ANTI BETTIE: Hatamani tena kuwa faragha kama zamani, nimekosea wapi

Sunday May 12 2019

 

Nimeolewa huu mwaka wa pili, mwaka mmoja na miezi miwili baada ya ndoa nilibaini mume wangu hana hamu na penzi langu wala kuwa karibu nami.

Nifanyeje?

Mke wa mtu

Tanga

Kama alikuwa na hamu na wewe siku za nyuma jiulize wa nini hana hamu tena. Inawezekana kuna kitu unakosea mnapokuwa faragha. Hakikisha unabadili aina ya mandhari, acha kufanya mazoea huenda mwenzio amechoka. Jifunze aina mpya, mfanyie mshituko faragha, jiachie ukiwa faragha, mhamasishe hata akichoka. Akikataa hakikisha anakubali kwa kufanya kile unachoamini anapenda kufanyiwa akiwa faragha.

Nimemsotea kwa miaka sita

Huu ni mwaka wa sita nahangaika kumuonyesha hisia zangu kijana ninayempenda , lakini hajaona wala kustuka.

Nifanye nini ili atambue nampenda?

Nikita

Masasi

Nikita unaniangusha. Miaka sita unasotea penzi? Hata enzi za zamani hawakuchukua muda wote huo. Mwambie ukweli ni jinsi gani unamzimia ili ajue jinsi ya kukusaidia. Kukaa kimya kunaweza kumpa mwanya mtu mwingine mwenye nia kama yako akafanikiwa kuibuka naye.

Nyumba ndogo siyo dili

Nina nyumba ndogo kwa muda mrefu sasa. Nimeisomesha lakini siku za hivi karibuni naona kama inataka kunikimbia.

Nifanyeje?

Mrisho

DSM

Kama ni nyumba ndogo jipange jinsi utakavyokwepa kukimbiwa. Huyo naye ana akili zake timamu. Anafahamu ipo siku utamuacha na kurudi kamili kwenye familia yako, ndiyo maana ameamua kuchukua tahadhari kwa kuwa mbali nawe.

Tafakari kuhusu hili, una sababu gani ya kuwa na nyumba ndogo? Kama kuna vitu mkeo hakutimizii, mwambie ili ajirekebishe kuliko kuongeza matatizo na uwezekano wa kupata maradhi kirahisi kwa kuwa na mtu usiyeweza kumlinda kutokana na kugawa muda kwako na kwa familia yako.

Advertisement