VIDEO: Ofisa rasilimali watu aliyegeukia uchimbaji madini, pia ni dereva wa kijiko kwenye mgodi

Sunday September 15 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Ukikutana na Sophia Mbimbi akiwa amevaa nguo za kazi awapo mgodini, utapata ukakasi kumtofautisha pale utakapokutana naye akiwa nje ya mgodi.

Sophia ni mrembo na anayejipenda, lakini shughuli zake ni uchimbaji wa madini kwenye migodi.

“Kazi ngumu hazimkomazi mwanamke ila zinampa heshima, kama umekosa kazi fanya yoyote ilimradi upate kipato halali.” Hivyo ndivyo anavyojinasibu Sophia akitetea kazi anayofanya ambayo baadhi ya wanawake huamini itamkomaza.

Anasema baada ya kuacha kazi aliyokuwa akifanya awali na kujitosa migodini tena akichimba madini chini ardhini, kazi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikifanywa na wanaume pekee.

Anasema kazi hiyo imemfanya azidi kuwa mrembo na ajiamini, tofauti na mtazamo wa wengine.

Akizungumza kwenye viunga vya mji wa Geita, Sophia anasema haikuwa rahisi kujikita kwenye kazi hiyo, alitumia akili ya ziada kuaminisha watu kuwa anaweza.

Advertisement

“Nilianza kazi hii mwaka 2013 nimefanya kwa miaka sita, mitatu nilikiwa ofisa rasilimali watu (HR) kwenye Mgodi wa Tanzanite One kabla haujafungwa, kiu ya mafanikio ilinifanya nitamani kufanya kitu tofauti,” anasema.

Anasema akiwa anafanya kazi kwenye kitengo hicho alikuwa akihudumia watu wengi wakiwamo wachimbaji madini, asilimia 90 wakiwa ni wanaume.

Anasema alizoeana nao wengi, kiasi cha kutamani kufanya kazi mgodini baada ya kusikiliza stori kuhusu wanayoyafanya wakiwa huko ardhini wanakoyachimba.

“Niliwashirikisha wazo langu, nilipata hamasa hiyo baada ya kuona hakuna mwanamke anayefanya kazi hiyo badala yake ninahudumia wanaume pekee.

“Nilijipa moyo ninaweza ingawa sikuwa najua kiuhalisia nitakutana na nini zaidi ya kusikia stori juu juu ya kinachofanyika huko,” anasema.

Anasema pia alijiridhisha kwa Wazungu aliokuwa akifanya nao Mgodi wa Tanzanite One kama amewahi kuwapo mwanamke aliyefanya kazi chini ya mgodi. “Waliniambia hakuna historia hiyo, na hata kwenye migodi mingine midogo midogo ukiwamo Nahoro,” anasema. “Historia hiyo ilifanya iwe changamoto kweli kweli mimi kufanya kazi hiyo, wengi walikuwa wanajiuliza kwani Sophia amekuwa chizi au vinginevyo nikasema hapana nataka kufanya.

“ Wazungu wakawa wananiuliza unataka kujaribu? Nikawa ninawajibu, hapana nataka kufanya.”

Anasema kwamba hatimaye alikata shauri na kuonana na mkuu wa kitengo alichokuwa anafanyia kazi akamueleza nia yake.

“Alilipokea vizuri, sikuamini kwa sababu alikuwa mkali sana, ingawa maswali yalikuwa mengi na nilitumia muda mwingi kumrekebisha kutoka mawazo aliyokuwa nayo juu ya azma yangu na uhalisia”.

Anasema alimuuliza anataka kwenda kufanya au kuangalia, kwa sababu kwa miaka mingi hajamuona wala kusikia mwanamke anatamani kufanya shughuli ile.

Anafafanua kuwa alimshawishi ikiwamo kumuahidi kuwa atafanya vizuri kuliko wanaume.

“Majibu hayo hayakutosha ikabidi vifanyike vikao kumjadili ambapo baadhi ya Wazungu waliokuwa wasimamizi wa mgodi walikuwa wakilipinga suala hilo kwa hoja za kiusalama.

“Kwenye vikao kukawa na pande mbili zinapingana na kulikuwa na babu wa Kizungu anaitwa Anthony akashauri wanipe wiki mbili za mafunzo ili waone nitafanya nini.

Anasema alishiriki mafunzo ya wiki mbili na wanaume kama majaribio, akafanya vizuri zaidi yao na kuaminiwa kuwa anaweza.

Safari chini ya ardhi inaanza

Anasema kwa kuanzia alifanya kama kama opareta wa simu na mitambo ya lifti kwa muda mfupi juu ya ardhi eneo ambalo kuna mawasiliano kati ya chini na juu.

