TUONGEE KIUME: Muda sahihi wa kuondoka baa ni upi?

Monday August 12 2019

 

By Kelvin Kagambo

Ukianza kuona kila mhudumu ni mzuri, ni dalili kwamba umeshalewa vya kutosha, nenda nyumbani kwa mkeo, ukalale. Kauli hii inazalisha moja ya swali muhimu sana ambalo labda linaweza kuwafaa walevi, wanywaji au mtu yeyote mwenye ukaribu na aina hiyo mbili ya watu; Je, ni muda gani sahihi wa kutoka baa?

Ni swali la kujibiwa kwa uzoefu sana. Kuna wengine wana jibu rahisi tu, kwamba ukiona hela ulizoingia nazo zimeisha, huo ni muda mzuri zaidi wa kutoka baa. Wakati wapo wanaosema kwamba ukiona vitu vyako vya thamani vinatoweka katika mazingira ya kutatanisha jua wakati wa kwenda nyumbani kwako umewadia.

Yaani mfano uliingia na pochi ikiwa mfuko wa nyuma wa suruali, saa nzuri mkononi, na ‘smartphone’ yako ya Sh450,000. Ukapewa kiti, ukaagiza mambo yako, baada ya raundi kadhaa, mara saa mkononi huinoni, pochi imehama mfuko wa nyuma na hujui imehamia mfuko gani, simu haipo mezani, haiko mfukoni, haiko mkononi na kichwani haziko akili hata za kuomba mtu akusaidie kukupigia ili usikie ikiita ujue iko wapi.

Ukiona umefika huko, nyanyuka, nenda msalani, jisaidie kisha ondoka bila kuaga, ukapumzike.

Ulimi wako pia ni kitu muhimu ukiwa baa ukianza kuona ukitaka kuzungumza maneno ya kawaida ulimi unakuwa mzito, lakini ukitaka kutukana, tusi linakuja kwa ulaini na kuteleza kama tonge la ugali juu ya mlenda, wala usijiulize mara mbili; ondoka hapo tena mbiombio.

Pia, ukianza kuona mikono inawashawasha hiyo si dalili nzuri. ondoka. Kuwasha si ile ya kuwasha dalili ya kupata hela, hapana. Ikiwasha kama ambavyo Matumla alikuwa akiwashwa mikono ulingoni, ondoka kwa sababu haitaacha kuwasha hadi upate mtu wa kumlima makonde hapo baa. Na inaeleweka kabisa, suala la kumtia mtu mangumi linataka ujuzi, hakuna mlevi wa pombe aliyewahi kushinda ugomvi kwa kupigana.

Advertisement

Kwa hiyo unaweza ukajikuta unatoka baa ukiwa umeacha kila kitu hapo hela, simu, akili, meno na hata roho.

Lakini jibu la uhakika ni lipi? Uhakika ni kwamba muda sahihi wa kutoka baa ni pale ambapo umekunywa lakini bado hujalewa. Bado pombe haijapanda kichwani kisawasawa.

Kwa sababu ni muda huu pekee ndio unakuwa na akili ya kufanya maamuzi kulingana na mazingira. Yaani kabla hujalewa unakuwa na akili ya kujua ugomvi si kitu kizuri, sitakiwi kupigana baa, pesa yangu imeisha natakiwa kurudi nyumbani, nitapoteza simu nikishalewa na hawa baamedi ni wafanyakazi wa hapa baa kwa hiyo si makahaba, wako ofisini kama mimi nilivyotoka ofisini na kupitia hapa.

Ukiwa umelewa, huwezi kuelewa yote haya. Ondoka, rudi nyumbani kwaa mkeo na watoto kwa kuwa wamekumisi.

Advertisement