KUTOKA LONDON: Malalamishi kuhusu mapenzi na ngono yanazidi kuchemka duniani - Sehemu ya 1

Mara nyingi nimeigusa mada hii hapa. Ila baada ya kuihakiki kupitia kipindi changu maalum “Kwa Simu Toka London”, yamezuka maoni ambayo yanastahili kujadiliwa kwa wale wasiomo You Tube au mitandaoni. Kuna tatizo kubwa la kimahusiano.

Kilio cha mapenzi na ngono kimeshika moto kwa wananchi Afrika Mashariki.

Imenidhihirishia kuwa jumuiya zetu zimeshaathiriwa vibaya sana na Uzungu.

Uzungu una ncha mbili. nzuri na mbaya. Tunazungumzia, mabaya.

Zamani Mwalimu Nyerere na viongozi wa Tanu walisititiza sana Uafrika. Si kwamba uongozi wa sasa wa CCM hauendelezi dhana hizo, ila enzi za Tanu hatukuwa na mitandao jamii na urahisi wa wananchi kuona mengi yanayoendelea duniani.

Kilio cha mapenzi kimegawanyika sehemu mbili.

Huku Majuu, kilianza karne kadhaa zilizopita. Wenzetu wamekuwa na matatizo ya ngono toka dini za Mashariki ya Kati zilipoingia na kusisitiza kuwa ngono ni uchafu. Changanya hilo na hali ya hewa, baridi. Ubaridi huu ulichanganyika na mila za kujinyima; lililoruhusiwa ni ndoa tu.

Hivyo waliokuwa nje, hususan wanawake, walijinyima. Lakini kijamii kulikuwa na ubaridi uliozua kila aina ya mitafaruku. Mathalan tendo lenyewe la ndoa lilifanywa vinginevyo. Waandishi maarufu wa fasihi kama DH Lawrence walilia namna jamii ilivyozibwa kimapenzi.

Ikiwa unajifunza Kiingereza (na mpenzi wa vitabu) hebu zitafute riwaya zake DH Lawrence.

Mfano “Lady Chatterleys Lover” kilipigwa marufuku (Uingereza na Marekani) mwaka 1929 hadi kiliporuhusiwa 1960. Ni kisa cha bibiye aliyenyimwa mapenzi mazuri na mumewe akaenda ugoni na mfanyakazi wao wa nje.

Kisaikilojia, Ulaya palizuka daktari Sigmund Freud, ambaye husomwa na kupelelezwa miongo mingi na wasomi.

Haya yalifikia kilele miaka ya 60 wimbi la Ukombozi wa wanawake lilipotimba.

Wanawake sasa walitupilia ndoa nje, talaka zikastawishwa.

Wakati sisi wengine tunaingia Ulaya miaka ya 70 na 80 wimbi hili lilituathiri.

Waafrika tulionekana kama wachawi. Tulioa, tuliolewa; kipya kinyemi.

Wanaume weupe walisemwa hawayawezi mapenzi.

Leo, si tu hayo. Simu za mikononi zimeshadidi. Wanaume kwa wanawake wanatafutana hawaonani. Sinema za ngono, viganjani. Mitandao jamii inasambaza sinema na wananchi wanajifurahisha wenyewe kwa kutazama picha na filamu.

Matokeo maradhi ya kisaikolojia.

Si rahisi kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Ndoa zinavunjika. Ufirauni umekithiri. Wananchi wanasambaratika na mashine za ngono zinauzwa. Baada ya miongo kadhaa itakuwa kawaida kununua mpenzi sanamu kujiridhisha.

Haya ni ya Uzunguni. Afrika tulikuwa vingine.

Joto, desturi, vyakula, mahusiano; hayakuturarua rarua, asilani, kimapenzi.

Afrika Mashariki hapa kuwa mahali pa kukosa mpenzi wa kuoa au kwa kipindi.

Yalitokana na jadi zetu: ngoma, chakacha, kukatika viuno, vyakula asilia, ujirani mwema na mahusiano ya moto, utani na masihara masihara, vilichangia.

Ila yameanza kubadilika, tena kwa kasi.

Wanawake vijana wanalia ndoa tupu. Karibuni video zimezagaa mitandaoni. Wanawake wanalalamika wanaume wanakula vitu vinavyowafanya wasichoke kimapenzi. Nyingine Zambia ilidai Konyagi ya Tanzania ina hayo hayo. Kizungu neno la kitaalamu ni “priapism” litazame katika kamusi.

Kuna video mseto wa utani na uzushi. Kuwa wanawake Tanzania wamewaomba madaktari wawapime wanaume kuhakikisha watawaridhisha wakishafunga ndoa. Hii si kasheshe? Tufanye nini?

Tuendelee Jumapili ijayo...