TUONGEE KIUME: Ni mambo ya siasa au kweli hatuna nguvu za kiume?

Sunday May 26 2019

 

By Kelvin Kagambo

Kuku wa kienyeji kwa mbio hana mpinzani —lakini ukimfunga kamba mguuni kwa muda mrefu, kisha ukamfungua hatokimbia. Atakaa palepale alipokuwa muda wote kwa sababu akili yake inamwambia bado amefungwa kamba.

Ndio shida tunayopitia wanaume kipindi hiki. Ukifungua gazeti unakumbana na tafiti za jinsi wanaume wa sehemu fulani wanavyoongoza ligi ya tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

Ukiwasha redio, utasikia mahojiano na anayejiita daktari bingwa wa tiba mbadala, anataja namba zake za simu na ilipo ofisi yake ili wanaume wote wenye tatizo la upungufu wa nguvu za kiume wakamuone, ana dawa inayotibu kwa kutoa matokeo ya haraka kama chumvi, ndani ya siku tatu tu unapona kabisa.

Ukiwasha TV, tangazo lingine hili hapa. Mtabibu mwingine anaelezea namna ya kumaliza tatizo la upungufu wa nguvu za kiume kwa dawa alizozitengeneza kwa kutumia matunda na mitishamba baada ya kuzifanyia utafiti wa miaka minne.

Utachoka; utasema utoke nje, huko utakutana na kibao kimebandikwa kwenye nguzo ya umeme, kinasomeka; Dokta Mfumalanga kutoka Handeni. Anatibu nguvu za kiume… kisha namba ya simu chini ya maneno hayo kwa ajili yako kumpigia, upate dawa.

Ukiingia kwenye mitandao ndiyo utapotea kabisa, kila sehemu habari ni wanaume na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume siku nzima. Tatizo linazungumzwa kwa herufi kubwa kana kwamba ni tatizo kubwa kuliko tatizo lolote kuwahi kutokea Tanzania.

Advertisement

Kila unachokigusa siku hizi kinahusishwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume. Wanawake wanaouza mihogo mibichi, karanga na nazi za kutafuna barabarani wanakushawishi kununua kwamba zinaongezea nguvu za kiume. Anayeuza supu ya pweza biashara haidodi kwa sababu inasemekana inaongeza nguvu za kiume. Anayeuza juisi ya miwa naye ana bango limeandikwa safisha kibofu, ongeza nguvu za kiume kwa kunywa juisi ya miwa — fujo kila mahali.

Hata juzi kuna waziri alikuwa anatushawishi Watanzania tununue korosho za Kusini zilizoko ghalani kwa sababu inasemekana zinaongeza nguvu za kiume.

Cha kujiuliza ni je, kweli hili tatizo lipo kwa namna linavyozungumzwa, au ni vile linaongelewa kwa kupakwa rangi na kunogeshwa sana kiasi kwamba linaingia kwenye vichwa vya watu kufikia hatua hata wasiokuwa na tatizo wanakuwa na mashaka na afya zao.

Isije ikawa siasa za kibiashara, kwamba watu wametengeneza tatizo ili wajifanye wana suluhisho, wachume pesa zetu.

Hii ndio kama stori ya kuku wa kienyeji tu, tunafungwa kamba kwa kulishwa taarifa nyingi kuhusu afya zetu, ili hata siku wakitufungua, tusiende kokote, tuwe chini yao.

Advertisement