Breaking News

Mshangao shule 100 bora kidato cha nne 2019

Tuesday January 28 2020

 

By Halili Letea, Mwananchi

Yalipotoka matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2019 na shule 10 bora kutangazwa, hakukuwapo na shule hata moja ya Serikali.

Inaweza lisiwe jambo la kushangaza kwa shule za Serikali kutokuwamo hasa kwa kuzingatia uzito na ushindani uliopo ili hatimaye shule ijikute katika kundi hilo la ‘dhahabu’’ Ukweli ni kuwa shule nyingi za umma zinakabiliwa na changamoto zinazofanya zipigwe kumbo na shule binafsi.

Hata hivyo, inashangaza zaidi inapotokea shule hizo za Serikali kushindwa kufurukuta hata katika orodha ya shule 100 bora zenye watahiniwa zaidi ya 40.

Hivi ndivyo uchambuzi wa Mwananchi ulivyobaini baada ya hivi karibuni Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kutoa orodha ya shule ya kwanza hadi ya mwisho katika matokeo ya mtihani huo uliofanyika mwaka 2019.

Uchambuzi unaonyesha kati ya shule 100 bora, shule za Serikali zilizojitokeza ni saba pekee. Shule hizo na nafasi yake kwenye mabano ni Tabora boys (28), Ilboru (36) Kibaha (44), Kilakala (51), Mzumbe (55), Msalato (62) na Lumumba ( 98).

Mwalimu mstaafu Bakari Heri anaitaka Serikali kujipanga hasa kwa kuwa ndio mdau mkubwa wa elimu nchini.

Advertisement

‘’ Haileti picha nzuri, shule saba ni chache kwa Serikali. Inasikitisha hata zile tunazoziita za wanafunzi wenye vipaji au kongwe kama Tabora Girls nazo hazimo. Serikali ina wajibu kubadilisha hali ya mambo katika shule zake hasa wakati huu ambao inazifanyia ukarabati mkubwa ,’’ anasema.

Shule za jinsi moja zatamba

Unaweza kusema shule za wanafunzi wa jinsi moja pekee (wavulana au wasichana) ndio zilizofanya vizuri kwenye matokeo ya mtihani huo.

Kati ya shule 100 zilizofanya vizuri zaidi kwenye mtihani huo shule 67 zilikua ni za jinsi moja. Shule za wanawake ndizo zilizoongoza kwa kushika nafasi 39 wakati za wavulana zikiwa 28 na shule mchanganyiko zilikua 33.

Hali ilikua hivyo pia kwenye kumi bora ambapo ni shule mbili pekee zilizokua za jinsia mchanganyiko wakati za jinsia moja zikiwa nane (wanawake 4 na wanaume 4).

Mkurugunzi wa TGNP, Lilian Liundi anasema ufaulu wa shule za zote unategemea zaidi mazingira licha kabla ya kuwa ni shule ya jinsia moja au mchanganyiko. “.. ni rahisi kwa wanafunzi kufanya vizuri zaidi kama itakua na mazingira mazuri hata kama iwe ni mchanganyiko au jinsia moja”.

Lilian aliendelea kufafanua kuwa licha ya haya wadau wa shule za mchanganyiko wanan kitu cha ziada cha kuwafundisha wanafunzi ikiwepo elimu ya uhusiano na namna ya kushirikiana na wenzao ukilinganisha na shule za jinsi moja.

Uchambuzi wa ufaulu kwa mikoa

Ripoti ya Necta inaonyesha kuwa katika mikoa yote 31 iliyopo Tanzania Bara na visiwani ni mikoa 23 pekee iliyofanikiwa kuingiza angalau shule moja kwenye shule 100 zilizofanya vizuri zaidi.

Mikoa wa Kilimanjaro na Mwanza ndiyo iliyoongoza kwa kuingiza shule nyingi (shule 12 kila mmoja) ilifuatiwa na Dar es Salaam Shule 10.

Miongoni mwa shule hizo tatu zilizofanya vizuri zaidi mkoani Kilimanjaro ni Maua Seminary (nafasi ya 9), St Marie Eugenie (29) na St. Joseph Boys’ Science (38) wakati za mkoani Mwanza ni Musabe Boys’ (10) , Nyegezi Seminary (16) na Musabe Girls’ (27).

Mikoa mingine iliyoingiza shule nyingi kwenye 100 bora ni Pwani (shule 9), Arusha (7), Morogoro na Kagera shule 6 kila moja.

Mikoa saba ilikua na shule moja kila moja. Mikoa hiyo ni Mjini Magharibi, Mtwara, Njombe, Rukwa, Shinyanga, Simiyu na Tabora.

Shule ya kwanza Mjini Magharibi ni shule ya Sekondari ya Lumumba iliyoshika nafasi ya 98 kitaifa, Wakati kwa mkoa wa Mtwara ni Shule ya Abbey iliyoshika nafasi ya 42.

Shule ya Umawanjo ya mkoani Njombe ilishika nafasi ya 75 kitaifa, Rukwa ni shule ya Santakagwa iliyokuwa ya 97 kitaifa, Simiyu ni shule ya St. Aloysius nafasi ya 20, Shinyanga shule ya Queen of Family nafasi ya 52 na Tabora ni Tabora Boys’ iliyoshika nafasi ya 28 kitaifa.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira anasema mkoa huo unafanya vizui licha ya kuwa na changamoto nyingi kwa kuwa wanatumia vizuri rasilimali chache walizo nazo.

Alizitaja rasilimali hizo ni kama walimu ambapo alisema, “Tunafanya semina za walimu mara kwa mara kwa kuwatenganisha kwa kabu mbalimbali za masomo lakini pia zawadi kwa wale wanaofanya vizuri”.

Mghwira alizitaja sababu nyingine ni ushirikiano wa wazazi kwenye kufuatilia maendeleo ya watoto na kuchangia suala la chakula pamoja na kuandaa idara za masomo kwa wanafunzi ambapo hukutana na kushirikiana kwa mambo mbalimbali kama masomo, michezo na Tehama

‘’ Katika kila mkutano wa hadhara na ile ya redio na mitandao, lazima nizungumzie elimu, lishe na mifumo yetu ya ufanyaji kazi kutokana na umuhimu wake,’’ anasema.

Mikoa nane haikua na shule hata moja kwenye 100 bora

Mikoa nane, minne ya Tanzania Bara na minne ya Visiwani Zanzibar haikubahatika kuingiza hata shule moja kwenye shule 100 zilizofanya vizuri. Mikoa hiyo ni Katavi, Manyara, Lindi, Songwe, Kaskazini na Kusini Pemba, Kaskazini na Kusini Unguja.

Shule ya kwanza mkoani Katavi ni Utende iliyoshika nafasi ya 580 kitaifa, wakati Shule ya iliyongongoza mkoani Manyara ilikua ni shule ya Genda iliyokua ya 272 kitaifa.

Shule ya Wama ya wasichana iliyoongoza mkoani Lindi ilikua ya 260 kitaifa na Shule ya James Sangu ya mkoa wa Songwe ilikua ya 127 kitaifa.

Katika visiwa vya Kaskazini unguja shule ya sekondari ya Kidoti iliyoongoza ilikua ta 1,310 kitaifa, Shule ya Pemba Islamic iliyokua ya kwanza kaskazini Pemba ilishika nafasi ya 558, Shule ya Maahad ya Kusini Unguja ilikua ya 543 kitaifa wakati shule ya kwanza Kusini Pemba, Chekecheke ilikua ya 540 kitaifa.

Advertisement