Hivi ndivyo mlemavu wa macho anavyoweza kutumia kompyuta

Ni katika banda la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), lililopo katika maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Mtu mmoja wa makamo amekaa akichezea kompyuta, huku watu wakimzunguka na kumshangaa. Ni kawaida kwa Watanzania kushangaa hata vitu vya kawaida, nami naingia katika mkumbo, nasogea ili nikashangae najiuliza kulikoni?

Siamini macho yangu baada ya kumkuta mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Clement Ndahani, akitumia kompyuta kwa ufasaha wa hali ya juu.

Hayupo hapo kimakosa, anakiwakilisha chuo chake kama mtaalamu wa kompyuta akiwa na uzoefu wa kufundisha kwa zaidi ya miaka saba.

Namna ya kutumia kompyuta

Ndahani anasema kompyuta wanazotumia ni za kawaida ila huwekewa programu maalumu inayotoa sauti ya kuongea inayosoma chochote kinachofunguliwa au kubonyezwa. Program hiyo huwapa uhakika watumiaji kuwa sehemu anayobonyeza ni sahihi au la jambo ambalo huwapa urahisi.

Ili mtu asiyeona aweze kutumia kompyuta, kuna hatua kadhaa za kujifunza ambazo Ndahani anataja: “Kwanza huwa tunamfundisha kujua keyboard (kicharazo) ilivyo baadaye atafundishwa mbinu za uchapaji na baadaye ndiyo anaanza kusoma rasmi.”

“Akishajua mambo muhimu sasa ataanza kufundishwa kazi mbalimbali katika kompyuta, kuchapisha kazi zake na hata kuweka rangi kwa sababu kompyuta itakutajia ni rangi gani uliyoichagua,”anafafnua.

Anasema mwanafunzi anaweza kutumia kati ya wiki tatu hadi miezi mitatu kusoma na kuwa na uwezo wa kutuma barua pepe, kutafuta vitu mbalimbali katika mtandao wa google na kujisomea.

Anasema tangu wameanza kufundisha kozi hiyo mwaka 2011 zaidi ya wanafunzi 200 wameshahitimu huku wengine wakiitumia elimu hiyo kutafuta maisha kwa kufungua maduka ya vifaa vya shule na wengine kufanya kazi ya kuhamisha miziki katika simu na flashi.

“Wale waliopo shuleni inawasaidia kusoma kwa sababu masomo mengi yanapatikana huko na vyuo vingine vina mtandao wa kusoma, hivyo kupitia programu hii anaweza kuingia katika mfumo wa chuo kujisomea bila wasiwasi,”anaeleza.

Anasema tangu afanikiwe kujifunza matumizi ya kompyuta, amefanikiwa kusoma shahada ya ustawi wa jamii na hivi karibuni anatarajia kumaliza shahada ya uzamili.

“Mitihani yote natumia kompyuta hivyo ni fahari kuona wenzangu nao wanafanikiwa kama mimi.”

Alivyopata ulemavu

Ndahani alizaliwa akiwa mzima na mpaka anamaliza chuo kikuu mwaka 1982 alikuwa anaona vizuri, lakini alianza kusumbuliwa na presha ya macho mwaka 2007.

Ugonjwa huo ulimfanya kuanza kupoteza uwezo wa kuona taratibu kabla ya madaktari kubainisha kuwa hayawezi kutibika tena.

ilipofika mwaka 2008 alipoteza kabisa uwezo wa kuona jambo ambalo lilibadili mwelekeo wake wa maisha na kumfanya apoteze kazi ya uhandisi taaluma aliyoisomea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Ilikuwa ngumu kwangu kukubaliana na suala hilo, nilijinyanyapaa, nilijiona mpweke kwa sababu siwezi kwenda sehemu nyingine tofauti na ndani wala kupata taarifa yoyote katika magazeti,”anasema na kuongeza:

“Niliyumba sana kiuchumi kwa sababu sikuweza kufanya kazi huku nikiwa na familia ya watoto watano na mke mmoja wanaonitegemea.”

Anasema baada ya kukaa ndani kwa muda mrefu aliamua kujipa moyo na kuanza kutembea tembea ndipo alikutana na wenzake ambao walimshauri kujiunga katika chama cha watu wasioona (TLB) ambao pia waliweza kumpatia mafunzo na kupata fursa ya kuhudhuria warsha mbalimbali.

“Baadaye walinishauri nijifunze maandishi ya watu wasioona nikafanya hivyo, nilijifunza maandishi ya nukta nundu kwa miezi mitatu nikajua kusoma na kuandika,” anasema.

Anasema baada ya kujua kusoma na kuandika alianza kutafuta namna ya kumudu gharama za maisha hivyo aliamua kwenda Chuo cha OUT kuomba kusoma stashahada ya ualimu licha ya kutokuwa na fedha.

‘’Kwa sababu sikuwa na fedha nilishauriwa kutuma barua ya maombi katika chuo hicho ili niweze kuwa mwalimu wa kitengo cha walemavu kama kazi ya muda ili kupata fedha ya kujikimu. Uongozi ulinikubalia na kunipa kazi ya muda katika kitengo cha teknolojia saidizi kwa ajili ya watu wenye ulemavu mwaka 2011,’’ anasema na kuongeza kuwa mwaka huohuo alipata fursa ya kujifunza kompyuta.

Atoa rai

Ndahani anasema walemavu hawapaswi kuchukulia upungufu wao kama kisingizo cha kudumaa na kuacha kufanya kazi. Badala yake wapewe au wautaafute ujuzi utakaowasaidia siku zote.

“Sisi tumejitoa kutoa mafunzo bure kwa watu wenye ulemavu lakini wakati mwingine tatizo lipo kwao, wakija wanategemea wapate fedha kidogo au nauli. Wakati mwingine sisi tunaowafundisha tunakuwa na shida zaidi,”anasema.