Kila shule kulima muhogo ili kuwapa chakula wanafunzi

Handeni. Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe amesema kila shule ya msingi na sekondari kwenye wilaya hiyo inatakiwa kulima eka tatu za zao la muhogo.

Gondwe alisema kilimo hicho kitaondoa tatizo la wanafunzi kukosa chakula cha mchana shuleni, pia kitasaidia kuwafundisha watoto elimu ya kilimo kwa vitendo.

Akielezea mikakati ya kuinua kiwango cha elimu wakati wa Juma la Elimu wilayani humo, Gondwe alisema miongoni mwa mipango ya wilaya yake ni kuhakikisha kila shule inatoa chakula cha mchana kwa ajili ya wanafunzi.

“Tunataka wanafunzi wajifunze kwa vitendo lakini hicho ndicho chakula chao,” alisema.

Aliwataka walimu kutotumia mwanya huo kuwatumia wanafunzi kwa ajili ya kulima mashamba yao.

Gondwe alisema mpango mwingine walio nao kwenye wilaya hiyo ni kila shule kuwa na washauri wawili kwa ajili ya kuwasikiliza wanafunzi na kutatua changamoto zao.

“Hawa watakuwa kama bibi na babu anavyokaa na wajukuu zake, tunataka kuona wanafunzi wanaweza kujieleza na kupewa ushauri vizuri ili baadhi ya changamoto washauri hao waweze kuzitatua,” alisema Gondwe.

Gondwe alitaja mipango mingine ni ukamilishaji wa maboma yakiwamo madarasa, nyumba za walimu na vyoo, kupandisha kiwango cha ufaulu, kampeni ya kupambana na mimba za utotoni inayoitwa ‘Binti Shujaa’ na ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya maendeleo ya elimu.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella alisema mkoa huo kwa ujumla umejipanga kuhakikisha unaondoa sifuri.

“Tunataka kuona wanafunzi hawapati bughudha katika elimu, tumedhamiria kuondoa kabisa sifuri na tumejipanga vizuri,” alisisitiza.

Alisema anaamini kuwa Tanzania ya viwanda haiwezi kufikiwa ikiwa sekta ya elimu itaachwa nyuma.