ANTI BETTIE: Naijali familia yake lakini yeye hafikirii chochote kuhusu yangu

Mume wangu ninampenda na wakwe zangu pia. Kila nikipata likizo huwa nakwenda kuwasalimia na ninafanya hivyo miaka yote tangu niolewe. Lakini mume wangu hajawahi kufanya hivyo hata kuwasalimia tu sikumbuki mara ya mwisho ni lini.

Hii hali inaniumiza na sijui nifanye nini ili abadilike.

Hujasema kama umewahi kuzungumza naye kuhusu kutofurahishwa na hali hiyo, kuna baadhi ya binadamu hawafanyi kitu hadi wahimizwe au kusukumwa.

Watu hao huona bora mambo yao kuliko ya wengine, inawezekana mumeo ni mmoja wao hivyo jukumu lako ni kuhakikisha unasema naye na kumkumbusha umuhimu wa wazazi wenu. Hujaniambia ushiriki wake kwao, inawezekana hata kwao ni wewe umeamsha mawasiliano yao, hivyo endelea kumhimiza na ikiwezekana kama ana familia sikivu na yenye maamuzi uwashirikishe wana familia yake kama kaka zake, shangazi zake.

Ikiwa unahisi unaweza kuibua hisia mpya na zinaweza kutokea kwa wanafamilia ya mumeo kuhisi kuwa unataka kumteka mtoto wao aelemee kwenu, washirikishe waliosimamia ndoa yenu au mshenga ili wakusaidie kumshauri na kumkumbusha umuhimu wa watoto kuwajali wazazi wao.

Pia nakupongeza licha ya mumeo kutojali familia yenu hukuchagua upande kwa kuitelekeza yake pia, uliendelea kutimiza majukumu yako ya kibinadamu.

Nimezaa na mume wa mtu bila kujua nifanyeje?

Habari Anti!

Naomba ushauri, nimezaa na mwanaume bila kujua kama ni mume wa mtu. Tulikuwa tukimlea vema mtoto kwa kushirikiana, mtoto alipotimiza miaka miwili ndiyo kaniambia kuwa ameoa na ana watoto wawili. Nifanyeje na bado ninampenda?

Pole sana, mwanaume ndiyo ana makosa kwa sababu alikuficha labda ungejua mapema usingefika naye mbali kiasi hicho.

Kwa sababu ameshaoa huna namna ya kufanya zaidi ya kukaza moyo na kuachana naye kwa makubaliano ya kumtunza mtoto wake. Hujaniambia ni dini gani, angekuwa Mwislamu labda mngefikiria kumshirikisha mkewe na kufunga ndoa halali ili usiendelee kubomoa ndoa ya watu, kama ni upande wa pili huna namna zaidi ya kukubali matokeo.

Najua utaumia kwa sababu ni mwanaume uliyempenda na pengine hajakukosea, lakini ili ubaki salama na usiwe na deni moyoni huna budi kuachana naye.

Achana naye kabla hujajivunjia heshima kwa jamii mkewe akifahamu na kuanza kukusumbua, pia mkanye huyo mwanaume kwa tabia aliyoifanya ya kutokukuambia ukweli.

Pia msisitize afanye kila njia aifahamishe familia yake kuhusu mtoto wako ili asije kukosa haki zake za msingi mbele ya safari.

kiwezekana ufahamu wanapoishi wazazi wake na umpeleke mtoto, kisha amtambulishe kwa ndugu zake yaani watoto aliozaa na mkewe.

Yote haya yatakuwa na maana nje iwapo utakaza moyo na kuachana na huyo mume wa mtu.

Kuwa naye ni kujizibia riziki, kwa sababu huwezi kupata mwanaume wa maana ukiwa unaye mwingine.

Suala lako liwe fundisho kwa wanawake wengine kama wewe ambao wanaanzisha mahusiano bila kuyachunguza na kufika nayo mbali, kabla ya kuamua kuzaa na mwanaume kwa mustakabali wa mtoto ajaye hakikisha unafahamu kwa uchache kuhusu unayezaa naye.