USHAURI WA DAKTARI: Mambo mengine yanayosaidia moyo kufanya kazi vizuri-2

Wiki iliyopita tuliona mambo mbalimbali ikiwamo vyakula, mazoezi na kuepuka matumizi ya sigara ambayo yakifanyika yana faida kubwa kwa afya ya moyo. Leo tunaendelea sehemu ya mwisho.

Wapo baadhi ya watu hawafahamu kama pombe si rafiki mzuri wa moyo. Baadhi hudhani kuwa kunywa pombe kali kunakata mafuta ya mwili hivyo kufanya hivyo wanaepuka magonjwa ya moyo.

Zipo tafiti zinazoonyesha kuwa unywaji wa glasi moja kwa siku ya mvinyo mwekundu unaimarisha afya ya moyo. Ingawa bado sishauri moja kwa moja mtu kuufanya mvinyo kama hatua ya kujikinga.

Unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kusababisha kupanda kwa msukumo wa damu, kuongeza kiwango cha mafuta katika damu na vilevile huchangia moyo kushindwa kufanya kazi.

Ni kweli wanadamu huchukulia kunywa pombe ni sehemu ya burudani ndiyo maana ni vigumu kukataza unywaji wa pombe katika jamii. Pale mtu anaposhindwa kuacha kunywa pombe basi anywe kwa kiasi kwa kutozidisha glasi moja kwa mwanamke na mwanaume asizidishe mbili kwa siku.

Pia, ieleweke kuwa pombe kali zina kiasi kikubwa cha kilevi, kuzitumia kupita kiasi zinachangia zaidi kuharibika kwa mishipa ya damu ikiwamo ile ya moyo.

Nashauri kwa mtu ambaye hajawahi kunywa pombe ni vizuri asijaribu kuanza kutumia.

Kabiliana na magonjwa yanayozorotesha afya ya moyo ikiwamo msukumo wa damu, kupanda kwa kiwango cha lehemu mbaya (bad cholestrol) na kisukari.

Mgonjwa mwenye matatizo haya anatakiwa kushikamana na matibabu na ushauri kwani magonjwa haya yanaongoza kwa kuharibu mishipa ya damu.

Ni vizuri kuwa na vifaa tiba nyumbani ikiwamo kipimo cha kupima kiwango cha sukari katika damu na mashine ya kupima shinikizo la damu.

Vipimo hivi vinakuwezesha kujua endapo matatizo haya yanazidi au yanapungua hivyo kukusaidia kuwahi kufika katika huduma za afya au kumjulisha daktari wako mapema kwa ajili ya matibabu na ushauri.

Kabiliana na shinikizo la akili kwani uwepo wa tatizo hili mwilini husababisha mabadiliko hasi ya hisia pamoja na kusababisha kupanda kwa mapigo ya moyo na vijeraha katika kuta za mishipa ya damu.

Mtu mwenye shinikizo la akili au msongo wa mawazo hujikuta akijitumbukiza katika unywaji pombe, uvutaji sigara na dawa za kulevya.

Wengi hudhani kuwa mambo haya yanawapunguzia shinikizo la akili au msongo wa mawazo (stress) kumbe vitu hivyo vinaongeza hatari ya kupata matatizo ya moyo zaidi.

Njia sahihi kiafya za kukabiliana na shinikizo la akili ni pamoja na kusikiliza muziki, kucheza michezo midogomidogo, kutembea, kutazama burudani mbalimbali, kuongea na kupata ushauri kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Fahamu matatizo ya kiafya yanayowasumbua ndugu zako wa damu, kwani baadhi ya matatizo ya moyo yanahusishwa na kurithi chembe za urithi zenye hitilafu na mitindo ya kimaisha.

Kuyajua matatizo hayo inakufanya kuchukua tahadhari na namna ya kujikinga nayo mapema zaidi.

Mbinu ya mwisho ni kuhakikisha unabakia katika uzito ambao ni salama kiafya, hakikisha kuwa unapima mara kwa mara uzito wa mwili.

Ili kuwa kujua upo katika uzito wa kawaida zao la uwiano wa uzito na urefu wa mwili (Body Mass Index) unatakiwa kuwa kati ya BMI 18.5-24.9.