Mkereketwa wa Magufuli anayeamini siku moja nchi itapata rais mwanamke

Mara nyingi huonekana akiwa amevaa nguo zenye rangi ya bendera ya taifa.

Marysina Ngowi, ofisa utamaduni wa Manispaa ya Iringa, amejipambanua kwenye jamii kwamba ni mzalendo.

Katika siku zote nilizokutana naye, sikuwahi kumuona akiwa kwenye mavazi ya kawaida bila kuwa na chochote chenye bendera ya taifa hasa katika matukio muhimu.

Kwenye wasifu wake katika mitandao ya kijamii, ameweka picha ya Rais John Magufuli huku akijiita wazi ‘Mary wa Chama cha Mapinduzi’ hasa ‘Instagram’.

Kitaaluma ni mwalimu na hivi karibuni alivuma kwenye mitandao ya kijamii kutokana na video yake ya “Don’t Touch’ aliyowaimbisha wanafunzi wa kike na kiume akiwafundisha kutojiingiza kwenye mapenzi wakati wakiwa na umri mdogo.

“Niliwaimbia watoto wimbo wa ‘Don’t Touch’ baada ya taarifa kuonyesha bado mkoa wa Iringa una tatizo la ukatili wa watoto,” anasema.

“Ilibidi niwakusanye, niwafundishe wimbo huu huku nikigusa maeneo muhimu mwili wasiyotakiwa kuruhusu mtu mwingine ayaguse.”

Hivi karibuni alikuwa miongoni mwa walimu waliopata nafasi ya kutembelea miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya nne, ambayo ni pamoja na jengo la tatu la Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na daraja la Selander.

“Ninachopenda ni kufanya kazi kwa bidii, weledi na akili na ninachofurahi ni kwamba nina chombo ninachoweza kufanya nacho kazi nyuma yangu. Mimi ni mwenyekiti wa Jukwaa la Walimu Tanzania, Mkoa wa Iringa,” anasema Ngowi.

“Nataka kuonyesha uzalendo wangu kwa taifa langu na ninachotaka kueleza ni kuwa yote ambayo yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania chini ya Rais John Magufuli, sisi kama watumishi wa umma tunaunga mkono.”

Kabla hajawa ofisa utamaduni huyo kuanza harakati zake za kizalendo, alikuwa akifundisha Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa.

“Natamani niendelee kutumika kwenye jamii zaidi ya ninavyotumika. Nina uwezo huo na niseme tu nitaendelea kumsaidia Dk Magufuli hasa kwenye yale aliyoanzisha, mfano sera ya elimu bure,” anasema Mwalimu Ngowi.

Japo hapendi kuwa mwanasiasa, harakati zake zimewafanya baadhi ya watu kumuona kama mwanasiasa.

Anasema kinachowafanya wamuone hivyo ni zile harakati zake za kusambaza uzalendo hasa akiunga mkono kazi za Rais Magufuli kiasi cha kuingia kwenye malumbano na wanaompinga.

“Sijawahi kutamani kuwa mwanasiasa, lakini napenda kazi za wanasiasa hasa Rais Magufuli. Amefanya mabadiliko makubwa Tanzania ambayo kwa muda mrefu hatujawahi kuona. Navutika na shughuli zake lakini navutika na kazi za watendaji wengine chini ya CCM,” anasema.

Ndoto yake ni kuendelea kuwa mtumishi wa umma akiitumikia Tanzania kwa bidii na weledi hasa akiamini katika yale anayofanya.

Mkoani Iringa, Mwalimu Ngowi ameanzisha kwaya anayoiita kuwa ya wazalendo, akiwa amekusanya wanafunzi wa shule kadhaa. Kwaya hiyo hutumbuiza katika shughuli za kitaifa.

Kazi yake ya ofisa utamaduni wa manispaa imempa nafasi ya kutafuta vipaji mbalimbali na mara nyingi ameshiriki mashindano kadhaa yenye nia ya kukuza vipaji hivyo.

Kuhusu nafasi ya wanawake kwenye jamii, anasema wamepiga hatua kubwa sana kiuongozi na hilo linajidhihirisha kwa vitendo.

“Kuna wanawake wengi wameteuliwa, wamechaguliwa na wanafanya vizuri kwenye nafasi zao za uongozi,” anasema.

Anasema kwa mara ya kwanza Tanzania imefanikiwa kuwa na Makamu wa Rais mwanamke, Samia Suluhu jambo linalopaswa kujivunia.

“Wanawake tunaona hiyo ni nafasi kubwa na tunaaminika. Tumepewa nafasi nyingi mfano, mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wabunge. Na wanafanya vizuri,” anasema Ngowi.

Huku akimtaja mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kama mmoja wa viongozi wadogo wanawake wanaofanya kazi vizuri, Ngowi amewataka wale wenye ndoto za kiuongozi kutokubali kufifisha ndoto zao.

Anasema changamoto kubwa ni kwamba wanawake wengi hawajawa na uthubutu wa kutosha.

“Bado tuna woga na tunadharauliana wenyewe kwa wenyewe. Tumekuwa hatupendani kwa kiasi fulani na tukiona mwanamke anafanya vizuri tunaanza kuwa na figisufigisu za kutaka kumrudisha nyuma na kumpa ‘stress’ na mwisho wa siku hafikii ndoto zake,” anasema.

“Niseme tu wanawake tupendane. Unapoona mwanamke mwenzako anafanya vizuri, mtie moyo. Tuache majungu na fitina na kusingiziana maneno ya hovyo,” anasema.

Anasema kama wanawake wakiungana mkono na kushikamana, siku moja Tanzania inaweza ikapata rais mwanamke.