Ishu siyo ile video, kuhisiwa tu ni dhambi

Saturday May 11 2019

 

By Dk Levy

Navuta pumzi kibwegebwege utadhani Mungu ni babu mzaa mama. Nadeka kiboya na mavazi meusi kama popo wa mapango ya Amboni. Najidai. Natembea kwa kurukaruka kama kangaroo. Maji mengi kuliko mchanga. Kila hatua dimbwi la maji. Kifupi Dar mvua ikinyesha huitwa Majimaji City.

Natazama kulia naona totoz imeshikilia dera. Kalivuta juu kabisa karibia na hifadhi ya taifa ya nafsi na roho. Najiuliza anaogopa kulowesha dera au ni kampeni shawishi apate mpiga kura wa kuondoa baridi mwilini? Maji hayafiki kwenye kisigino, lakini dera limebaki robo tu kwa juu, huku chini limekunjwa lote.

Nikajisemea moyoni, hii surua sijui dengu ya kike itaharibu funga yangu. Naangalia kushoto balaa lingine. Dada ambaye kwa uzoefu wangu juu ya viumbe hawa anaonesha ni ‘singo mamaz’. Kifua, ngozi, utembeaji, kujiamini na ndita kadhaa kwenye paji la uso. Nagundua analea mtoto peke yake.

Ngoja nikuibie siri. ‘singo mamaz’ hawajirembi sana kama ‘singo geloz’. Lakini wana mvuto wa pekee kwa sababu miili yao haifichwi sana, yaani anaweza vaa dera tu bila ‘bra’ mpaka mtaa wa tatu kuazima dekio. Wana ngozi laini kwa sababu ya uzazi na kushinda ndani muda mwingi. Ndita zina ubia na mapaji yao ya uso kwa kisirani cha kulea watoto peke yao.

Hutembea kwa kujiamini kwa sababu ya kuitwa mama fulani. Kuanzia miaka 25 kuendelea, totoz kuitwa mama fulani, ‘automatikale’ hujivunia. Umri huo akiitwa kwa jina halisi kama yuko Form 3 B One, Jitegemee Secondary School. Ni maumivu. Ni umri wa kuwa na mwenza au mtoto zaidi ya hapo ni mateso kwa wanawake wengi.

Sasa huyu wa kushoto alijiamini kama gari la taka. Moyo wangu siyo toi nione totoz na kanga moja kwenye mvua akimkimbiza mtoto nijifanye sina habari. Nipite? Nikasimama ili nijue kosa la yule mtoto mpaka akimbizwe namna ile bila kujali mvua. Nikagundua anamkataza asichezee maji ya mvua.

Alikuwa sahihi. Ila angekuwa mke wa mtu angetuma mtu, au asingevaa kanga moja na kukimbizana na mtoto vile mtaani kwenye mvua na watu wakiona. Wajanja tukagundua kuwa yeye nd’o mwenye mtoto ila hana mume. ‘Singo mamaz’ kawaida hujiamini kimaongezi, kimavazi na utembeaji. Amuogope nani?

Sifa nyingine ya ‘singo mamaz’, mapenzi yote kwa madanga kabla hajazaa yanahamia kwa mtoto. Mimi nilisimama nijikinge mvua na nimalizie ile sinema ya bure. Alipomkamata mwanaye hata hakumchapa akarudi akicheka sambamba na mtoto wake. Ilivutia sana. Na hapo ndipo nikagundua yule mtoto ana mama mrembo sana.

Picha yote niliitazama nikiwa nimesimama kando ya kiduka cha Mangi nikizuga mvua iishe. Alikuwa mrembo hasa nikatamani niwe baba wa mwanaye ghafla. Ni kama filamu ya Hollywood, lakini lilikuwa tukio halisi mitaa ya Sinza. Nilijikuta natabasamu. Sikusita kumuita... naye bila kujali akaja na mtoto wake nilipo.

Nikacheka na mtoto huku namuuliza jina lake. Akagoma kunitajia mpaka mama mtu alipoingilia kati. Hata sielewi nguvu na ujasiri ule ulikotoka. Nikalala ubavu na kutoa noti mbili za elfu kumi na kuiacha kipweke noti ya elfu tano tu kwenye ‘waleti’. Nikamkabidhi yule dada na kusindikizia na neno “mnunulie anachotaka mtoto.”

Mengine haya ni ya kusamehe tu. ‘Hakunaga’ mwanamume bahili na jasiri kwa mwanamke, bali kuna mwanaume jeuri na katili kwa mwanamke. Urembo alionao niliona ile elfu 20 haitoshi. Ningekuwa na zaidi ningetoa bila hofu. Sikuwa na ujasiri wa kumpa kidogo nibaki na kingi. Labda alikufa, kama jamaa aliyemzalisha kamuacha huyo ni jeuri na katili.

Ninachokumbuka nilichukua mawasiliano yake ili baadaye nimpigie kujua hali ya dogo maana alivyoloa ni rahisi kupata homa. Mwezi wa toba huu lazima tuwe na moyo wa kujali. Kuna totoz zinavutia mpaka unatamani yeye na mtoto wake wote wawe wako milele amina. Ndiyo huyu niliyekutana naye wiki hii.

Ukiona mtu anapinga hili ujue ni wivu tu au hana hela za kuhonga. Nd’o yaleyale ya video inayodaiwa ni ya baba askofu. Ukiitazama vyema ile video na picha za anayedaiwa ndiye mrembo husika utaelewa kuwa wanaume wanaolaumu sana wanatamani wangekuwa watuhumiwa.

