UJASIRI: Maanda Ngoitiko anavyopigania maisha ya wanawake wa jamii ya kifugaji

Kwa mujibu wa takwimu za Unicef kati ya mwaka 2010 na 2017, Tanzania imekuwa nchi ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda.

Kiwango cha watoto walio na umri chini ya miaka 18 nchini Sudan Kusini ni asilimia 52, nchini Uganda ni asilimia 40 huku Tanzania ikiwa ni asilimia 31, wakati Kenya ni asilimia 23.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa nguvu kubwa ya kutokomeza tatizo hili la ndoa za utotoni ilihamia Afrika, ambapo jitihada zaidi zilihitajika ili kupunguza tatizo hilo.

Umoja wa Mataifa huchukulia ndoa za watu wa chini ya miaka 18 kuwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Hata hivyo, shirika hilo limekadiria kuwa ndoa za utotoni zipatazo milioni 25 zimeweza kuzuiwa muongo iliyopita.

Kwa sasa ni msichana mmoja kati ya watano anaolewa akiwa chini ya miaka 18, tofauti na miongo iliyopita wakati kiwango kilipokuwa msichana mmoja kati ya wanne.

Jitihada hizi za kupunguza tatizo hili zimekuwa likifanywa kwa kiasi kikubwa na mashirika ya kutetea haki za watoto na wanawake, ambazo kwa kiasi kikubwa zimeuwa zikihusisha elimu ya kujitambua.

Kuna athari kwa msichana kupata mimba akiwa katika umri mdogo, kama kushindwa kuhimili mikiki ya ulezi wa mtoto, kukatizwa ndoto zake katika maisha, kufikwa na mauti wakati wa kujifungua kutokana na njia ya uzazi kuwa ndogo, athari ambazo zinaweza kuepukia.

Hata hivyo kuna usemi usemao siri ya mtungi aijuaye kata, ikimaanisha huwezi kujua kitu kwa undani kama hujawahi kuishi maisha yake.

Hii ndivyo ilivyo kwa mkurugenzi mtendaji wa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), Maanda Ngoitiko, ambaye ni mmoja ya wasichana walionusurika kuozeshwa kwa nguvu na wazazi wake, akiwa na miaka 12.

PWC imekuwa ikijishughulisha na kuwawezesha kiuchumi, kielimu na kujua haki wanawake wa jamii hiyo ya kifugaji kiuchumi.

Maanda ambaye kwa sasa ana miaka 41 anasema wakati akikwepa kiunzi hicho kwa kukimbia nyumbani kwao, rafiki yake alikamatwa na kuozeshwa akiwa na miaka 12.

Anasema pamoja na kupitia changamoto mbalimbali wakati wa kujinusuru, anashukuru aliweza kumaliza elimu yake ya msingi na baadaye sekondari ambapo alipata ufadhili wa kwenda kusoma nje ya nchi.

Anafafanua alisoma kwa bidii na kila hatua ya masomo yangu ilikuwa inalenga kutoa funzo kwa wasichana na jamii ya Kimasai kwa ujumla kuwa kusoma kunawezekana.

“Enzi zetu mtoto wa kike alikuwa hana thamani na alifikiriwa kuwa ni mtu wa kuolewa na kutunza familia,” anasema..

“Bila kujua kwamba mtoto wa kike ukimsomesha anakuwa na msaada mkubwa wakati mwingine kuliko hata mvulana, kwani yeye anapopata mafanikio ni rahisi kukumbuka familia.”

Anasema kama ilivyo ada baada ya kumaliza masomo ilikuwa lazima arudi nyumbani kwa ajili ya kuelimisha jamii iondokane na mila potofu.

Anasema alianza taratibu kwa kuzungumza na mtu mmoja mmoja, ingawa alionekana kama anadharau mila zao.

“Haikuwa kazi rahisi kwa sababu bora ugonjwa ni rahisi kuutibia hata kama ni sugu kuliko imani,” anasema.

