Msongo wa mawazo kazini na jinsi ya kukabiliana nao-1

Hii ni aina ya msongo wa mawazo unaowasumbua sana wafanyakazi na watu wengine walio makazini, na tatizo hili limekuwa likisababishwa na mazingira, umuhimu wa kazi na uwezo wa mtu husika kazini. Kwa pamoja mazingira haya ndiyo huleta msongo wa mawazo kwa mwajiriwa. Sababu nyingine zinazotengeneza msongo wa mawazo kazini ni nafasi ya mwajiriwa katika ofisi husika, mahusiano baina ya waajiriwa ofisini, pia uhusiano baina ya viongozi na waongozwa. Wakati msongo wa mawazo unapozidi huwa unachangia uwepo wa matatizo kwa waajiriwa na mara kwa mara husababisha mtu kuwa mgonjwa au mwili kutokuwa katika hali yake ya kawaida.

Hamasa ya kazi inapokuwa chini sana mfanyakazi anakuwa anawaza kazi yake ofisini au nafasi yake haina maana na si muhimu na kuhisi kuwa muda wowote anaweza kufukuzwa na nafasi kujazwa na mtu mwingine. Wakati huohuo msongo wa mawazo uliozidi husababishwa na hali ya mfanyakazi au mwajiriwa anapokuwa na majukumu mengi na yenye kuchosha na usimamizi mkali wenye kusudio la kuzuia makosa ya aina yoyote. Kwa namna yoyote mazingira haya humfanya mwajiriwa kuwa katika mazingira hatarishi ya kupata msongo wa mawazo kazini, kitu ambacho kinasababisha udhaifu wa mwili au ugonjwa.

Vyanzo vya msongo wa mawazo kwa mwajiriwa vimegawanyika katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni vyanzo vya msongo wa mawazo kutoka ndani ya mtu mwenyewe, msongo huu hutokea ndani ya mtu husika na hasa inaweza kujumuishwa kwenye tabia yake. Pia uwezo pekee wa mtu/mwajiriwa kuvumilia au kubeba majukumu magumu aliyonayo, kujiamini na woga juu ya kazi yake. Kundi la pili ni vyanzo vya msongo wa mawazo kutoka nje mtu, vyanzo hivi kidogo ni tofauti kwani ni vya kutoka nje ya mtu mwenyewe, vyanzo hivi vinajumlisha vitu vyote vilivyo nje ya mazingira ya kazi pamoja na uwezo wa mtu husika kazini. Vitu kama vile matatizo ya kifamilia, ugumu wa maisha, changamoto za kipato na za kimazingira. Kwa pamoja, vyanzo hivi vinaweza kusababisha dalili za matatizo ya kiafya kwa mwajiriwa, vitu ambavyo kama havitachukuliwa hatua za mapema ugonjwa unaweza kukua na kuleta madhara makubwa zaidi kiafya au kiakili (health and psychiatric problems).

Ingawa vyanzo hivi vya msongo wa mawazo, vinatofautiana kutoka kwa mfanyakazi mmoja na mwingine, kulingana na mazingira ya kazi na kazi yenyewe. Hii hutokana na kila mtu kwa namna yake pekee ya maisha, na upekee huu unaweza ukawa kwenye maeneo kama vile matatizo ya kifamilia, sababu za kiuchumi, kifedha, hali hii huleta misongo mbalimbali ya mawazo kwa waajiriwa na madhara yake ni dhahiri.

Itaendelea...