Huhitaji kipimo kujua ni wa daraja gani. Kama hujaona video basi soma haya maandishi kisha weka akilini kuwa ni mrembo wa dunia ya kwanza.

Na hata wanawake wanaopinga pia wanatamani wangekuwa huyo mwanamke. Maana ule ufundi na swaga za ‘baba’ ni vigumu kukutana nazo kwenye dunia hii ya janga la nguvu za kiume.

Warembo wa namna ile huwezi kuwamiliki kwa maisha ya mshahara. Ni wale ambao unatakiwa umpe pesa, mpe pesa, mpe pesa, wewe mpe pesa tu. Zaidi ya hapo utaishia kumuita shem au shemela kama zuzu. Ile video niliifuta ‘imidietili’ baada ya kuiona. Kama imebaki katika simu yangu basi ni muujiza au shetani kanipitia.

Sipo katika kundi la ‘maibilisi’ wanaolazimisha yule ni askofu, ila nipo kwenye kundi ‘teule la Bwana’ linaloamini yule mrembo anastahili kuitwa mrembo.

Tuwekane sawa hapa, kinadada wengi miaka ya karibuni wanakimbilia kwa ‘watumishi’, maaskofu na wachungaji kuombewa. Kinachowapeleka wengi wao ni kupata mume, ndoa au mimba. Haya nd’o matatizo makubwa ya dada zetu. Na matatizo haya umekuwa mtaji mkubwa kwa makanisa mengi ya kiroho.

Nataka kumaanisha nini? Kwamba kisiwe kitu cha ajabu watumishi kukutwa na janga kama hili. Na huyu amekuwa mhanga wa ‘skendo’ hizi kwa sababu siyo mara ya kwanza. Huwezi kuvuna njegere kwenye shamba ulilopanda kunde. Waumini wao wengi ni kinamama.

Jitu linaendekeza mipombe, bange na kila aina ya ulevi kiasi kwamba linashindwa kutimiza wajibu wake kwa mkewe.

Mwanamke anajua karogwa nd’o maana hapati mimba anaamua kwenda kwa watumishi wamuombee. Kumbe hana tatizo lolote bali mume ndiye anayehitaji maombezi.

Wasichana wengi wanaishi maisha ya kimjinimjini sana. Asubuhi yuko baa anapata supu, mchana yuko saluni kwenye umbea. Usiku yuko baa kwenye mitungi. Muda wote anakoleza marangi usoni akiamini ndiyo mvuto wa kupata mume. Anageuzwa kifaa cha starehe tu.

Kuna miaka kati ya 18 mpaka 25. Hapo msichana akipoteza mwelekeo wake basi imetoka hiyo. Kuanzia hapo wengi huishia katika ‘usingo mamaz’ kwa kuzaa na yeyote. Mpaka unafikisha miaka 25 unatakiwa kuwa na bwana mwenye miaka 35 na kuendelea.

Usianze kusaka bwana sahihi baada ya kufikisha miaka 25, tafuta kabla. Kuanzia hapo kwenda juu utaishia kusumbua watumishi na waganga wa jadi. Wakati muda wa kufanya hayo uliishia kurukaruka na kudanga kama ngisi. Kosa la wengi ni katika kuzingatia muda.

Okay kwenye ile video tusimjadili yule mwanaume. Tuanze kumjadili yule ‘kicheche’ tunamuita ‘kicheche’ kwa sababu ni ‘kicheche’ pekee anayeweza kurekodiwa kibwege namna ile kwenye lile tendo. Mwenye akili timamu hawezi kukubali.

Kwa uzuri ule hawezi kukosa kuwa na mume, mchumba au bwana’ake wa uhakika. Kwa lile umbile, rangi na sura ni dhambi kukosa bwana sahihi wake wa pekee. Mana’ake nd’o wale wasichana wanapoteza dira na mwelekeo kwenye miaka 18 mpaka 25. Wako wengi.

Muda wa kutulia na bwana mmoja na sahihi wanadanga ili wavae nguo mpya kila wiki, walewe na kubadili nywele zao.

Muda wa kusoma wako ‘bize’ mitandaoni kufuatilia maisha ya mastaa ambao asilimia tisini wamefeli maisha ndipo wakajiingiza kwenye uigizaji na muziki.

Haya matukio yanazalisha wadangaji na ‘usingo mamaz’ pia kwa kiasi fulani huletwa na wadangaji. Wadangaji huvuruga ndoa, penzi na uchumba. Kifupi ni kwamba kwa kiasi kikubwa chanzo cha ‘singo mamaz’ pia ni ‘singo geloz’ ambao hawataki uhusiano sahihi zaidi ya kudanga.

Uzinzi siyo kwamba unaharibu ndoa, familia na maisha tu, lakini huharibu roho na roho kwa njia inayosababisha kifo cha kimwili na kiroho.

Mungu anatamani kwamba tuwe bila hatia na tutumie miili yetu kama zana za matumizi na utukufu wake. Mwili siyo kwa uzinzi bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili.

Ingawa uzinzi ni dhambi, makahaba hawajazidi upeo wa Mungu wa msamaha. Biblia inaonyesha matumizi ya kahaba aitwaye Rahabu ili kuendelea na kutimiza mpango wake. Kwa sababu ya kutii kwake, yeye na familia yake walitunukiwa na kupewa baraka.

Yote kwa yote ile video tusimame kwenye ukweli, kwamba urembo wa yule ‘dem’ lazima shetani achukue pointi zote tatu ugenini.

Advertisement