ANTI BETTIE: Mke wangu hanisisimui baada ya miaka minne ya ndoa

Sunday January 19 2020

 

Habari! Nimeoa huu mwaka wa nne. Lakini sifurahii penzi kama zamani, sisimki hata akikaa mbele yangu bila nguo, hata mke wangu naye nikimtizama hafurahii penzi langu na kuna wakati anakereka hata akiniona.

Nifanyeje?

Pole sana. Kuna kitu kimebadilika katika mahusiano yenu ambacho hujakijua bado. Rudisha mawazo nyuma, kumbuka mlikuwa mkifanya nini siku za mwanzo za penzi lenu.

Ukikumbuka utaona kuna tofauti kubwa, inawezekana majukumu ya familia yameongezeka hivyo kupunguza muda wa kufanya baadhi ya mliyokuwa mkiyafanya wakati ule, lakini kumbuka penzi ni kama ua ili listawi na kuwa katika mwonekano wa kuvutia linahitaji kumwagiliwa.

Kumwagilia penzi maana yake kufanya yatakayolifanya liwe jipya siku zote. Jiulize mara ya mwisho kulala hotelini na mkeo lini, kumnunulia, kununuliana zawadi, kutoka kwa ajili ya matembezi, kulishana na hata kumbusu mkiwa sebuleni?

Inawezekana mlikuwa mnasuguana mgongoni mkioga, yaani kuoga wote bafuni, mnakatana kucha, mnakumbatiana, mnapika pamoja jikoni, yote mmeyaacha, kibaya zaidi hata mnapotaka kujadili masuala yenu binafsi mnafanya hivyo wakati wa kulala.

Advertisement

Mara ngapi mnaanzisha mazungumzo na kabla hamjafikia muafaka mmoja wenu anakuwa amelala, unadhani hapo hata ukitekenywa utastuka ilihali unaamini anakudharau wewe unazungumza yeye analala. Unasahau kitandani si mahala pa mijadala ni mahala pa kubembelezana ili mpate usingizi.

Anzia hapa, kama umebadili sana mfumo wa maisha yenu urudishe kama ulivyokuwa awali, naamini mtafurahia penzi lenu.

Pia jipe muda wa kupumzika pamoja naye, kama kuna kazi nyingi za nyumbani angalia namna ya kumpunguzia bila shaka atakufanya uwe na furaha kwa sababu atakuwa na nuru ya mke umpendaye au uliyempenda.

Nimfanye nini mume wangu apunguze kuzungumza kama kinanda?

Nikiri kuwa ninampenda mume wangu. Tatizo linalonifikirisha nipumzike kuwa naye ni mdomo. Anazungumza kuliko watangazaji wa michezo. Huwa najaribu kuwasikiliza wanaume wengine akiwamo baba, kaka, shemeji na wajomba zangu hawana tabia hii.

Kibaya zaidi kuna mada anakurupuka kuzichangia ilihali hazijui.

Nifanyeje, kuna siku ni aibu mbele za watu?

Katika mahusiano hususani ya ndoa ambayo yakivunjika huwachukiza wengi, dawa ni kusemezana na kupata jibu la pamoja, mwambie hufurahishwi na tabia yake.

Ili aone kosa lake, fanya hivyo siku ambayo amezungumza na hilo jambo limeleta sintofahamu miongoni mwa watu mliokuwa nao, au akianza kuzungumza kama kasuku.

Advertisement