Mrisho Mpoto kuwatembeza watu peku wakati wa Mapinduzi ya Kimkakati

Saturday May 11 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Labda umeshawahi kukutana na Mrisho Mpoto au kuona picha zake akiwa peku peku (hajavaa viatu). Kwake sio nembo ya kumtambulisha kama msanii bali anachota madini kutoka katika uasili.

“Wataalamu wa afya wanasema kukanyaga chini ni afya ndio maana nimechagua mtindo huu, lazima uconnect (uungane) na nature (asili). Waswahili wanasema ardhi imemeza vingi pia, kwa maana hiyo unapotembea bila viatu unachota vilivyomo.”

Anasema amekuwa akisifika kwa umahiri wa masuala mbalimbali: Vingine ninavyofanya vinatokana na watu ambao wapo chini lakini hawakutumia talanta zao. Ndio maana kuna wakati watu wanasema Mpoto una uwezo. Mimi nachota maarifa kwa kutembea peku.

Kuhusu unadhifu wa kuvaa viatu na mavazi mengine ya gharama anasema vinamtenganisha binadamu na asili yake.

“Umaridadi umetutenganisha na uasili. Mtu anavaa vizuri. Mwonekano mzuri kweli unakufanya uonekane maridadi hasa lakini kiafya kuna vitu vingi unakosa. Kuna wakati mambo ya kisasa yanakata mawasiliano ya binadamu na asili yake ambayo ni udongo.

Mpoto ni msanii wa aina gani?

“Mimi ni msanii wa sanaa za maonyesho lakini zaidi ninafanya ushairi. Nimechagua ushairi kwa sababu ya kukienzi Kiswahili. Wenzetu hawana lugha moja halafu ya kwetu inapenda na kuheshimika duniani kote.”

Mapinduzi ya Kimkakati ni nini?

Anasema, “tunalenga kubadili fikra na kuwa na mijadala. Tunaamini tukiwekeza katika fikra za Watanzania hasa vijana tunaweza kubadilisha nchi yetu. Mchango wangu nataka kuwa Serikali iendane na mtazamo wa vijana. “Tunataka kuondoa fikra potofu katika jamii yetu kama zile Mzungu ana uwezo kuliko mtu mweusi.

“Tunataka vijana waache kuamini kuwa Uafrika ni bara la giza. Nataka waamini kuwa tunaweza kujitegemea na sio kusubiri mzungu asaze ndio atupe sisi.

Mpango wa kimkakati ni agenda kubwa ambayo itajadili miaka 20 kabla na baada ya Nyerere.

“Kikubwa ambacho kitatokea katika maadhimisho hayo pamoja na mambo mengine, itakuwa siku ambayo watu wote watatembea peku.”

Wewe ni rastafari?

Anasema hakuna kitu chochote kinachohusiana na imani katika kila kitu anachokifanya.

“Hizi nywele ni urembo tu lakini mimi sio rasta fari kwa maana kwamba nina imani zao kama vile kutokula nyama,” anasema.

Akiombwa ushauri kuhusu mapenzi anasemaje?

Anasema, “mapenzi yapo, hayana shujaa, hayana fomula. Mapenzi yako usiyafananishe na ya wengine. Maneno yangu hayawezi kumsaidia mtu kwenye mapenzi yake kwa sababu kila mtu ana namna yake ya kuishi na mpenzi wake.”

Anafafanua kuwa ni vigumu kutoa ushauri wa mapenzi kwa sababu watu huzama katika huba kwa sababu tofauti vivyo hivyo katika kuachana.

Kwa nini wasanii wanaingia kwenye mambo maovu?

Anasema sababu ya wasanii kuingia kwenye uovu ni kutoandaliwa na mfumo wa sanaa nchini.

“Ni kwa sababu hawajijui, ghafla mtu anakuwa msanii na kuanza kuishi kwa kuiga wengine. Akikwama anashindwa pa kushika. Wakati mwingine jina linakuwa kubwa kuliko kipato chake na hapo ndipo anapopotea njia,” anasema.

Wito wake kwa Baraza la Sanaa nchini (Basata) kuandaa mazingira mazuri ya kuwafanya wasanii wajitambue na hiyo itawasaidia kutoingia katika matendo maovu.

Advertisement