Juma Kakere : Hawezi kumsahau Sintah alivyoipaisha Pole kwa Safari

Saturday May 11 2019

 

By Rhobi Chacha, Mwananchi

Wapenzi wa muziki wa dansi wanaukumbuka sana wimbo wa ‘Pole kwa safari’ wa Juma Kakere ulivyobamba na hasa video yake iliyonakshiwa na staa wa zamani wa kundi la sanaa la Kaole, Christina Manongi a.k.a Sintah.

Wimbo huo bado unabamba vilivyo masikioni mwa mashabiki wa miondoko hiyo, ulimpa jina kubwa Kakere ambaye anaeleza mengi ikiwamo kukiri video hiyo ilivyompa ulaji ndani na nje ya nchi.

Kakere anasema wimbo huo ulimpatia umaarufu kwa wadau wa muziki wa dansi na watu wengine, na wala hakutarajia kama ungepokewa kwa staili hiyo.

“Kwanza nashukuru kwa kuniuliza hili swali, ambalo sikuwahi kulielezea, Pole kwa safari ni wimbo ulioniongezea umaarufu kwa wapenzi na wadau wa muziki na burudani, video yake ilipendwa sana ilinisaidia kupata shoo nyingi mno,” anasema Kakere.

Anamtaja Sintah na mvuto wake ulichangia kuupa mafanikio, licha ya ujumbe mzuri uliopo katika ngoma hiyo iliyotoka mwanzoni mwaka 2000.

Kulikuwa na taarifa Kakere ameachana na fani ya muziki, lakini amesisitiza kuwa bado yupo sana na bado hajakaa kimya kama inavyofikiriwa.

Anasema sasa anamiliki vyombo vyake vya muziki na huwa akiwa na kazi ya shoo anawakusanya baadhi ya wanamuziki wanapiga kazi.

“Sijaacha muziki, naendelea kuimba na kutoa kazi kama kawaida, tena kwa sasa namiliki vyombo vyangu vya muziki na napiga kazi kama kawaida,” anasema na kuongeza mbali na Pole kwa Safari na Betty ambazo ndio nyimbo maarufu zilizowahi kubeba pia albamu zenye majina hayo, lakini pia alishatoa Watu Fulani na Kimbembe ambazo hata hivyo, hazikubamba sana.

“Baada ya hizo nilitulia na kuangusha moja moja na mwaka jana tu nimefyatua Happy na Kaa la Moto ambazo ziko YouTube,” anasema mkongwe huyo.

Mkali huyo anafichua kuwa utunzi wa nyimbo alianza mwishoni mwa miaka ya 1970 akishirikiana na kaka yake ambaye sasa ni marehemu, Belesa Kakere aliyetamba na bendi za Dar International, (Vijana Jazz, hakukaa sana), Juwata Jazz (Msondo Ngoma) na Bima Lee na ndiye aliyemtia moyo baada ya kusikia tungo zake.

“Kitu ambacho wadau wengi wa muziki wa dansi hawakifahamu ni kuwa mimi ni utunzi nilianza 1978-79.Belesa alikuwa mkubwa sana, ndiye chachu kubwa iliyonifanya kuendelea kutunga kwani yeye ndiye mtu wa kwanza kusikia tungo zangu na kwa jinsi alivyoshangaa uwezo wangu na kunitia moyo ndivyo nilivyozidi kuendelea katika utunzi.

Kuhusu dansi kudoda na kipi kifanyike, Kakere anasema; “Hali ya muziki wa dansi si nzuri kwa sasa na inahitajika juhudi kubwa za wadau wote. Mazingira ni tofauti na ya zamani. Kunahitajika mtazamo wa kibiashara ya muziki miongoni mwetu wanamuziki na wafanyabiashara ya muziki (burudani) na wamiliki wa vyombo vya habari.

“Hivyo inahitajika wanamuziki tutambue hilo na kufanya ambavyo soko linataka. Nyimbo bora katika mifumo ya kiteknologia ya kisasa, kufanya kama biashara nyingine katika kanuni za matangazo, brandi na kutumia ipasavyo mitandao ya kijamii. Lakini iambatane na kusikika na kuonekana nyimbo zetu bila kubaguliwa.

Alipoulizwa kama vyombo vya habari vinachangia kuuangusha muziki huo, anasema; “Sina hakika, ila kungekuwa na televisheni na Redio zenye kurusha muziki wa dansi muda wote, wafanyabiashara na wadhamini wa kuandaa matamasha mengi ya dansi ni wazi hali isingekuwa hii ya

Mpaka sasa Kakere amepakua albamu tatu za Betty, Remmy na Pole kwa Safari, kila moja ikiwa na nyimbo sita na baadhi yake ni Catherine, Ndoa ya Lazima, Mtoto Mridhawa, Mimi Mwanamuziki na Mambo ya Kiswahili.

“Albamu ya Betty ni ile niliyoitoa mwaka 2000, ile ya Pole kwa Safari ni ya 2004 ikiwa na nyimbo kama Mama Monica, Queen Misifa, Fadhili ya Punda, Remmy na Mary. Nyimbo zote kwenye albumu hizi mbili nilizitunga miaka mingi zaidi ya 10 nyuma,” anasema.

Advertisement