yake pia na kisichoweza kusahaulika kwa muda mfupi.

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kitabu hiki kilichomwa moto na wale waliokuwa wakimpinga Gaddaf.

Ilikuwa ni lazima watoto wote katika shule za msingi kutumia saa mbili kwa wiki kukisoma kitabu hiki. Baadhi ya sehemu katika kitabu hiki zilikuwa zikiirushwa na runinga, redio na hata kuwekwa katika mabango barabarani ili tu kila mtu aupate ujumbe ulioandikwa ndani ya kitabu hicho.

Kitabu hiki kina sehemu tatu muhimu kama vile njia mbadala au njia za kutatua matatizo yatokanayo na demokrasia, utatuzi wa matatizo au changamoto za kiuchumi, misingi ya kijamaa kwa nadharia ya mataifa yanayoendelea.

Kitabu hiki kinakataa ubeberu, ujima na pia kutumia demokrasia ya kutoka mahala pengine. Badala yake inapendekeza demokrasia ya moja kwa moja ambayo inaangaliwa na kusimamiwa na kamati kuu ya watu/nchi husika, ambapo huruhusu kazi za kijamii, kisiasa kwa watu wote.

Kitabu hiki kinasema kwamba uhuru wa kujieleza ni haki ya kimsingi kwa kila mtu hata kama anafanya kile kisichohitajika kama vile mtu asiyejielewa.

Kitabu cha kijani kinasema uhuru wa kujieleza au uhuru wa habari utategemea na jinsi ya umiliki wa redio, runinga, magazeti, wachapishaji utakavyokuwa.

Kwa kuongezea, kitabu hiki kimeangazia mapinduzi ya kijamii na kupendekeza njia za mtu kuweza kujikomboa kiuchumi na kimaisha na kuangalia njia gani hasa za kumwezesha mtu aliye chini kwa kuweka mipango na mikakati imara kwa watu wote.