ANTI BETTIE: Tatizo nikimwambia nampenda, yeye anajua ninamtania

Habari Anti Betie, kuna dada nimezoeana naye sana kiasi kwamba kila ninachomueleza anaona ni utani.

Ukweli kutoka moyoni nimempenda na iwapo ataridhia nimuoe kabisa awe mke wangu.

Tatizo ni mazoea nikimgusia tu anajua ni utani, nitumie mbinu gani kumueleza hadi anielewe?

Pole sana kwa kuendekeza utani na sasa inakugharimu, ila hujachelewa na ni rahisi kufanikisha lengo lako.

Umesema unampenda na akiridhia mtafunga ndoa, hilo ni jambo jema. Kwanza jiridhishe kuwa hana mtu, inawezekana anatanguliza utani mbele unapogusia suala hilo kwa sababu ana mpenzi mwenye malengo naye.

Ukishajiridhisha, zungumza naye kwa kituo kama ataleta utani hakikisha kila siku usiku unamtumia ujumbe kwa kumueleza azma yako hiyo huku ukimsisitiza kuwa humtanii.

Ukiona mnashindwa kuelewana, mtumie rafiki yako au wake kufikisha ujumbe wako. Hakikisha suala la kumuoa ni la uhakika kwa sababu mlipofikia hawezi kukubali umchezee na inawezekana hata habari zako kidogo kuhusu wanawari anazijua.

Ukitumia njia hizo zote atakuwa anafikiria mara mbilimbili inawezekana kweli huyu bwana anataka kunioa, au ananitania?

Kitendo cha kufanya hivyo kina maanisha ameelewa, ila kutokana na mazoea mliyojenga ya kutanianataniana atakuwa anashindwa kukuambia. Kwa hiyo tumia nafasi hiyo kutuma mshenga kwao kwa ajili ya taratibu za ndoa.

Mwanamke kama huyu hawezi kuwa hawara yako kwa sababu mmetaniana sana. Kama una nia ya kuwa naye maishani mwako, wazo la kuwa mpenzi wako kabla ya ndoa liondoe.

Kama anajitambua anaweza kukubali baadaye baada ya kuona taratibu za ndoa zina mwelekeo.

Amenizalisha, kanitelekeza na mtoto

Shikamoo Anti!

Kuna kijana nilikuwa kwenye mahusiano naye hadi tumebahatika kupata mtoto. Cha kushangaza tangu nilipozaa alinihudumia zile siku saba za awali kuanzia hapo hatoi huduma kwa mwanaye wala kwangu.

Nifanyeje ili tushirikiane kumlea huyu mtoto?

Pole sana. Hapa nawakumbusha wasichana muwe makini kabla hamjaamua kuzaa. Kufanya hivyo kwa kukurupuka matokeo ndiyo kama hayo mtoto anateseka kwa sababu ya uamuzi wenu usiokuwa na utulivu. Pili inaonekana wazi hamkuwa makini na sijui kama mlijipa muda wa kupima afya zenu kama mpo salama au laa!

Sasa sikiliza hapo unapoishi nenda kituo cha polisi kilicho karibu nawe, ukiweza nenda kikubwa. Kaeleze tatizo lako, huko kuna madawati ya jinsia kwa ajili ya kutatua changamoto kama hizo.

Wao watakusaidia kumuita huyo mwanaume na kumueleza yanayompasa kuhusu suala lenu.

Mbali na polisi, pia unaweza kwenda ofisi za ustawi wa jamii ambao watamuita na kumpa masharti na maelekezo ya namna atakavyomtunza mtoto wake hata kama hana mpango wa kuendelea na uhusiano wenu wa kimapenzi.