Hiki hapa kinachoziponza shule za Zanzibar kuvurunda mitihani

Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yameendelea kutokuwa upande wa shule za Zanzibar.

Wakati matokeo ya mwaka 2018 yakitajwa kuwa na ahueni kwa ufaulu kuipanda hadi asilimia 92.8 kwa kwa daraja la kwanza hadi la tatu, matokeo ya mwaka 2019 yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yanarudisha hisia za simanzi walizonazo wadau wa elimu visiwani humo.

Ni simanzi itokakanyo na ukweli kuwa sio mwaka 2019 pekee; shule za Zanzibar hasa zile zilizopo mikoa ya Unguja kwa miaka zaidi ya mitano zimekuwa zikitamba katika orodha ya shule 10 za mwisho.

Taarifa za Necta, zinaonyesha tangu mwaka 2014 Zanzibar imekuwa ikitoa shule nyingi zilizofanya vibaya. Mwaka 2015 ndio pekee ambao Zanzibar haikuwa na shule katika orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya.

Kwa mujibu wa Necta shule zilizofanya vibaya na miaka yake ni kama ifuatavyo; Mwaka 2014: Ben Bella, Fidel, Mazizini, Al Fallah zote za Unguja na Fidel Castro ya Pemba.

Mwaka 2016: Mpendae, Ben Bella, Tumekuja, Jang’ombe, Kiembesamaki, Al Ihsan Girls na Lumumba zote za mjini Unguja.

Mwaka 2017: Kiembesamaki, Ben Bella, Al Ihsan Girls za Unguja na Chasasa ya Pemba. Mwaka 2018: Jang’ombe na Ben Bella zote za Unguja.

Kutoka shule mbili zilizoingia katika orodha ya shule 10 zenye ufaulu wa chini kabisa mwaka 2018, mwaka huu Zanzibar imeingiza shule nne ambazo ni Haille Sellasie, Tumekuja, Mpendae na Kiembe Samaki A.

Kwa mujibu wa takwimu hizi, mwaka 2016 ulikuwa mbaya zaidi kwa Zanzibar ikiwa imetoa shule saba, ambazo zote zilitoka mjini Unguja. Kwa matokeo haya, wasiwasi unaibuka kuhusu mustakabali wa elimu visiwani humo.

Hali sio nzur hata kidato cha nne

Siyo matokeo ya kidato cha sita pekee, hata katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017, Zanzibar ilishuhudia ikitoa shule sita katika orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya zaidi.

Shule hizo ni Mtule,Langoni, Mwenge S.M.Z , Pwani Mchangani, Kusini, zote za Unguja na Chokocho ya Pemba.

Taarifa za Necta zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2017, mikoa ya Zanzibar imekuwa ikliburuza mkia katika viwango vyua ufaulu kimikoa.

Mwaka 2017 mikoa ya Zanzibar ilishika nafasi kama inavyoonyeshwa kwenye mabano kati ya mikoa 31; Mjini Magharibi (26), Kusini Pemba (28), Kaskazini Pemba (29), Kusini Unguja (30) na Kaskazini Unguja (31). Ufaulu huohuo ukajirudia tena kama ulivyo katika matokeo ya mwaka 2018.

Mjadala wa kitaifa

Baadhi ya wadau akiwamo Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh, wanapiga chapuo kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu hatima ya elimu visiwani humo.

Anasema inawezekana kutofanya vizuri kwa Zanzibar katika miaka yote kunaweza kusababishwa na matatizo ambayo yanaweza kupatiwa ufumbuzi wake iwapo mjadala wa kitaifa utafanyika.

‘’Sitaki kuamini kwamba Wazanzibar hatuna akili, kwa nini wanaotoka kwenda kusoma vyuo vikuu Tanzania bara hufaulu vizuri iweje iwe hapa kwenye shule za sekondari tu bila shaka kuna tatizo’’anasema.

Wakisemacho wazazi

Pamoja na kukubali kuwapo kwa wanafunzi wazembe na wasiojitambua ambao ndio hao wanaofeli, Mzazi Seif Ibrahim anawatupia mzigo wa lawama walimu akidai hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

‘’Kuna baadhi ya shule zinazofanya vibaya kila mwaka, ukichunguza kwa undani kuna upungufu mkubwa wa walimu wenye uwezo tangu madaraja ya chini. Kwa sababu ya upungufu huo wanafunzi huendelea kusonga mbele na kwa kuwa walikosa msingi imara, huishia kufanya vibaya katika mitihani yao ya Taifa, ‘’ anaeleza.

INAENDELEA UK 16

INATOKA UK 15

Kwa upande wake, Saadie Hemedi anasema kitendo cha wanafunzi kutumia simu za mkononi, kinawashughulisha zaidi na masuala ya anasa na kusahau mambo muhimu ikiwamo elimu.

‘’Kwa mfano, leo hii ukitembelea kwenye shule nyingi hapa mjini utakuta wanafunzi wana simu kubwa na za gharama zaidi kuliko wazazi wao kila kinachoendelea huko mitandaoni wanakiona na huiga huko’’anaongeza kusema.

