ANTI BETTIE: Sifikirii kuachana naye, tabia zake zinanilazimisha

Anti habari, nina mwanaume naishi naye kwa miezi sita sasa. Hatujafunga ndoa kwa sababu hana kazi, hivyo navumilia akipata tutakamilisha lengo hilo.

Lakini mwenzangu haonyeshi kujali kama mimi nimejitolea kwa ajili ya penzi letu, kila kukicha anabadili wanawake hadi wengine wananitukana, sifikirii kumuacha, lakini tabia yake inashawishi kufanya hivyo.

Nifanyeje?

Pole sana. Ushauri wangu kwako ni kusema naye kabla hujalalamika, kwa sababu inawezekana anadhani hujui vitu anavyovifanya. Pia ukizungumza naye utajua msimamo wa mahusiano yenu kulingana na namna anavyokujibu.

Nakushauri pia usinyong’onyee kwa kumvumilia mtu amabye haonyeshi dalili za kutimiza mlichokipanga, kwani anaweza kukufanya kimada milele na wewe ukaendelea kusubiri ndoa hadi unazeeka. Kumvimilia mwenzako kama hana fedha au kazi ni jambo jema, lakini shirikiana naye kufanya mipango ya kuhakikisha mnajiingizia kipato siyo lazima aajiriwe mnaweza kujiajiri hata kwa mtaji mdogo.

Haogopi corona, nifanyeje?

Mume wangu sijui mtu wa aina gani jamani, kila mahali wanazungumzia janga la corona, lakini yeye haogopi hata kidogo. Anakesha katika mabaa anarudi usiku mwingi akiwa amelewa, nikimweleza hanisikii. Nifanyeje?

Waswahili walisema unaweza kumpeleka punda mtoni, lakini si kumlazimisha kunywa maji. Umesema anakesha baa na kurudi usiku mwingi, tuseme labda anakwenda baa ambazo hazina watu wengi, lakini bado anapaswa kutulia nyumbani wakati huu wa tishio la maambukizi ya ucorona.

Jambo la kufanya hakikisha akirudi nyumbani unamsimamia ananawa maji yanayotiririka na sabuni, ikiwezekana weka beseni lenye maji na sabuni nguo zake akivua aziweke humo.

Pia shirikisha ndugu zake na zako kuhusu ukaidi wake huo kwani hiki si kipindi cha mzaha, mkishindwa kuelewana ujitenge naye hadi hatari ya corona itakapokwisha.

Naamini akisikia suala kujitenga anye pamoja na wanafamilia wengine ataona umuhimu wa kubadili mienendo ya maisha. Hii pia iwe fundisho kwa wengine, dunia inapambana kukabiliana na janga la corona, lakini wa kwanza kukabiliana na janga hilo ni mtu binafsi kwa kubadili mtindo wa maisha kwa wakati huu. Kuacha kuchangamana na watu, kuepuka mikusanyiko na kupeana mikono, katika baa hatari inakuwa kubwa hata kama mpo wachache kwa sababu mnapoanza kila mmoja anakumbuka kuhusu corona, lakini kinywaji kikipanda siyo rahisi kukumbuka na badala yake mtakuwa mnashikana, mnakumbatiana na kupeana mikono, jambo ambalo ni hatari.