“Asikuambie mtu, imani za makabila ni zaidi ya dini. Nilionekana kama muasi, lakini niliungwa mkono kwa siri na kina mama ambao walichoshwa na vilio vya binti zao.

“Kingine tayari baadhi ya familia 100 kwa moja zilikuwa zimeamka na kuondokana na dhana kuwa mtoto wa kike hapaswi kusoma bali kuolewe tu na kulazimika kuhamisha mabinti zao ili wakasome maeneo mengine.”

Lakini wakati akitoe elimu alipata wazo la kuanzisha baraza.

“Niliamini ili mwanamke hususan wa Kimasai aheshimike ni lazima ajue masuala ya kiuchumi, kielimu, umuhimu wa kumiliki ardhi na uongozi,” anasema.

Anasema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali alifanikiwa kuanzisha baraza hilo ambalo limekuwa likitoa ufadhili wa masomo kwa wasichana wa jamii hiyo walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na ama kuozwa kwa nguvu au kupata mimba.

“Kwa miaka 20 tangu baraza hili lianze tumekuwa tukisomesha wasichana wa aina hiyo, kuanzia sekondari hadi ngazi ya vyuo na sasa kuna wasichana 56 ambao wapo vyuoni wakisomea kozi mbalimbali,” anasema Maanda.

Anasema anapata changamoto baadhi ya wasichana wanakosa mikopo ya elimu ya juu, hivyo kulazimika kuitisha harambee mara kadhaa ili kuwasaidia.

“Mwaka jana Oktoba nilifanya katika kijiji cha Ketumbeine, Wilaya ya Longido, iliyoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa baraza hilo,” anasema.

“Katika harambee hiyo iliyoongozwa na mbunge wa zamani wa Longido, Michael Laizer nilikusanya Sh94.7 milioni kati ya fedha hizo, Sh61.5 milioni ni fedha taslim huku Sh33.8 milioni zikiwa ni ahadi.”

Ushuhuda

Mmoja wa walionufaika na mpango huo ni Resiato Lembaka.

“Elimu niliyoipata imenipa mwanga na naamini itabadili tabia za jamii yetu ya kuona mtoto wa kike hastahili kusomeshwa,” anasema Resiato.

Kuhusu uwezeshaji wanawake kiuchumi, PWC imeanzisha vikundi 260 vyenye wanachama 3,000 katika wilaya za Longido na Ngorongoro.

Maanda anasema mtaji unaozunguka ndani ya vikundi hivyo ni Sh800 milioni na kwa kijiji cha Kutumbein wamekopeshana hadi Sh160 milioni.

Kutokana na kutambua umuhimu wa vikundi hivyo, mkurugenzi huyo anasema hata tabia za wanaume sasa zimebadilika na wanaruhusu wake zao kwenda kwenye vikao.

“Mafanikio haya yanatokana na kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa vijiji pamoja na familia na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa wanawake kuingia kwenye shughuli za ujasiriamali, na kuna wanachama zaidi ya 4,000 kwa sasa wanaotengeneza bidhaa mbalimbali na kuziuza, jambo linalowasaidia kuongeza vipato katika familia zao,” anasema Maanda.

wameweza kumiliki ardhi na kujenga nyumba zao jambo ambalo zamani ilikuwa ni nadra kumuona mwanamke wa kifugaji akiwa na nyumba.

Anafafanua tangu kuanzishwa kwa baraza hilo hadi sasa wanawake 160 wana maeneo yao na wengine wameshajenga miji yao.

Anasema pia wasichana wamekuwa na uwezo wa kujitetea, wanaweza kusimama mbele ya wanaume na kutoa misimamo yao ikiwemo suala zima la kukataa kuolewa pale wanapolazimishwa.

Mikakati

Maanda anasema mikakati ya PWC ni kuendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na mengine yatakayowawezesha kukabiliana na kutafuta suluhu ya matatizo yanayoizunguka jamii ya kifugaji kila siku.

Pia wana mpango wa kujenga chuo cha kufundisha masuala ya kazi za mikono jambo ambalo litasaidia wasichana wengi kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa pale wanapomaliza shule