Walimu

Mwalimu Yussuf Issa wa shule ya Mtambile, ananasibisha matokeo mabaya na hoja ya walimu kuwa na maslahi duni. Anasema kama maslahi yangekuwa bora, walimu wasingefikiria kufanya mambo mengine nje ya elimu kama ilivyo sasa.

‘’Leo walimu wengi wamekuwa wajasiriamali na wengine hulazimika hadi kuchukua likizo bila ya malipo ili wafanye shughuli zao nyingine ambazo wanaamini zinawaingizia kipato zaidi’’anasema.

Wanafunzi hawajitambui

Mhitimu wa kidato cha sita, Abdul Azizi Kheri anasema baadhi ya wanafunzi hawajitambui na wala hawaelewi maana ya kuwapo shuleni. Akiwa kidato cha sita anakumbuka namna alivyokuwa akiwaona wenzake wanavyokwenda shule kama watu waliolazimishwa.

Asma Ismai anayesoma shule ya Haile Selasie anasema kuna makosa yanayofaywa na wanafunzi wanapochagua tahasusi za kusomea wanapochaguliwa kujiunga na kidato cha tano. Anasema wapo wanaochagua masomo kwa kufuata mkumbo, hivyo kuja kuwagharimu katika mitihani ya kidato cha sita.

‘’ Utamkuta mwanafunzi amefaulu zaidi ya masomo saba alipokuwa kidato cha nne, lakini akiingia kidato cha tano atachagua masomo matatu tena yale aliopata ufaulu wa alama ya C na kuacha yale aliopata alama ya A au B kwa sababu tu ya kufuata mikumbo,’’ anaeleza.

Wanafunzi na utovu wa maadili

Utovu wa maadili unaweza ukawa sababu nyingine ya baadhi ya wanafunzi kuvurunda kwenye masomo.

Baadhi ya wanafunzi katika shule ya sekondari Fuoni wanasema ni jambo la kawaida kwa wanafunzi kufika shuleni wakiwa na bangi na kuzificha chooni.

Mwanafunzi Abdallah Majid anasema mara kadhaa ameshuhudia wanafunzi wenzake wakivuta bangi vyuooni.

Summaya Kheri anasema wapo wanafunzi wa kike wanaotembea na nguo za nyumbani katika mikoba yao, jambo linalompa shaka kuwa pengine wana

Makambi ya wanafunzi yashindwa kuleta ufaulu mzuri

Wakati maeneo mengine kama Mkoa wa Simiyu, makambi ya wanafunzi yakitajwa kama moja ya chachu za ufaulu, hali haiku hivyo hasa katika Wilaya ya Kaskazini B Unguja. Mkuu wa wilaya hiyo, Rajab Ali Rajab baadhi ya wanafunzi wamegeuza makambi ya wanafunzi kama maeneo ya kujifichia badala ya kwenda shule au kuyatumia kwa ajili ya kujisomea.

Kheri kwa upande wake anasema baadhi ya wanafunzi wanatumia kambi hizo kama maeneo ya makutano na wapenzi wao.

Ripoti ya hali ya elimu

Ripoti ya Hali ya Elimu Zanzibar inakiri kuwapa kwa matokeo ya chini ya kujifunza kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari

Kwa sekondari ripoti hiyo ya mwaka 2016 pamoja na mambo mengine inaeleza kuwa baadhi ya wanafunzi wanaoingia daraja hilo la elimu ni wale waliofeli katika mtihani wa darasa la saba.

‘’ Zaidi ya asilimia 20 ya wanaokwenda sekondari walifeli mtihani wa darasa la saba, na hawana maandalizi ya kutosha ya kulikabili daraja hilo la elimu,’’ inasema sehemu ya ripoti hiyo iliyotayarishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa ushirikiano na Oxford Policy Management Limited.

Aidha, ripoti hiyo inataja baadhi ya mambo yanayochangia kuzorotesha elimu visiwani humo kuwa ni pamoja na walimu wasio na sifa hasa ujuzi mdogo wa lugha ya Kiingereza inayotumika kufundishia sekondari, uhaba wa vyumba vya madarasa na uwezo mdogo wa wazazi kugharimia elimu.

Mikakati ya kukuza ufaulu

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Said Mohamed anasema kufeli kwa shule za Zanzibar kusichukuliwe kama tukio la kipekee, kwa kuwa hali hiyo inatokea maeneo mengi ya nchi.

Hata hivyo, anakiri kuwa kwa upande wa Zanzibar mojawapo ya sababu zinazochangia ufaulu mdogo ni wazazi kuwa na mwamko mdogo wa kufuatilia elimu ya watoto wao.

‘’ Ili mtoto aweze kusoma na kufaulu, kunahitajika mkazo kutoka kwa wazazi wake , jambo ambalo halifanyiki kwa familia nyingi hapa visiwani,’’ anasema.

Kwa kutambua hilo, anasema Serikali imebuni mikakati kadhaa ikiwamo kuzitumia kamati za wazazi shuleni, zitakazokuwa na jukumu la kuhamasisha wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Unguja, Rajab Ali Rajab anasema kuna haja ya kurudisha viboko shuleni ili virudishe ari ya wanafunzi kujituma na kufaulu.

‘’Mbona sisi tumepigwa tukiwa shuleni na tulisoma vizuri, kwa nini leo wanafunzi wasipigwe?’’ anahoji.