TUONGEE KIUME: Tunachowapa madada wa kazi, sicho walichokifuata

Sunday November 3 2019

 

By Kelvin Kagambo

Tusiwaharibu hawa watoto, wanakuja kwenye majumba yetu kufanya kazi wakiwa na umri mdogo si kwa sababu wanapenda hapana, bali maisha yamewafurusha na kuwasogeza kwetu.

Huenda mioyoni mwao wanatamani muda huu wangekuwa darasani wanafunzwa Fizikia na mwalimu Mbaga, lakini njaa kali katika familia zao imewafurusha na kuwaangushia kwako muda huu anaosha vyombo vingi kwenye karo ili apate hicho unachokiita mshahara, amtumie bibi yake aliyemuacha Kigoma vijijini anunue angalau mafuta ya taa usiku asilale giza.

Huenda muda huu angekuwa na wanafunzi wenzake kwenye ziara ya kimasomo Bandari ya Dar es Salaam, ameshika kalamu na karatasi, anasikiliza na kunakili maelekezo kutoka kwa ofisa wa Bandari jinsi makontena yanavyopakuliwa melini lakini hapana, maisha yamemfurusha na kumuangushia kwako na muda huu yuko sokoni kwenye ziara ya manunuzi kwa ajili ya chakula cha familia yako, ameshika kikapu na karatasi mkononi, karatasi yenye maelekezo ya anunue bamia, viazi fungu ngapi? Mchele na nyama nusu kilo buchani kwa Msambaa.

Huenda muda huu alitakiwa kuwa anarejea nyumbani kutoka shule akifika anakula, kisha anashika daftari zake na kusoma kidogo akijiandaa na mitihani ya ‘moko’ kesho lakini hapana, maisha yamemfurusha na kumsukumia kwako, na muda huu anarejea nyumbani kutoka sokoni akifika anatakiwa awapikie, kisha afue majinzi yako magumu, nguo za mkeo na za watoto nyumba nzima, halafu ajiandae kuoga masimango na matusi kutoka kwa mkeo kwa kosa dogo tu alilofanya la kuacha taa ya chumbani ikiwaka siku nzima.

Sisemi kwamba mnawaharibu watoto hawa kwa kuwapa hizi kazi hapana, inawezekana wanastahili kwa sababu walikuja kwenu kwa ajili hiyo kwa makubaliano kwamba mtawalipa, na ni kweli mnawalipa. Ninachosema ni mnawaharibu hawa watoto kwa kuwapa kazi zingine ambazo awali hamkukubaliana nao.

Wakati mnawachukua hawa watoto hamkuwahi kuwaambia kwamba kila ikifika usiku watu wote wakiwa wamelala, wewe mzee mtu mzima utamvizia na kuingia chumbani kwa kunyata na umfanyie mambo ambayo nina uhakika hutamani na hutaki kuona watoto wako wa kike wakifanyiwa, kwa hakika huku ni kuwaharibu hawa watoto.

Advertisement

Wamekuja kwenye familia zetu kutafuta maisha, kufanya kazi kama ambavyo sisi tunaamka asubuhi kwenye vibarua vyetu hawajaja kupata manyanyaso ya kisaikolojia na kijinsia, huko ni kuwaharibu.

Ni vyema kama unahisi wewe na familia yako ni wadhambi kushinda shetani ni bora umkatalie mkeo asiende kijijini kumchukua huyu mtoto wa watu ili aje kutesekea zaidi. Kama unahisi wewe na familia yako ni mashetani kuzidi ibilisi, kwamba hamuwezi kumlipa hizo elfu 35 mnazoziita mshahara pasi na mkeo kumtukana bila sababu za msingi kila kukicha au wewe kumuingilia kimwili bila hiyari yake.

Ni vyema mumuache kwa mzazi wake ateseke kwa shida ambazo zimemlea na kumkuza kuliko haya matatizo mnayomfanyia.

Advertisement