ANTI BETTIE: Mpenzi anakaa mbali na mimi, je fimbo ya mbali inaua nyoka?

Monday August 12 2019

 

Anti habari! Nina mpenzi yupo Bukoba na mimi nipo Dar. Tatizo lake ni kuwa bize muda wote, kibaya zaidi ubize unaongezeka ninapompigia simu hawezi kuzungumza nami zikazidi dakika tatu, lazima atakata na kunitumia ujumbe mfupi kuwa kuna kazi anafanya, wakati mwingine ni usiku.

Je, ananipenda kweli?

Sitaki kukujibu moja kwa moja anakupenda au hakupendi kwa sababu hana kizuizi cha kumpenda mwingine, hamjaoana.

Haya mambo ya mpenzi wangu...mpenzi wangu ni mtihani sana, mwanaume huna agano naye la kisheria na kidini una haki gani ya kumbana? Jitafakari na uchukue hatua ya kuhakikisha mnafunga ndoa au anakulipia mahari angalau uwe na sababu ya kumzuia kuwa bize na kulalamika kwa sasa wewe ni mpenzi wake kama wapenzi wengine na anaweza kukujibu lolote na kufanya chochote na hutakuwa na jinsi ya kumbana.

Halafu si unadai huyo ni mpenzi wako? Funga safari siku moja nenda kajionee kwa macho huo ubize wake unatokana na kazi kweli au? Chelewachelewa utamkuta mwana si wako. Inawezekana pia humpi muda wa kupumzika unapigia simu kila mara anachoka ndiyo maana anakukatia simu, ingawa si tabia ya kiungwana.

Hivi kusoma ndiyo kutafuta maisha?

Advertisement

Nina mpenzi wangu aliniambia amekwenda kutafuta maisha, baada ya mwaka kuisha nimefuatilia na kugundua kuwa yupo mkoa mwingine anasoma.

Je, ananifaa na kwa nini alinidanganya?

Kusoma ni miongoni mwa kutafuta maisha au hujui? Inawezekana aliona kukuambia anakwenda kusoma amalize ndiyo atafute kazi ungemkatisha tamaa ukizingatia labda anasoma kozi ya muda mrefu.

Inawezekana amekudanganya kwa sababu hiyo, lakini kulingana na mazungumzo unayozungumza naye ameona akikueleza mambo ya kusoma ili atafute maisha hautamuelewa.

Hata wewe kama hujasoma au umeishia darasa la saba, tafuta namna ya kujiendeleza.

Mwenza wangu kama kiredio kolu kwa umbea

Mwenza wangu amenishinda tabia natamani hata niachane naye. Kila ninalomwambia anamueleza rafiki yake ambaye huja kuniambia yote. Nikimuuliza anakataa ilihali niliyoambiwa yote nilizungumza na yeye tu.

Ananifaa au niachane naye?

Utafanya kosa kubwa kama utaachana naye pasi na kujiridhisha kuwa ni kweli huwa anamueleza huyo rafiki yake? Maneno ya kusikia usiyaamini hata kama unadai maneno unayoyasikia kwa rafiki yake ulizungumza na yeye tu. Inawezekana huyo rafiki yake kuna kitu anataka kwako hivyo anawafarakanisha na ameweka kinasa sauti kinachosikiliza mazungumzo yenu...huwezi kujua binadamu wana mbinu nyingi wanapotaka jambo lao.

Tafuta namna ya kujiridhisha kwanza, kisha uchukue hatua kama kumkanya na kumueleza madhara ya kutoa siri za ndani.

Advertisement