TUONGEE KIUME: Ndoa ingekuwa mtu ingefanana hivi

Watafute watu kadhaa walio kwenye ndoa, mathalani watu 10 hivi.

Kisha waambie unataka kuumba mtu mwenye taswira ya kufanana na ndoa, hivyo wakusaidie kupata picha kwamba mtu anayefanana na ndoa anaweza kuwa anaonekanaje? Niamini mimi, utaumba mtu mbaya kiasi kwamba kama marehemu, gwiji wa muziki wa Tanzania Dk Remy Ongala angekuwa hai, angesimama mbele ya vyombo vya habari na kutangaza kuacha kujinasibu kuwa ana sura mbaya kuliko wote.

Kwa nini? Kwa sababu leo hii tunaishi katika dunia ambayo kila mtu anayeongea kuhusu ndoa anaizungumzia kwa taswira za kutisha. Mama, bintiye anapoolewa atamwambia; mwanangu, ndoa si lelemama, ina changamoto nyingi sana, misukosuko, ugomvi, purukushani na makorokoro ya kila namna, kwa hiyo inahitaji uvumilivu wa kiwango kikubwa sana.

Baba naye, wakati kijana wake anaoa atamuelezea ya kufanana na hayo. Mwanangu ndoa ngumu, wanawake wana matatizo mengi, kuishi nao kunahitaji moyo wa kustahimili na akili kubwa sana, changamoto ni nyingi.

Watu hawa wawili wakikutana ndani ya nyumba ni kama Chadema na CCM kama sio Simba na Yanga, upinzani wa kufa mtu. Kila mtu kwa nafasi yake akili yake imejazwa habari hasi kuhusu ndoa. Habari hasi ambazo kimsingi zinaweza kuwa za kweli, lakini zinasemwa sana, kiasi kwamba ndoa inaonekana lazima iwe hivyo tu. Kwamba kuwa na furaha ndani ya ndoa… Mungu wangu, huo ni muujiza.

Lakini ni kweli iko hivyo? Au labda kwa misingi ya kidini tuseme Mungu aliamuru tuoane ili iwe kama adhabu kwa Adamu na msaidizi wake Hawa ya kuyapinga maagizo pale Edeni, sitaki kuamini.

Imani yangu ni kwamba ndoa inastahili kuwa tulizo kubwa kuliko kawaida, inastahili kuwa kimbilio kuu kwa mwanandoa mmoja anapopata matatizo mazito.

Mke akikumbwa na janga akimbilie kwa mumewe, akumbatiwe vizuri tu na kwa upole apewe maneno ya kutia nguvu na kuibua upya imani yake. Na ni hivyo kwa mume pia, purukushani anazokumbana nazo siku nzima ziyayushwe kama barafu juani kwa upendo wa daraja la juu sana kutoka kwa mkewe.

Ndoa haistahili kabisa kuwa namna ambayo watu wengi wanaifikiria kwamba ni ngumu. Labda tuamue, tuseme sisi ndiyo wagumu. Tusiipake matope ndoa.

Hata nakumbuka kuna kichekesho kimoja kuhusu ndoa, tuliwahi kukiongelea hapa hapa. Kwamba mwanaume akifa, akiwa mbinguni, kitu cha kwanza kuulizwa kabla ya kupimiwa dhambi zake ni kwamba Je duniani ulikuwa umeoa? Jibu likiwa ndio, Mungu atasema “mpelekeni peponi moja kwa moja mtu huyu. Moto alishaupata huko huko duniani.

Hapana, ndoa haistahili kuwa moto bali kinyume chake. Yaani pepo.