TUONGEE WAZAZI: Mambo 6 ya kuzingatia kabla ya kuweka picha ya mwanao mtandaoni

Kadri siku zinavyokwenda wazazi hupenda kuweka picha za watoto wao mitandaoni huku wakiwapongeza na kujivunia walivyo warembo, wenye akili, wepesi wa kujifunza na wanavyowaletea furaha. Mshawasha na wepesi wa kutaka ‘kushea’ picha za mtoto wako hasa kwa marafiki (na hata wasio marafiki) kwenye mitandao ya kijamii na blogu hauzuiliki kirahisi. Bahati mbaya, athari za maamuzi hayo pia haziepukiki.

Ingawa imekuwa kawaida kuweka picha za watoto mitandaoni, zipo athari zinazoweza kumkuta mtoto tusipokuwa waangalifu. Picha tunazoweka mitandaoni zinaweza kuibiwa na kutumiwa na watu baki, lakini pia zinazopigwa na simu au vifaa vyenye teknolojia ya kuonyesha mahali ulipo (GPS), vinavyoonyesha mahala picha ilipigwa.

Zifuatazo ni hatua sita ambazo mzazi anapaswa kuchukua ili kulinda watoto/mtoto wake.

Matumizi ya faragha. Takribani mitandao yote ya kijamii huwapa watumiaji fursa ya kuamua nani wa kuangalia picha zao na taarifa binafsi (mfano mwaka wa kuzaliwa, nk.). Facebook inawapa watumiaji ruhusa kuamua kama wanataka ‘marafiki’ tu kuona picha zao, au kila mtu. Ni vyema kudhibiti idadi ya watu wanaoweza kuona picha za mwanao kuepusha watu baki kuzitumia kwa namna ambayo mzazi hukukusudia.

Fahamu marafiki zako. Kama una mamia ya marafiki kwenye mitandao ya kijamii, upo uwezekano huwajui wote vizuri. Jipange upitie orodha ya marafiki zako kuhakikisha kama mnaendana kimaadili na hata katika mambo mnayopenda. Pengine ulikubali ombi la rafiki toka enzi za shule ya sekondari na sasa huna taarifa zake kama ni mwema au laa. Unaweza kumuondoa katika orodha ya marafiki mtandaoni.

Zima teknolojia ya kuonyesha mahali ulipo (GPS) kabla ya kupiga picha kwa simu kama una mpango wa kuzipakia mtandaoni. Baadhi ya kamera za kisasa zina teknolojia hii, chunguza iwapo imezimwa kabla ya kupiga picha unazotaka kuziweka mtandaoni. Ikiwezekana zima teknolojia hii hasa ukiwa nyumbani, shule kwa mtoto, kwa ndugu au kwingineko kwani huwezi kujua ni wakati gani hasa utajikuta unapiga picha za ‘tukio’ linalokulazimu ‘kushea’ mtandaoni.

Chukua tahadhari ili kuepusha kutoa taarifa zako binafsi pasi kutarajia. Mfano picha uliyopiga mbele ya nyumba yako inaweza kuonyesha makazi yako wapi, au fulana yenye nembo ya shule anakosoma mwanao inatoa taarifa za mtoto wako. Inashauriwa kuchukua tahadhari hizi iwapo lengo la picha ni kutumika katika mitandao ya kijamii au blogu.

Picha za utupu ama mtoto akioga. Swali ni iwapo mtoto wako akizikuta miaka 10 au 20 baadaye atajisikieje. Kama inavyofahamika picha hizo zinaweza pia kuonwa na marafiki zake wa kiume/kike?

Atafurahia mwalimu wake ama bosi wake akimuona hivyo? Kamwe usipakie picha za mwanao akiwa anajisaidia, anaoga na akiwa mtupu bila nguo.

Picha ya mwanao isipakiwe mtandaoni bila idhini yako. Iwapo ndugu au rafiki amepakia picha ya mtoto wako mtandaoni na hujapenda muombe aiondoe. Hii ni kwa kuwa huna hakika na umakini wao na hujui aina za marafiki wake mtandaoni wanaoweza kuitumia kwa nia ovu. Hapa pia tunashauri ukitaka kuweka picha ya mtoto mtandaoni omba ridhaa kwanza.