TUONGEE KIUME: Mbinu tatu za kumkomesha mwanamke anayewaalika marafiki ukimtoa ‘out’

Kwa kuonyesha mahaba unaamua kumtoa ‘out’ mpenzi au mchumba wako kumpeleka sehemu mkapate vinywaji na msosi wa tofauti kidogo na ule mliozoea, ili pia mpate fursa ya kupiga soga za tofauti na zile mlizozoea na mkuze uhusiano wenu muwe maswahiba, ili hata mtakapofikia kuwa wanandoa muungano wenu uwe wa amani.

Lakini kwa sababu duniani kuna wanawake wengi wenye akili za kushikiwa kama ilivyo kwa wanaume wasiokuwa na akili kabisa, unashangaa mwanamke anakuja na kikosi. Anakuja na shoga zake watatu, wawili aliosoma nao chuo na mmoja mfanyakazi mwenzake jumlisha na binamu yake wa Tegeta.

Unabaki unajiuliza kweli huyu ndiye mwanamke ninayetaka kumuweka ndani, mwanamke mwenye akili hizi? Na isitoshe hao waandamanaji aliokuja nao si watu wa mchezo mchezo wanajua kuagiza kupita maelezo. Unaweza ukakuta kasichana ‘chembachemba’ lakini kakaagiza kuku mzima yaani kanakula kama Didier Drogba na ‘hakafanyagi’ mazoezi hata ya kukimbia nusu uwanja.

Kuna ambao wameshakutana na tukio kama hili na walilishughulikia kwa njia walizoona zinafaa.

Wewe ambaye linakutatiza ukikutana nalo hizi hapa njia tatu unazoweza kutumia kulishughulikia tukio kama hili.

Njia ya kwanza ni ya ‘Kidemokrasia’ inahusisha uhuru wa kuzungumza na kujielezea lakini pia inakupa haki ya kugoma ukiona kuna ulazima wa kufanya hivyo

Yaani ukiona kaja na timu, unamwambia ukweli mbele ya kikosi chake kwamba hujaridhishwa na tabia aliyoifanya, huu ndiyo uhuru wa kuzungumza. Lakini pia unaweza kuamua kutonunua chochote na mtoko ukafia hapohapo hii ndiyo tunasema haki ya kugoma.

Njia ya pili ni ya ‘Kitapeli’ unafahamu tapeli akishakuingiza mjini anavyokuacha kwenye mataa? Basi hivyo ndio unatakiwa uwafanyie na wao uwaache kwenye mataa. Yaani waache waagize, waagize, waagize tena na waagize zaidi. Kisha omba kwenda msalani halafu ukiwa huko tafuta upenyo wa kutimka zako.

Watakusubiri sana na mwisho wa siku watagundua tu kwamba tayari umeshatokomea hivyo watatakiwa kujilipia na kama hawana uwezo huo, basi jiandae kusikia stori ya namna walivyoosha vyombo na ‘makucha’ yao marefu ya kubandika.

Njia ya tatu ni ya ‘Kidiplomasia’ hii inahitaji utumie propaganda zaidi. Unachokifanya ni kumtumia salamu mpenzi wako kuwa hujapendezwa na tabia yake bila hata kumwamba kuwa ‘sijapendezwa’.

Unachotakiwa kufanya hapa ni rahisi angalia rafiki yake mzuri zaidi katika ile timu aliyoileta, kisha papo hapo mbele ya mpenzi wako anza kutengeneza ukaribu na kuonyesha kwamba umevutiwa naye kwa urafiki wa kawaida tu.

Msifie, mwambie mzuri na hakikisha unasifia vitu vya ukweli ambavyo hata mpenzi wako anaviona. Kisha ikiwezekana muombe hata namba ya simu, mwambie; “Shemu inabidi tuwasiliane bwana. Nipe namba zako.”.

Ndugu yangu, kwa njia hii, kuna uwezekano mkubwa watu wakaomba kuondoka kabla ya kumaliza mlivyoagiza na siku nyingine atakuja peke yake kwa heshima na adabu.