Namna bora ya kutunza afya ya mtoto nyumbani

Sunday May 12 2019

Usafi ni moja ya nyenzo bora za mtu kuwa na afya njema. Ili mtu awe na afya bora, hana budi kuzingatia usafi wa mwili, mazingira anayoishi pamoja na vile anavyokula na kunywa.

Magonjwa kama kipindupindu na kuhara husababishwa na kula vyakula au kunywa vinywaji visivyo safi na salama, upele na mba husababishwa na kutokuoga mara kwa mara na magonjwa ya meno na fizi nayo husababishwa na mabaki ya chakula kwenye meno. Leo tunakuletea namna mbalimbali ambazo mzazi au mlezi unaweza kuzitumia ili kutunza afya ya mtoto wako kwa kuzingatia usafi;-

Usafi wa Ngozi

Ogani kubwa kabisa katika mwili wa binadamu ni ngozi. Pamoja na kazi nyingi, ngozi hufanya kazi ya kulinda mwili dhidi ya vimelea vya magonjwa. Tunashauriwa kuzitunza ngozi za watoto wetu kwa kuwaogesha kila siku kwa maji safi ya vuguvugu na sabuni ili kuondoa vimelea vya magonjwa juu ya ngozi ambavyo huwasababishia magonjwa ya ngozi watoto. Vilevile, nyuso za watoto zisafishwe kila siku wanapoamka asubuhi na kila wanapooga kwa maji safi ya vuguvuvgu na sabuni ili kuzuia inzi wenye vimelea vinavyoweza kusababisha magonjwa ya macho kama vile trakoma kwa watoto na hatimaye upofu.

Usafi wa Kinywa

Ni vema kutunza meno ya watoto wetu kwa kuwapigisha mswaki kila siku asubuhi na ikiwezekana kila baada ya kula. Mfundishe mtoto namna ya kuswaki vizuri ili kuondoa mabaki ya chakula katikati ya meno ili kuzia meno yasioze na magonjwa ya fizi kwa watoto.

Advertisement

Usafi wa mikono

Wazazi tuwanawishe watoto wetu mikono kwa maji safi ya vuguvugu yanayotiririka na sabuni kila wanapotoka kucheza, kabla ya kula, baada ya kula na baada ya kutoka chooni. Watoto wadogo hasa wanaotambaa mara nyingi huweka mikono yao mdomoni, hivyo ni muhimu kuwanawisha mikono yao mara kwa mara. Vilevile wazazi tuwafundishe watoto kunawa mikono yao na pia kuwakanya wasicheze mahala pachafu kama vile karibu na vyoo au majalalani.

Uzoefu unaonesha kuwa magonjwa mengi ya kuambukiza hasa ya kuhara yanayo-sababisha vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kila mwaka yanasambaa kupitia mikono yao.

Usafi na usalama wa maji

Ikiwa vyanzo vya maji pamoja na vyombo vya kuhifadhia maji si safi na salama, magonjwa kama vile kipindupindu, mchochota wa ini (hepatitis) na homa ya matumbo huweza kuwapata watoto. Wazazi tunashauriwa kuwa maji ya kunywa tunayowapa watoto yawe yamechemshwa vizuri kwa kiwango cha nyuzi joto la 100 (yaani hadi maji yatokote). Katika baadhi ya maeneo, watu huchuja maji kwa kutumia vitambaa safi kasha huyachemsha na kuyahifadhi kwenye vyombo safi. Vilevile mzazi hakikisha kuwa maji yanayotumika kusafishia vinywa vya watoto, kuogeshea watoto, kupikia na kufulia nguo za watoto yawe yanatoka kwenye vyanzo safi na salama.

Usafi wa matunda

Matunda yanayonunuliwa sokoni mara nyingi huwa yametoka mashambani ambapo yalikwisha pigwa madawa na pia kukusanya uchafu wakati wa usafirishaji na hata yakiwa sokoni. Mzazi unashauriwa kusafisha matunda kwa maji safi yanayotiririka kabla ya kuyamenya na kumpa mtoto. Kufanya hivyo kutasaidia kutunza afya za watoto wetu kwa kuwaepusha na magonjwa ya kuhara na kipindupindu.

Usafi wa Mazingira

Mazingira safi hufaya mtoto awe na afya bora. Ili kutunza afya za watoto kwa kuwaepusha na magonjwa ya ngozi kama vile upele na mba, mzazi unashauriwa kufanya usafi wa mazingira wa mahali ambapo mtoto hupendelela kucheza na mahali anapolala. Kadri watoto wanavyokua, wafundishe kufanya usafi wa nyumbani pamoja na mazingira ya nje na eneo lolote wanalotumia kwa muda wowote.

Advertisement