ANTI BETTIE: Binti huyu amenitongoza, je anafaa kweli kuwa mke wangu?

Sunday May 26 2019

 

Nimekutana na binti katika sherehe, nikampenda kabla sijamwambia hisia zangu, kanianza yeye na kunitamkia wazi ananipenda.

Je, tutadumu kweli, au atakuwa kila anayempenda anamwambia?

Hussein

Kisarawe

Unadhani kukueleza hisia zake ndiyo ishara ya uhuni, hizo ni fikra zilizojengeka hasa kwa Waafrika, wapo wasichana, wavulana hawasemi lakini ndiyo wahuni wakiambiwa hawakatai. Inawezekana yupo makini ndiyo maana amekuambia hataki kuitesa nafsi yake. Nafasi bado unayo kuliangalia hilo kwa upande wa pili. Kukutamkia anakupenda hakumaanishi ni uhuni, uhuni ni tabia ya mtu tafakari, msikilize yupo makini kiasi gani kwa alilokuambia, kukubali kukataa ni jukumu lako, kulingana na utakavyoona, lakini sababu isiwe hisia hasi, jaribu kufikiri chanya inaweza kukusaidia kufanya maamuzi sahihi.

Naogopa kumpeleka kwetu kijijini sana

Advertisement

Nimeishi na mpenzi wangu kwa miaka mitatu, ana sifa za mke ninayemtaka. Tatizo naogopa kumpeleka nyumbani kwa sababu ni msomi na wazazi wangu hawajasoma na kwetu ni kijijini ndani ndani, nahofia hataweza mazingira ya huko. Je, niwalete wazazi wangu aje kuonana nao hapa mjini au nifanyeje?

Gilbert

DSM

Siamini kama hadi leo kuna mtu tena yupo Dar ana mawazo kama yako! Nani mwenye jukumu la kufanya kwao kuvutie naamini ni wewe kama umeshindwa hiyo ni aibu yako, mpeleke ukamtambulishe kwenu badala ya kuwaleta wazee hapa mjini hiyo siyo heshima wala utaratibu.

Muhimu na kipimo tosha kwa mpenzi wako ni kuweka pembeni usomi na kukubali wewe ni wake wa maisha na anatakiwa akubaliane na kila hali uliyonayo ikiwamo wazazi wasiosoma. Zingatia na umfunze mpenzi wako pia, mapenzi na usomi ni vitu visivyopanda boti moja, ni vitu viwili tofauti, anayependa haangalii amesoma au ngumbalo.

Mke mwema ana sifa zipi?

Anti habari za kazi.

Nimebakisha mwaka mmoja kwa mujibu wa malengo yangu kabla ya kutafuta mchumba na kuoa. Naomba sifa tatu za mwanamke atakayekuwa kiungo cha familia, zinisaidie wakati natafuta mke.

Zuyuni

Dodoma

Ngumu kutambua vigezo maalumu kwa sababu kila mmoja anapenda vitu tofauti na anavyopenda mwingine. Ushauri wangu zingatia mwanamke mwenye imani ya dini, atakuwa na hofu ya Mungu na itakuwa rahisi kwako kumkanya, kumuelekeza kwa sababu angalau atakuwa msikivu.

na uelewa kidogo wa baadhi ya mambo kwa maana ya kutokuwa mbishi, ajitambue, na awe na subira kwa maana ya kushinda asira zake.

Kwa uchache ni hayo kwa sababu ni binadamu hawezi kuwa na kila kitu, usikivu, uelewa, utulivu ni muhimu na akiwa na sifa hizo nyingine ni rahisi kujifunza hata kwa wengine.

Xxxxxxxxxxxxxxssssxxx

Natafuta dawa ya jasho kali

Anti naomba kuuliza, ninaweza kupata dawa ya kuzuia harufu ya jasho kali hospitalini?

Javie

DSM

Mh.. hadi umri huu sijawahi kusikia kama kuna dawa ya aina hiyo hospitalini, ushauri jitahidi kwanza kupambana na hali hiyo wewe mwenyewe kwa kusugua makwapa na ndimu kila unapooga. Nawa maji ya ukoko, tumia majivu kujisugulia pia inakata hiyo harufu, yapembue utoe vimikaa mikaa vyote hakikisha yamebaki laini ndiyo ujisugulie . Ila siyo mbaya ukienda kuonana na daktari kujiridhisha , inawezekana ana njia mbadala ya kitaalamu zaidi.

Muhimu ni kuhakikisha unakuwa msafi muda wote kwa kuoga mara kwa mara huku ukisugua ipasavyo maeneo ambayo unahisi yanatoa jasho kali linalokunyima raha.

Advertisement