Maajabu ya shule ya msingi Ludete

Muktasari:

Ina msongamano mkubwa wa wanafunzi, ambapo darasa la nne pekee lina wanafunzi zaidi ya 1400

Mojawapo ya mafanikio makubwa ya mpango wa elimu bila malipo ni ongezeko la wanafuzi wanaoadikishwa katika shule za msingi.

Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo ongezeko hilo limezua majanga kama ilivyo kwa shule ya msingi Ludete iliyopo mkoani Geita.

Kama ni mwitikio wa kuandikisha watoto, huu umetia fora. Wazazi kata ya Ludete katika mji mdogo wa Katoro ilipo shule hiyo, wana kila sababu ya kusifiwa kwa mwamko huo, lakini hali halisi shuleni hairuhusu.

Inaweza ikawa shule yenye rekodi za aina yake mkoani humo na pengine ikawa na sifa ya kuwa shule ya maajabu.

Shule hii ina wanafunzi 6,066, zaidi ya mara tatu ya kiasi cha wanafunzi wanaotakiwa kuwa katika shule moja.

Moja ya maajabu ya Ludete ni kuwa ina wanafunzi 1,480 wa darasa la nne pekee ambao wao tu ni sawa na shule nzima moja au zaidi.

Uongozi wa shule

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Mathias Masalu anasema kutokana na wingi wa wananfunzi wamelazimika kuwagawa katika makundi mawili, ambapo darasa la kwanza, la nne, sita na la saba wanasoma kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 6:20, huku madarasa yaliyobaki wakiingia 6:20 hadi 10:50 jioni .

Shule hiyo mwaka 20017 ilikuwa na wanafunzi zaidi ya 8,000 ambapo kutokana na nguvu za wananchi walitenga maeneo ya ujenzi wa shule mpya na mwaka 2018 wananchi walifanikiwa kujenga shule mpya ya Msufini na hivyo kupunguza wanafunzi 2,840

Jitihada hizo ziliendelea mwaka 2019 kwa wazazi kuenga tena shule nyingine mpya ya Bwawani ambayo ilipelekewa wanafunzi 894, lengo likiwa ni kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi katika shule ya Ludete.

Hata hivyo, juhudi zote hizo hazikufu dafu mbele ya mwitikio wa wazazi, mwaka huu shule hiyo ina wanafunzi sawa na idadi ya wanafunzi wa zaidi ya shule tatu kwa pamoja.

‘’Bado idadi ya wanafunzi inaongezeka kutokana na ongezeko la watu katika mji huu ambapo kwa mwaka huu wazazi wameanza ujenzi wa shule nyingine katika mtaa wa Mji Mwema ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya Ludete,’’ anasema.

Kauli ya uongozi

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Geita Ali Kidwaka anasema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika halmashauri hiyo changamoto sasa sio tu vyumba vya madarasa, bali zinahitajika shule mpya zitakazoweza kupunguza idadi ya wanafunzi katika shule zilizopo.

Anasema mwaka 2019 halmashauri yake ilijenga shule mpya 14 kwa nguvu za wananchi, wadau pamoja Serikali kuu na kwamba mwaka 2020 watajenga shule mpya 31.