ANTI BETTIE: Hataki kunipeleka kwao licha ya kumzalia je, ananipenda?

Ninaishi na mwanaume nimezaa naye mtoto mmoja, kila nikimuambia aipeleke kwa wazazi wake hataki na amenunua kiwanja anajenga bila kunishirikisha na nilipomuuliza amenijibu siyo kazi yangu.

Je, huyu mwanaume ana nia njema na mimi kweli?

Kukupenda hakupimwi na kumzalia hilo liondoe akilini kwanza. Kwenye swali lako la msingi ni kuwa endelea kuzungumza naye akupelekae kwao kwa faida yake na yako kwa sababu kuna leo na kesho na mmezaa.

Mweleweshe ukiwa umetulia, ukitaka kulazimisha kwa sababu umezaa hutafanikiwa, inawezekana ana sababu za msingi kuwa anataka kufanya hivyo atakapokuoa, hivyo aseme mnaoana lini ili unaposubiri uwe na sababu. Hakikisha yote hayo mnajadili kama familia na siyo maadui kwa kulazimisha, hautaambulia kitu.

Kumbuka pia zipo familia kijana au binti yao akishazaa kabla ya ndoa anakuwa kama ameua, hivyo inawezekana anatafuta muda mzuri wa kuzungumza na wazazi au familia yake, hivyo kuwa na subira huku ukizungumza naye kwa lugha, lafudhi na sauti ya kike ili kulipa wepesi suala lako.

Amepigwa chini na mwanaume wa mtandaoni amerudi kwangu

Habari!

Kuna mwanamke nilikuwa nina uhusiano naye, akapata kazi nje ya nchi kwa mkataba wa miaka minne, akasema nimvumilie akirudi tutaoana. Nikavumilia aliporudi baada ya miaka minne ameniambia anaolewa na mwanaume aliyekutana naye mtandaoni. Niliumia sana, cha kushangaza amerudi tena anataka turudiane.

Pole kwa kufanywa kama mtoto. Mwanamke alikuwa na ujasiri wa kukuambia anaolewa na mwanaume wa mtandaoni hata baada ya kumsubiri kwa miaka minne, unadhani utapata nini tena kwake.

Kwa kuwa ndoa ni maisha, nakushauri kama unampenda ujipe muda wa kumsoma sana kujiridhisha kama amebadili tabia yake, tofauti na hapo tafuta ustaarabu mwingine.

Huyo mwanamke ana tamaa kabla hujafunga naye ndoa hakikisha amepona huo ugonjwa, inawezekana alipata mwanaume mwenye fedha au magari ya mitandaoni akajua amepata amekwenda huko hakukikuta alichokitaka amerudi kwako.

Angalia mkija kuanza maisha itakuwa tabia yake, anatafuta nafasi anakwenda kufanya anayoyataka kisha anarudi kwako.

Hatari nyingine ya mwanamke au mpenzi anayependa kujaribu jaribu mara mpenzi huyu mara yule ni kuleta maradhi kwenye familia.