TUONGEE KIUME: Mwambie binti yako kuwa, kutokuolewa si dhambi

Sunday September 29 2019

 

By Kelvin Kagambo

Ukipata muda kaa na binti yako na umwambie kuwa kutokuolewa si dhambi na haijawahi kuwa dhambi. Kwa sababu huku mtaani wenzie wamechanganyikiwa kwa kuwa wamefikia umri wanaodhani ndiyo wa kuolewa, lakini bado hawajazipata hizo ndoa. Wanahisi wana gundu na bahati mbaya, wanahisi si wazuri wa kutosha au labda hawana tabia nzuri au kuna kitu wanakosea.

Kaa mwambie binti yako kuwa, akifikia umri huo na hajaolewa si kwamba ana gundu au bahati mbaya. Kuolewa hakuna uhusiano wowote na bahati nzuri kwa sababu ndoa si kitu kizuri wala si kitu kibaya hakibebi hali yoyote kati ya hizo mpaka itakavyoamuliwa na mhusika. Ukiamua kuona ni nzuri basi ni nzuri, ukiamua kuona kinyume, huwa hivyo pia.

Asidhani yeye si mzuri, mwambie ni mrembo sana lakini ndoa haziji kutokana na uzuri wako, zinakuja kutokana na makubaliano ya wawili walioamua kuoana ndiyo maana kuna wanawake wazuri walioolewa na kama wapo wabaya, basi wapo waliolewa pia.

Labda hana tabia nzuri ila mweleze kuwa ndoa si mshahara wa tabia njema. Na mwambie kwamba hatakiwi kuwa na tabia nzuri kwa sababu ya kuolewa, anatakiwa awe hivyo kwa sababu yeye ni binadamu. Mpe mfano kwamba uasherati si tabia mbaya kwa sababu hakuna mwanaume anayetaka kuoa mwanamke mwasherati, bali ni tabia mbaya kwa sababu uasherati ni uchafu.

Msisitizie kwamba jeuri, kiburi, mvivu na vitabia vyote vichafu, si vichafu kwa sababu wanaume watamuogopa, ni vichafu kwa sababu ataogopwa na kila binadamu hakuna bosi anayetaka mfanyakazi kiburi, hakuna shangazi anayependa mpwa jeuri kama ambavyo hakuna mwanaume anayependa kuoa mwanamke wa hivyo, mweleweshe awe mtu mwema si kwa sababu ya ndoa, bali kwa sababu dunia inahitaji watu wema.

Hakikisha husahau kumdadavulia kuwa kutokuolewa ni dhambi kwa wanawake wasiojielewa kwa nini wapo duniani. Ajue kuwa siku zote wanawake wasiokuwa na ndoto zozote, ndoto yao huwa kuolewa.

Advertisement

Mwanamke ambaye hana mpango wa kuja kuwa mmiliki wa gazeti kubwa la fasheni Afrika Mashariki, ndoto yake huwa ni kuolewa. Mwanamke ambaye hana ndoto kubwa ya kuwa Spika wa Bunge au mwanasiasa mkubwa msaidia watu, ndoto yake kubwa huwa ni kuolewa. Mwanamke ambaye hajui yupo duniani kwa ajili ya nini, huishi kwa ajili ya kuolewa, kubebeshwa mimba, kuzaa, kulea watoto na kuzeeshwa, kufariki na kuzikwa.

Sijakwambia umwambie ndoa ni kitu kibaya au asiolewe, hapana. Mwambie ndoa inaweza kuwa kitu kizuri lakini kamwe asikae chini kuisubiri. Aendelee na maisha yake, aendelee kufukuzia ndoto zake, ndoa itakuja itamkuta huko huko mbele ya safari.

Advertisement