Vishkwambi kuwakomboa watoto mbumbumbu mkoani Tanga

Wednesday July 31 2019

 

By Hadija Jumanne,Mwananchi [email protected]

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni(Unesco) ya mwaka 2013 inaonyesha kuwa dunia ilikuwa ana watu milioni 774 wasiojua kusoma na kuandika. Idadi kubwa ya watu hao wanaishi katika bara ya Afrika na Asia

Hapa nchini, hadi kufikia mwaka mwaka 2015 idadi ya wanaojua kusoma na kuandika ilifikia asilimia 77.

Licha ya Serikali kukabiliana na changamoto ya watoto wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu, bado tatizo hilo lipo hasa katika wilaya za pembezoni.

Vishkwambi na vita dhidi ya mbumbumbu

Hali hii ndio iliyoisukuma taasisi ya Xprize Foundation ya nchini Marekani, kupitia mradi wa Xprize, kuanzisha program maalumu kwa ajili ya watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Katika programu hiyo, watoto wanafundishwa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kupitia teknolojia ya vishkwambi (tablets).

Advertisement

Wanufaika kwa sasa ni watoto wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 11 katika wilaya saba za Mkoa wa Tanga walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Mwakilishi wa Unesco nchini, Tirso Dos Santos anasema mradi huo unalenga kutatua matatizo ya kujifunza, kuandika na kuhesabu kwa watoto waliopo nje mfumo rasmi wa elimu.

“ Mradi huu ni wa majaribio wa miezi 15 na unatarajia kukamilika Septemba 2019, umelenga watoto wenye umri huo kuwapatia elimu ya kusoma, kuandika na kuhesabu kupitia programu ya Kiswahili katika vishkwambi” anasema Dos Santos.

Dos Santos anasema mradi huo unatekelezwa katika wilaya saba za mkoa wa Tanga, ambazo ni wilaya ya Handeni, Korogwe, Lushoto, Muheza, Mkinga, Pangani na Kilindi.

Anasema, mradi huo unaotumia ubunifu wa teknolojia unafanyika kwa ushirikiano wa Unesco, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tamisemi.

Anasema vishkwambi hivyo vinachajiwa kwa kutumia nishati jadidifu ya jua katika maeneo maalumu yaliyotengenezwa kwa ajili ya kuzichaji.

“ Katika utoaji elimu kwa watoto hawa, watajifunza kwa kutumia program tano zilizowekwa katika kishkwambi zitakazomuwezesha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu” anasema Dos Santos.

Anasema mradi utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu utakuwa umewafikia wanafunzi zaidi ya 2,500 katika vitongoji 141 vinavyofanyiwa mradi huo wa majaribio.

Sababu ya kuanzisha mradi huo mkoani Tanga

Mkuu wa kitengo cha elimu Unesco, Faith Shayo anafafanua kuwa stadi mbalimbali zifanyika kuangalia takwimu za watoto ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa elimu.

“ Mradi huu unawapa nafasi watoto ambao hawakuwahi kujiunga na shule ya msingi, kupata fursa nyingine ya elimu,’’ anasema.

Anasema ripoti ya Unicef ya mwaka 2016, inaonyesha kuwa watoto milioni tatu na nusu wapo nje ya mfumo usio rasmi wa elimu Tanzania.

“ Tulitumia takwimu za elimu kuangalia takwimu za mikoa ambayo haifanyi vizuri katika elimu” anasema Shayo .

“ Baada ya jopo kukaa, liliamua mradi huo upelekwe katika mkoa wa Tanga, kwa sababu mradi huu unaenda kuhusisha ngazi ya kijiji na vitongoji” anasema.

Mradi huo unatoa changamoto kwa timu ya wabunifu kuwezesha watoto walio na fursa ndogo ya kuingia katika elimu darasani kujifunza stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kutumia vishkwambi wakijifunza wenyewe.

“ Mradi huu unaendana na majukumu ya Unesco ya kuhamasisha elimu jumuishi katika kuhakikisha kwamba watoto wote wa Tanzania wakiwamo wa jamii za pembezoni na zilizo nyonge zinapata fursa ya elimu” anasema Shayo.

Namna vishikwambi vinavyofanya kazi

Shayo anasema wametoa mafunzo kwa vijana 10 ambao wanajua Tehama, ili waweze kuwafundisha na kuwasiadia mwanafunzi pindi vishkwambi hivyo vinapoharibika au kukwama kufanya kazi

“Mbali na kulipwa mshahara, vijana hawa tumewapatia pikipiki kwa ajili ya kuhakikisha wanafika kila kata yenye wahusika na kuongea nao kama kuna changamoto zozote” anaongeza.

Advertisement