ANTI BETTIE: Kuna wakati nikiwa faragha hisia zangu huja na kupotea

Monday December 9 2019

 

Nina umri wa miaka 44 ambao unasemekana ndiyo hasa ukiwa faragha unahisi raha kwelikweli. Lakini kwangu ni tofauti, kuna kipindi napata hisia na ninafurahia tendo hilo hasa, lakini kuna wakati hisia hupotea kabisa.

Nifanyeje?

Kama ambavyo umesema mapenzi ni hisia. Achana na umri na wala usifikiri kwa kuwa una miaka 44, basi hata usipoweka mawazo yako kwenye tendo unalofanya utafurahia tu. Lazima utulize akili na mawazo yako yote yawe katika eneo la tukio, pia huyo uliyekuwa naye umpende kwa dhati ndiyo hisia zitadumu. Jambo lingine unatakiwa umpate anayekujulia kwa kumueleza au yeye kukutafuta, tofauti na hapo utakuwa na miaka 40 inayoelezwa hasa ndiyo unaanza maisha ikiwamo kufurahia faragha na usipate unachotarajia kwa sababu ili ufurahie hilo tendo kuna vitu vingi vinahusika ikiwamo utulivu wako pia.

Faragha ni eneo la raha, jipe raha kwanza kwa kujiandaa kimwili na kiakili hayo mengine yatafuata, ukitegemea umri basi ukishikwa kidogo uwe tayari mwanakwetu utasubiri na hutapata kitu.

Andaa mazingira ya kupata unachotaka au watoto wa mjini wanasema jibebishe kimahaba upate raha ya huba.

Akinipa tunda, ninakwenda kujitambulisha

Advertisement

Anti habari! Nina miaka miwili namlainisha msichana akubali kuwa mpenzi wangu ili niende kwao kujitambulisha.

Mwanzoni alianza kunikubali, lakini siku hizi amebadilika hataki hata kukutana na mimi mahali kwa ajili ya mazungumzo tu.

Nifanyeje nami sitaki kuuziwa mbuzi kwenye gunia?

Ukikutana naye kimwili ndiyo utakuwa umejiridhisha kuwa huyo ni mke bora kwako wa kuoa? Mbona unaangalia vitu vidogo sana, ninavyojua ndoa ni pana na mnahitaji kujiridhisha kwa vitu vingi ikiwamo kupendana kwa dhati.

Kama tafsiri ya kumpenda mtu kwako ipo kwenye kuingiliana kimwili sawa, ila kwangu sioni kama upo sahihi.

Haya ukimuingilia akikosa vitu unavyotaka ambavyo hapa hukuvitaja ina maana itakuwa basi umetimiza ulilolitaka, kama akikukubalia ukamkuta ana tabia mbaya utafanya maamuzi mengine? Unachowaza ili ukampose huyo binti ni kitu tofauti na vinavyoangaliwa na wengi, tafadhali jipange upya acha kumdhalilisha huyo dada, inaonyesha unachotaka kwake ni mapenzi na si kingine.

Kwanza miaka yote hiyo miwili umeshindwa kufanya uamuzi wa busara, nilifikiri anakataa kwenda kupima mjue afya zenu kabla hujakwenda kujitambulisha kwao, kwa sababu hilo lina faida kwenu nyote.

Kama unampenda kweli huyo binti na unataka awe mkeo, fuata taratibu kama kutuma washenga na uende kujitambulisha na umuoe, kushindwa kufanya hivyo eti kwa sababu hata kutoka na wewe kimapenzi ni dhaifu mno.

Advertisement