Hewa, maji na usingizi, viini hai muhimu kwa wanadamu

Wanadamu hupuuza au kuweka chonjo mambo tunayoona ya kijinga.

HEWA ni la kwanza. Kuivuta, kuijulia, kuiheshimu.

Faida kuu ya kuogelea, kukimbia na michezo mingine ya kuhema ni kujenga mapafu. Unapostuliwa na jambo, au kufukuzwa , hewa hugeuka kitu muhimu sana.

Ndiyo sababu mtu anapoona kitu kibaya hushauriwa, “pumua kwa nguvu” au “vuta hewa taratibu...” Ukikasirishwa au unapogombana, ukitembea hatua chache kisha ukajipiga kofi jepesi kifuani, ukavuta pumzi mara kadhaa husaidia kukutuliza ukafikiria sawasawa. Waafrika wengi tunapatwa na kiharusi (au presha) kwa kutopumua sawasawa. Unapokuwa na shida ya unene, mafuta au uzito-ziada, mazoezi ya uvutaji pumzi yaweza kurekebisha moyo na mapafu yako.

Miongo kadhaa iliyopita nilifanya utafiti wa SABABU KUU zinazosababisha vifo vyetu. Nilikuwa n’kiishi Brazil. Vita vilienea: bastola na mauaji ya kutisha Marekani ya Kusini, Mashariki ya Kati na Rwanda. Nikidhani kiini cha mauaji ulimwenguni ni bunduki na vita.

Nikazungumza na maaskari na madaktari. Nikatembelea maktaba kadhaa za kitabibu na wapasuaji maiti (baada ya vifo mahospitalini)...sababu mosi, kitakwimu, ilikuwa mapafu kushindwa kazi yake. Asilimia kuu ilitokana na sigara na hewa chafu.

Nikagundua suluhisho ni kusimamia vyema vifua na mapafu.

Na takribani miaka thelathini baadaye, mazoezi ya Yoga yanazagaa mithili ya siafu Uzunguni, hasa wanawake. Lakini Yoga si ya wanawake tu.

Yoga ni mazoezi yanayozingatia sana uvutaji pumzi. Iliasisiwa Uhindini.

Mwaka 1983 nilikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Hatha Yoga, Dar es Salaam. Sina hakika kama wenzangu, Juma na mkewe Sada bado wanayaendeleza.

Jambo la pili ni MAJI. Wapo wanaodai hawapendi maji. Hupendelea soda, chai, Cocacola, Fanta, kahawa, bia nk. Hukatisha kiu kwa sukari au kilevi. Wapo wanaodhani maji ni kinywaji cha watoto na wagonjwa. Ukweli twatakiwa kunywa lita mbili (glasi nane) kwa siku, kusaidia kazi ya figo, utumbo, ngozi, moyo, mapafu, ubongo nk. Asilimia 70 ya miili yetu ni MAJI.

La tatu? USINGIZI.

Hapa Uzunguni sasa hivi kuna tatizo la kukosa usingizi.

Hii ni kutokana na haraka haraka za kimaisha.

Fadhaa na mtafaruku huu unatufanya tulale saa sita tu kwa siku.

Kuna wanaokosa usingizi kabisa.

Upweke nchi zilizoendelea ni tatizo zito linalosababishwa na mawasiliano magumu, kuvunjika familia na uchumi. Karibuni, usingizi umeathiriwa na simu za mkononi na mitandao jamii. Watoto, kwa watu wazima hawaziachi hizi mashine. Kutwa kucha. Nimeshakutana na watu wengi sana ambao huwasiliana katika mitandao jamii - Instagram, WhatsApp na Facebook, kwa hamasa, ila mkikutana maso kwa maso, hawana la kusema.

Hugeuka baridi ya barafu.

Tunatakiwa kulala saa 7-8 kwa siku. Usingizi ni dawa.

Ukilala saa nane kila siku unarutubisha viungo vingi. Wataalamu wanaasa usipolala unachakaza viini vya uhai wako. Hudhoofisha ubongo na DNA - watawala wa uhai. Usipolala sawasawa utajisikia mchovu, msahaulifu na kuugua kirahisi. Kulala si uvivu ni tiba. Kulala hakuepukiki.

Ni suala la lazima kama kula na kuzaa.