Mambo ya kufanya miezi sita kabla ya siku ya harusi

Kawaida mpaka watu mnafikia hatua ya kufunga ndoa kumekuwa na makubaliano ya muda mrefu huku wengi ikiwa haipungui mwaka mmoja.

Pia harusi nyingi huwa na maandalizi ya muda yanayokwenda sambamba na uundaji wa kamati za maandalizi pamoja na mambo mengi zitakuwa na jukumu la kusimamia ukusanyaji michango.

Kabla ya kufika huku maharusi kwa umoja wao kuna vitu wanatakiwa kuvipanga miezi sita kabla ya harusi.

Miongoni mwa vitu hivyo ni pamoja na kuchagua tarehe na siku ya kufanya shughuli yenu. Pia mnapaswa kufahamu mnataka kufanya harusi ya aina gani na bajeti yake ni kiasi gani, itafanyikia wapi kanisa, msikitini, nyumbani, uwanjani ua ufukweni. Kadri miezi inavyopungua nanyi mnapaswa mwende sambamba nayo, ikibaki miezi mitatu kabla ya hafla au ndoa mliyokubaliana kufanya ni wakati wa kuchagua nguo, kutuma kadi kwa waalikwa kwa ajili ya michango au mialiko.

Wakati huu pia ni mzuri kuangalia washereheshaji mbalimbali, wapiga picha, watu wa chakula na muziki, ukienda katika sherehe unaangalia au kusikiliza nani anafaa ili nawe uje umtumie katika hafla au shughuli yako.

Hawa ni watu muhimu hivyo hupaswi kukurupuka, unatakiwa ujue kazi yao kwa kuiona badala ya kuambiwa.

Miezi miwili iliyobaki maharusi hapa sasa mnaweza kwenda kuchagua pete, kuchagua gari litakalotumika kuwabeba na yale yatakayobeba wazazi.

Mpaka kufikia hapa kutakuwa tayari kuna kamati ambazo zitakuwa na majukumu ya kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa, hivyo jukumu lenu ni kuwapa kile mnachoona kinafaa.

Mtakuwa mnajua mtafanyia wapi hafla au ndoa yenu, mtavaa nini, pete zenu ziko wapi, mtabebwa na gari gani, mtakaa hoteli ipi nani ataongoza shughuli yenu. Hivyo itakuwa kazi rahisi kwa kamati husika kufuata kile mlichokifanyia utafiti kwa miaka mitatu mpaka sita kabla ya kukamilisha tukio hilo muhimu maishani.