Uhaba wa walimu, kilio kinachowaumiza wengi

Muktasari:

  • Serikali yaagiza walimu wa sekondari kuhamishiwa msingi kunusuru upungufu kwenye shule za msingi ambazo zina hali mbaya zaidi.

Karibu kila taarifa ya mkuu wa shule iwe ya msingi au sekondari iliyosomwa katika maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) wilayani Handeni mkoani Tanga ilitaja uhaba wa walimu.

Uhaba huo wa walimu ni kati ya changamoto kadhaa zinaoikumba wilaya ya Handeni ambayo inaundwa na halmashauri mbili ya mjini na vijijini.

Zaidi ya asasi zisizo za kiraia 20 zinazounda Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) ziliweka kambi katika wilaya hiyo kwa lengo la kuchambua changamoto zinazokwamisha utoaji wa elimu bora na kuzitafutia suluhisho.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chanika, Elinisafi Msuya anasema kutokana na uhaba mkubwa wa walimu uliopo shuleni kwake, wanafunzi 328 wa darasa la awali wanaotakiwa kufundishwa na walimu 13, wanafunzishwa na mwalimu mmoja.

“Idadi ya wanafunzi wa darasa la awali ni sawa na mikondo 25 inayohitaji walimu 13, hivyo upungufu kwenye darasa hili peke yake ni walimu 12,” anasema Msuya.

Msuya aliyekuwa akizungumza katika uwanja wa shule hiyo, anasema elimu maalumu shuleni hapo inakabiliwa na uhaba wa walimu watatu.

Anaema wanafunzi 30 wenye ulemavu mbalimbali wanaosoma shuleni kwake wanahitaji walimu sita kukidhi mahitaji ya ufundishwaji lakini waliopo ni watatu tu.

Kwa upande wake, Mwalimu wa elimu maalumu katika shule hiyo, Omary Kigwamba anasema kulingana na mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu, idadi ya walimu wanaokuwepo inapaswa kulingana na idadi ya wanafunzi ili kumsaidia kila mtoto.

“Darasa la kwanza mpaka la saba kuna walimu 18 na upungufu ni walimu 16 na kwenye darasa la ufundi hakuna mwalimu kwa sababu aliyekuwepo amestaafu,” anasema Msuya, mwalimu mkuu wa shule hiyo.

Wakati Msuya akilia na upungufu wa walimu kwenye shule yake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisaza katika wilaya hiyo, Leonard Mshana anasema mahitaji zaidi yapo kwa walimu wa masomo ya sayansi.

“Japo shule hii haina maktaba kwa ajili ya wanafunzi na walimu, tunakabiliwa na uhaba wa walimu wa masomo ya biolojia na kemia,” anasema mwalimu Mshana.

Katika hotuba yake mwalimu wa Shule ya Msingi Kitumbi, Mary Mwangu aliyoisoma akimwakilisha mkuu wa shule hiyo, anasema wanakabiliwa na upungufu wa walimu tisa japo walimu 10 waliopo shuleni hapo wanajitahidi kuhakikisha vipindi vyote vinafundishwa.

“Tuna madarasa saba kati ya 19 yanayohitajika kwa sababu idadi ya wanafunzi waliopo shuleni hapa ni 842. Pia tunachangamoto ya vyoo vya walimu,” anasema Mwangu.

Mwalimu mkuu mwingine anayeelezea uhaba wa walimu shuleni kwake ni Eliakim Kipele, kutoka Shule ya Sekondari Kileleni ambaye anasema uhaba wa walimu wa sayansi ni kati ya changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Mbunge wa Handeni Vijijini Mboni Muhita, anasema jimbo lake linakabiliwa na upungufu wa walimu zaidi ya 600.

“Nikisema Handeni vijijini namaanisha ni vijijini kweli, hata sisi tunatamani siku moja wilaya yetu iwe kinara wa ufaulu lakini kwa upungufu huu wa walimu mmmh! sijui kama tutafika,” anasema Mboni na kuongeza;

“Sio walimu tu, tunachangamoto ya miundombinu, nyumba za walimu hata hivyo, nawapongeza walimu kwa kufanya kazi yao vizuri,” anasema.

Wakati Mboni akisema upungufu mkubwa zaidi wa walimu kwenye jimbo lake upo katika shule za msingi, Mbunge wa Handeni Mjini Omary Kigoda anasema jimbo lake linahitaji walimu 45 wa somo la hisabati.

“Mbali na hao 45 wa hisabati, tuna upungufu wa walimu 150 wa shule za msingi kwenye jimbo langu na nilishatoa Sh24 milioni kusaidia ujenzi wa miundombinu kwa sababu wananchi wamehamasika kuchangia maendeleo,” anasema Kigoda.

Agizo la Serikali

Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi anayeshughulikia elimu, Tixon Nzunda anasema Serikali inashughulikia tatizo la uhaba wa walimu.

Anatumia fursa hiyo kuziagiza halmashauri za wilaya ya Handeni kupunguza pengo la walimu kwa kuwahamishia shule za msingi walimu wa shule za sekondari.

“Kwa hiyo mpunguze pengo la walimu kwa kuwahamisha walimu kutoka shule za Sekondari, kuna fedha za ‘tekeleza kwa matokeo’ tulishazileta, hizi zitumike kwa kazi hiyo,” anasema Nzunda.

Anasema shule za sekondari zina ziada ya walimu 10,000 wa masomo ya sanaa wakati shule za msingi zinakabiliwa na uhaba wa walimu hao.

Ofisa elimu (Msingi) wilayani Handeni, Omary Mashaka anasema uhamisho wa walimu utafanywa zaidi wakati huu wa likizo ili kuziba sehemu zenye uhaba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe anasema wilaya hiyo inajitahidi kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kulingana na rasilimali zilizopo.

Anasema kati ya mwaka wa fedha 2015/2016 na 2018/2019 zaidi ya Sh2.2 bilioni zimetolewa na Serikali kwa ajili ya sekta ya elimu wilayani humo.

“Kila mbunge kwenye jimbo hili (Muhita na Kigoda) ametoa sio chini ya Sh20 milioni kwa ajili ya sekta ya elimu,” anasema Gondwe.

Mwakilishi wa Tenmet na Mkurugenzi wa Taasisi ya Hakielimu, Dk John Kalage wanasema ongezeko la bajeti ya elimu linaweza kutatua changamoto nyingi zinazojitokeza.

Anasema ili bajeti ya Serikali inayotengwa kwenye sekta hiyo ikidhi mahitaji inapaswa isiwe chini ya asilimi 20.

Waanzisha uchangiaji

Godwe anasema katika kupambana na changamoto ya miundombinu wameanzisha mtindo wa msalagambo (uchangiaji) ambao kila Jumamosi wananchi hushiriki katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.

“Kupitia msalagambo ujenzi wa madarasa umefikia asilimi 90 kwa sababu wananchi wamekuwa wakijitolea na Serikali inaongeza nguvu,” anasisitiza.

Mjumbe wa Tenmet, Clement Mganga anasema sababu za asasi za kiraia kuchagua wilaya ya Handeni ni mafanikio waliyonayo kwenye eneo la elimu jumuishi.

Elimu jumuishi ni ile inayowaunganisha wanafunzi wenye ulemavu na wasio na ulemavu katika darasa moja. Anasema mashirika yasiyo ya kiserikali yapo tayari kusaidiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu.