TUONGEE KIUME: Kwa nini uliamua kuoa?

Sunday October 27 2019

 

By Kelvin Kagambo

Je, ni kwa sababu ulikuwa unampenda mwanamke huyu zaidi ya kitu chochote duniani au alikuwa karibu yako wakati hamu ya kutaka kuanzisha familia imekushika?

Au pengine ulipelekwa kwake na upepo wa kisulisuli, kufumba na kufumbua ukajikuta ndani ya ndoa. Au labda muungano huu ulikuwa nje ya matakwa yako, wazazi wako walitaka muwe mke na mume au familia yake ililazimisha muoane. Au inawezekana ulimjaza ujauzito, ukatakiwa umuoe mkalee mtoto utake usitake. Au huenda ulikuwa na hali mbaya kiuchumi, katika kutapatapa kwako ukajikuta unaishi chini ya hisani yake, matokeo yake ukalazimika kuoa ili uendelee kusaidiwa au ukaamua kuwa mume kama malipo ya fadhila aliyokupa kipindi chote?

Au basi tuseme mwanamke huyu ni mzuri sana, ukimtazama hivi kuna baridi fulani unapata unahisi ni kama umeshinda jackpot hivyo ukaona huna sababu ya kuacha aolewe na baharia mwingine, ukachukua hatua na ukalipa mahari ukamuweka ndani. Au inawezekana hana huo uzuri isipokuwa ni mchapakazi, hana tamaa za kisichana wala mambo mengi ya ujana, ana maadili na mshika dini anayejua kutunza mume, watoto, wakwe na familia?

Ulioa kwa sababu gani?

Au kwa kuwa swahiba zako wote walikuwa wameingia kwenye ndoa, ukajisikia vibaya kuona umebaki mwenyewe huku nje, ukaamua utafute mtu harakaharaka uoe. Au itakuwa kila siku familia ilikuwa inakuuliza utaoa lini, ukachoka hili swali ukaona bora uoe.

Au umeshachangia sana harusi za wenzio kwa hiyo ili kurudisha fedha zako ukaona uoe fasta fasta ili uchangiwe.

Advertisement

Inawezekana kuna lengo ulikuwa unasubiri litimie ndiyo uoe kwa hiyo sasa imekuwa hivyo. Labda ulijisemea nikijenga au nikinunua gari au nikifungua biashara yangu nitaoa na kutulia niangalie familia au pengine mwenyewe ulijiwekea muda kwamba ukitimiza miaka 30 tu unaoa.

Kwa nini una mke?

Kwa sababu ya mafundisho uliyopewa kanisani yanasema inabidi uoe au labda wewe unafuata ulichoelekezwa na masheikh kwamba ndoa ni nusu ya dini? Au umeoa kwa sababu hutaki uzeeke ukiwa bachela kwa kuwa watu watakucheka na kutokuheshimu au basi tuseme umeoa kwa sababu ya kupata mtu wa kukusaidia kazi za nyumbani kama kupika, kufua na kadhalika.

Itakuwa umeoa kwa sababu dini yako inakataza zinaa. Kwa kuwa tendo la ndoa ni muhimu na la kibaiolojia na kihisia hivyo umeamua kupata mtu wa kushiriki naye kwa halali?

Kuna sababu nyingi sana zinazotuingiza wanaume kwenye ndoa na kwa kawaida sababu hizi ndiyo kitu pekee huamua itakuwa na hali gani.

Ukiona ndoa yako ina matatizo kaa chini tulia, rudisha akili yako nyuma kumbuka uliingia kwenye ndoa hii kwa sababu gani tatizo kubwa linaweza kuwa liko hapo.

Advertisement