Hata mparachichi ulianza kama figiri

Saturday May 11 2019GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nunduma

Aise hapa duniani wa mbili si wa moja. Mwenzio anazaliwa na kukuta mijengo, migari, miakaunti na miboksi ya hela, mwenzangu na mie unazaliwa kwenye nyumba isiyo na utaratibu hata wa mlo mmoja.

Kilichopo ni maziwa ya mama, ambayo pengine yanasalimika kwa sababu anatembea nayo. Hata mwenyewe yu tayari kufa kwa njaa ili akutunzie. Unawacheka wenzio wanapolia njaa maana wewe ukilia tu, mama anafungua mzigo.

Miaka miwili tu mbele kibao kitageuka. Utapangwa kwenye foleni ya kusubiri baba atoke kibaruani. Akirudi na kibaba cha sembe, mtapigana masingi mpaka makonzi kugombea uji wa chumvi. Lakini akirudi mikono mitupu ndo ishakula kwenu. Kwanza hamtamwona atakaporudi na hata atakavyosepa asubuhi.

Utasota kimkanda mkanda hadi kichwa kitakomaa. Utawaza “Nikiwa mkubwa ntakuwa dereva kama babaake Kulwa”. Lakini udereva gani hata kuandika jina lako hujui? Unabawabu na kuona hata kuku wa jirani wanakuja kutafuta msosi uwanjani kwenu.

Na wewe utadhani njia ya mkato ni kuingia kitaa. Kaka na dada zako walipoanza kuranda walirudi alfajiri tangu walipoondoka asubuhi. Ingawaje hukuona mabadiliko zaidi ya ngeu mbichi kwa braza kila akirudi na viguo vifupi kwa sista, lakini wangekuwa wanashinda na njaa wangedanga?

Na wewe unaanza za zako huku ukijipa moyo kwa kauli mbiu za wazamiaji: “wan dei yes!” Kwa kuwa akili ya mtoto inafanya kazi kwa haraka kama mchwa. utakuwa ushang’amua kuwa bro ni ‘mpiga ngeta’ na sista ni ‘changu’. Modo wako wa kwanza anakuwa braza kwa maana ya sista anayaweza mwenyewe.

Advertisement

Mchanganuo wako unakuambia kuwa mambo ya kabari yameshapitwa na teknolojia. Enzi zao mtu aliyepiga kabari aliogopwa na mji mzima. Lazima liwe mbavu nene. Lakini sasa ni hatari maana watu wana silaha za moto. Na unaweza kumkaba bingwa wa uzito wa juu bila kujua maana utakaona kadhaifu hivi lakini we… jaribu upoteze meno ya sebuleni.

Mpango-kazi wako wa kwanza ni kuranda kwenye vituo vya daladala, kuwavizia wageni wanaopiga simu kwa wenyeji wao kuulizia akodi bodaboda mpaka wapi. Ukishamweka kwenye kumi na nane unaikwapua hiyo simu na kula kona kwa spidi ya treni ya gesi. Yaani asipate hata wazo la kupiga kelele, achana na kukukimbiza.

Hatua inayofuata ni kuingia sokoni. Iwe simu ya kupangusa, kiswaswadu au hata simu ya gobore, kila kitu kinauzwa hapa mjini, hasara bei yake tu.

Kwa hiyo mchanganuo wote huo hautakuwa na maana iwapo utakamatwa. Ikitokea hivyo ni lazima utarudisha mali, lakini na fidia ya kufungwa au ngeu zinazofanana na za braza. Wahanga wengine huenda mbali zaidi kwa kukubali kuingia gharama ya spea tairi na mafuta ili mradi wakuchome mshikaki ungali hai.

Hivyo unajiandaa barabara kwa kuanza kukimbia ‘jogging’ kila Jumapili kwa lengo la kukusanya pumzi. Haina gharama kwani jogging itaishia pale Dar Live ambako mtapongezwa kwa soda na vitafunwa. Halafu unajituma kila siku kufanya mazoezi ya mbio fupi ili kujihakikishia spidi. Wanaokuona pale Uwanja wa Taifa wanaamini kuwa siku moja utatuletea medali ya dhahabu toka kwenye mashindano ya Kimataifa. Mh!

Sasa unaamini kuwa upo tayari kwa kazi. Siku hiyo unafanya savei kutoka kituo cha Buza Kanisani, unateremka kuelekea Machimbo kupitia Kwa Miundo Mbinu, Bondeni View mpaka Kwa Mhindi. Kote ni tulivu na rafiki kwa misheni hii ya kwanza.

Basi usiku unazuga kufanya manunuzi kwenye duka mojawapo jirani na stendi. Hammadi kabla hata hujauwasha sigara uliyonunua, anti mmoja anapaza sauti kwenye bonge la ‘aifoni’: “Sema kwa sauti bwana… Kwa Kidagaa ntalipia shingapi?... Haya basi na wewe unisubiri hapoha… Mtume Yaillahi… Simu yangu jamani!!!”

Ushakwapua. Lakini kumbe picha haliishii hapo… Pale kando kuna mmasai aliyewahi kupigwa kiswaswadu chake kilichokuwa kikimuunganisha na mama Yoyoo kule Monduli. Kipigo hicho kilisababisha amkose mwandani pale aliposhindwa kumtumia pesa za malezi ya mtoto wake. Mama alimfungasha mwanaye wakarudi Loliondo kwa wazazi wake.

Mungu bariki wakati Mmasai analiwazia janga lake, na hilo picha linachezwa mbele yake. Morani anapiga uyowe wa vita na anakuunganishia akiumbuka alivyofukuza na wezi wa ng’ombe. Kwa mdadi halisi anakupiga ovateki kisha anakupokea na mvua ya bakora mbele yake.

Watu wenye hasira nao wanampokea; unakula kichapo cha mbwa mwizi mpaka unapoteza. Kitendo mwana, majuto mjukuu. Unapokuja kushtuka watu washakutemesha meno yote kasoro gego, washaichakaza vibaya ‘risepsheni’ (sura) na kila unayemkaribia anasogea mbali na wewe. Na una bahati… wangekuua kama difenda ingechelewa kidogo tu.

Mbona siku hizi zipo njia za mkato za kutoboa? Kaombe kazi kwa mjasiriamali. Mwache akutume anavyotaka kwani kadiri unavyotumika ndivyo unavyojifunza. Hata kama atakulipa pesa kidogo wewe kula kidogo na uweke akiba. Mbona kule home mlikuwa mnapiga ndefu lakini ukaishi?

Advertisement