ANTI BETTIE: Ni rafiki yangu, ananisaidia ila tatizo ni mchonganishi, mlevi

Nina rafiki yangu ni mchonganishi na mlevi, pamoja na tabia hizo ananisaidia nikiwa na shida na nikikaa vibaya ananichonganisha na watu.

Nifanyeje?

Sina uhakika kama huyu ni rafiki kama unavyomwita, huwezi kuwa na rafiki anayekuchonganisha na watu, bila shaka huyu ni adui yako.

Kukusaidia kwenye shida haimaanishi anakupenda na ana sifa za kuitwa rafiki, anafanya hivyo ili kukujua kwa undani una shida gani ili iwe rahisi kwake kukufarakanisha au kukudhalilisha kwa watu.

Pia umesema huyu unayemuita rafiki yako ni mlevi inawezekana anayafanya hayo hususani hilo la uchonganishi akiwa amelewa, hivyo jaribu kumsaidia kuacha au kupunguza pombe, tofauti na hapo hata wewe hutakuwa na sifa ya kuitwa rafiki kwa sababu humsaidii huyo unayemuita rafiki yako kuwa katika hali nzuri.

Inawezekana si vizuri kuingilia maisha binafsi ya mtu, hata hivyo kwa maana ya urafiki una kila sababu ya kumsaidia kwani kufanya hivyo utamuepusha na mambo mengi kama vile matumizi mabaya ya fedha pamoja na kulinda afya yake.

Kuna uwezekano mkubwa akiacha pombe akawa si mchonganishi na akaendelea kuwa rafiki mwema kwako.

Sioni siku zangu na sina mimba

Habari Anti!

Sioni siku zangu na sina mimba je, linaweza kuwa ni tatizo kwenye mwili wangu?

Sidhani kama ni tatizo kwa sababu wapo watu wanawake wengine wengi tu ambao huwa hawazioni siku zao na hawana shida yoyote mwilini wakiwamo wanawake wanaonyonyesha.

Hata hivyo mwili unahitaji vipimo ili kujiridhisha kama ni hali ya kawaida au kuna shida, hivyo ni vema ukaonane na daktari akufanyie uchunguzi wa kitaalamu ili kupata jibu kamili.

Mara zote unapoona kuna hali isiyo ya kawaida katika mwili wako hata kama huumwi unachopaswa kufanya ni kwenda kupata ushauri wa kitabibu kwa wataalamu kuliko kukisia kisia labda itakuwa hivi au vile unaweza kusababisha tatizo kubwa.