USHAURI WA DAKTARI: Kuugua kwa muda mrefu huathiri nguvu za kiume

Kuugua magonjwa tofauti kwa muda mrefu ni moja ya sababu zinazoweza kuchangia ukosefu wa nguvu za kiume.

Ugonjwa wa kisukari, maradhi ya mishipa ya damu na shinikizo la damu ni mojawapo ya matatizo ambayo mara kwa mara yanaweza kusababisha tatizo hili.

Uwepo wa ugonjwa wa kisukari kisichodhibitiwa kwa muda mrefu huweza kusababisha mishipa inayopeleka damu katika uume kuharibika.

Sukari iliyo juu huiharibu mishipa hii ya damu na kuifanya iwe migumu, kukakamaa na iliyosinyaa.

Ili damu iweze kupita kiurahisi na kwa wingi inahitaji mishipa ya damu kutanuka na kuwa laini.

Kuharibika huku kwa mishipa ya damu husababisha damu kutotitirika kwa wingi katika misuli sponji ya uume.

Utiririkaji wa damu kwa wingi katika misuli ndiyo chanzo cha eneo hilo la uzazi kusimama.

Sukari iliyo juu mwilini huweza pia kuharibu mishipa ya fahamu sehemu mbalimbali mwilini ikiwamo mshipa muhimu unaopeleka taarifa na kurudisha eneo hilo baada ya ubongo kutoa tafsiri za mihemko ya kimwili.

Kuharibika kwa mishipa ya fahamu kwa eneo hili ndio mojawapo ya sababu kubwa ya kushindwa kusimama kwa uume kwani mawasiliano yanakosekana kati ya ubongo na uti wa mgongo (mfumo wa fahamu) hivyo ufanisi wa kuwezesha kutokea kwa mawasiliano ya eneo hilo kupotea.

Shinikizo la damu lisilodhibitiwa kwa muda mrefu ni mojawapo ya maradhi yanayochangia pia kuwapo kwa tatizo hili.

Shinikizo la damu likiwa ni kali mara kwa mara huweza kuleta uharibifu katika mishipa ya damu ambayo ni midogo midogo iliyotanda kwa wingi katika uume.

Magonjwa ya moyo, magonjwa ya mishipa ya damu na uwepo wa mafuta mabaya mwilini (cholesterol) nayo pia huchangia kuharibu mishipa ya damu ya eneo hili.

Mambo mengine ni utumiaji wa tumbaku, uvutaji sigara, ulevi uliopindukia na utumiaji wa dawa za kulevya navyo pia huweza kuharibu mishipa ya damu katika uume.

Magonjwa ya tezi ya koo inayotoa homoni za ukuaji mwili na kutengeneza kidogo kwa homoni muhimu ya kiume ambayo ni Testosterone pia huathiri nguvu za kiume.

Maumbile yasiyo timilifu sehemu za kiume kama vile kokwa kuwa ndogo au kunyauka na uume mdogo sana.

Maradhi mengine ni pamoja na ugonjwa wa kutetemeka pasipo hiari (Parkinsonism), magonjwa ya mfumo wa kinga mwili.

Unene uliopitiliza sana na mwili kuwa na uzito uliokithiri ni mojawapo pia ya chanzo cha upungufu wa nguvu za kiume.

Mambo mengine ya kiafya ni pamoja na magonjwa ya akili ya muda mrefu, magonjwa sugu ya muda mrefu ikiwamo VVU na matibabu ya muda mrefu ya saratani ya tezi dume.

Nihitimishe tu kwa kuwatoa hofu kwamba si kila anayeumwa magonjwa haya anaweza kupata tatizo hili la ukosefu wa nguvu za kiume.