“Moja kwa moja ilitakiwa nishuke chini ambako ni kama urefu wa viwanja vinane vya mpira kutoka juu mpaka chini si karibu ni mbali na kule ni giza kweli kweli, unaposhuka kuna kitu kinaitwa shafti lakini huko ndani kuna njia ‘mipenyezo’, nikawa nashuka siku ya kwanza nilishuka na vijana watano walifurahi sana.

“Kabla ya kuondoka kuna kusali baada ya sala nikatambulishwa na ndiyo niliokuwa nawahudumia na kuwahangaikia nilipokuwa HR, walifurahi nilibebwa kwelikweli.

Anaeleza siku ya kwanza alifanya kazi vizuri kwa sababu walimlinda na kumuelekeza kila hatua.

Anasema akiwa anafanya shughuli hiyo ardhini Wazungu, Wahindi waliokuwa huko walimshangaa na walipinga pia asiwepo.

Anafafanua kutokana na umahiri aliouonyesha na kitendo chake cha kujiamini huku akifanya kazi usiku na mchana, walimuogopa na yeye akasonga mbele.

Sophia anasema hakuishia hapo alifundishwa kuchonga miamba kwa kutumia mashine ya umeme wakati wa kutafuta madini ya Tanzanite, mashine inayohitaji nguvu, alijizatiti akaweza, lakini hakupewa cheti.

“Changamoto kubwa nikiwa mgodini ilikuwa nataka kujua tumezalisha nini kama umeiba nakwambia rudisha au tuibe wote tuone mapato yatapatikana vipi.” Kwa hiyo baadhi ya watu aliofanya nao kazi wakaanza kumchukia, wakisema anatumika na serikali.

Mgodi unafungwa

Baada ya kujengwa ukuta mgodi wa Tanzanite One ulifungwa na huo ukawa mwisho wa Sophia kufanya kazi kwani wafanyakazi wote walipewa barua na kuambiwa wangeitwa tena.

Kiu ya mafanikio iliendelea kwake hakusubiri barua akaamua kusonga mbele. “Sikwenda tu kukaa nyumbani, nilikuwa na akiba kidogo kwa hiyo nikaenda chuo, Shinyanga nikajifunza kuendesha motagreda na mashine ambazo kuna mwanamke mmoja kutoka Uganda alisomea (ni aina ya kijiko kile kinachotumika kwenye ujenzi wa barabara kubwa na madaraja).

Huku nako alikutana na kikwazo kwa walimu waliomwambia aachane na kusomea udereva wa motagreda kwani ni mgumu.

Anasema baada ya kutafakari aliamua kusomea fani hiyo hadi alipohitimu na kufanikiwa kupata mafunzo kwa vitendo katika mgodi wa Geita Gold Mine (GGM).

“Nikabahatika kupata nafasi ya mafunzo kwa vitendo GGM na nikafanya walisema hawakuwahi kupata mwanafunzi kama mimi, ilikuwa ngumu mwanzo wakitaka nikatafute barabarani, nikawaambia mimi ni mwanamke, Mtanzania na GGM ipo Tanzania kwa nini nikafanye barabarani wakaanza kulegea na wakanipa nafasi.”

“Nilianza kazi, nilikuwa nikiendesha madereva wakija kupakia wanashangaa kwa kuwa hakuna mwanamke anafanya hasa greda yenye virungu vingi nilikuwa naipenda japo watu wanaiogopa.”

Anasema alimaliza mafunzo kwa vitendo na baadaye alirudi nyumbani. Tangu wakati huo katika fani zote mbili imekuwa vigumu kwake kupata ajira. “Nimemaliza mwaka huu bado naendelea kuomba kazi hapo GGM nimefanya mahojiano mara nne lakini sijaitwa.

Sophia anatoa wito kwa wanawake, “Kinamama na kinadada ukiamua kufanya kitu fanya, ilimradi ujiridhishe unakiweza na ukipende. “Urembo, kupaka kucha rangi, kubandika hivyo vitu vipo tu, ukiviendekeza utajikuta unawategemea wanaume kwa kila jambo,” anashauri.

Anasema hata yeye akiwa mgodini huwezi kumtizama mara mbili, lakini akizichanga anajipodoa na kuwa mrembo kama wasichana wengine.

Anasema wanaume wengi wanapenda wanawake wenye msaada katika maisha ili wakikwama maisha yanasonga.

“Nafanya kazi ngumu sijafa, sijaharibika na ni mama nina mtoto mmoja wanawake waondoe dhana kuwa kazi ngumu ni za wanaume.

“Kila kazi ni ngumu kama hujajipanga, hivyo wakijipanga na kudhamiria wanaweza kufanya yoyote, wanaume pia watambue hakuna kazi zao, zilizopo ni zetu sote, ”anasema.

Advertisement