Tambola na Mokili moja ya nyimbo zilizotamba miaka ya 1970

Saturday May 11 2019Anko Kitime

Anko Kitime 

By Anko Kitime

Tambola na mokili di eh eh

Omona makambo

Moto ako sala yo mabe

Se moninga bo melaka na ye eh

Moninga to vandi na ye oh oh

Apesaka nga gentil ya monoko

Kasi na motema na ye oh oh

Azua nga enemi na ye ya liboso

Ako lingaka nga eh

Kaka soki amoni nga nazali

Soki na pesi ye mokongo

Bo ndoki nyoso ebimi

Soki na pesi ye mokono

Bondoki nyoso ebimi oh oh

Haya ndio maneno ya beti za mwanzo za wimbo Tambola na Mokili wa kundi la Conga Succes, kundi lililoongozwa na mwanamuziki Johnny Bokelo Isenge. Maana za beti hizi mbili kwa kifupi ni kama ifuatavyo,

Zunguka dunia

Uone mambo

Atakae kudhuru

Ni rafiki unayezunguka nae

Niliwahi kuwa na rafiki

Mzuri kwa nje.

Lakini rohoni mwake

Mimi ndie adui wake wa kwanza

Aninipenda nikiwa nae

Nikiondoka tu

Roho yake mbaya ndipo inajitokeza

Wimbo huu wa bendi ya Conga Succes uliopendwa sana, na mara ulipotoka mwishoni mwa miaka ya 60, ulikuwa ni wimbo uliokuwa ukipigwa sana kwenye majukebox yaliyokuwa yamesambazwa katika baa mbalimbali nchini kwa muda mrefu sana.

Johnny Bokelo aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo alizaliwa mwaka 1939 nje kidogo ya jiji la Kinshasa. Alikuwa mtoto wa familia iliyokuwa na wanamuziki kadhaa ambao walikuja kuweka alama yao katika muziki wa Kongo miaka hiyo kama ntakavyohadithia hapa.

Kaka yake Paul Ebengo Dewayon alikuwa kati ya wanamuziki wakubwa wa kwanza wa rumba nchini Kongo. Mwaka 1955 Paul Ebengo Dewayon alikuwa kiongozi wa kundi la Watam ambalo lilikuwa na mwanamuziki Franco Luambo na Johnny Bokelo Isengo.

Mwaka 1956 Franco na wenzie walienda kuunda OK Jazz Dewayon akaunda kundi lake na kuliita Conga Jazz akisindikizana na mdogo wake Johnny Bokelo.

Kundi hili la Conga Jazz lilikuwa na wanamuziki wengine ambao walikuja kutamba katika muziki wa Kongo, kundi lilikuwa na wakali wengine kama mtunzi na mpiga gitaa Lutumba Simaro na mpiga saksafon maarufu Kiamuangana Mateta Verckys.

Mwaka 1958 Johnny Bokelo akiwa na mdogo wake Mpia Mongongo maarufu kwa jina la Porthos Bokelo walianzisha bendi waliyoiita Conga Success, kaka yao Dewayon akajiunga nao mwaka 1960. Dewayon na Johnny walikuwa waimbaji, watunzi na wapiga magitaa ya solo, wakati Porthos ndie aliyekuwa mpiga gitaa la rhythm katika nyimbo nyingi zilizotamba za bendi hiyo. Mwaka 1962, Dewayon aliacha bendi ya Conga Succes na kuanzisha bendi ya Orchestra CoBantou ( Congo Bantu), bendi ambayo nayo ilikuja kufanya mambo makubwa katika muziki wa Kongo.

Dewayon alikuja kufariki mwaka 1993. Bokelo akaendelea kupiga muziki wake ambao ulikuwa ukifanana kwa namna flani na ule wa rafiki yake Franco, walieanza naye muziki wakiwa watoto.

Conga Succes ilikuwa ikitoa vibao vingi na karibu vyote vilipendwa. Bendi hii ilianzisha mtindo wa kutoa nyimbo zilizoitwa Mwambe, kulikuwa na Mwambe na 1 hadi 6 katika kipindi cha uhai wa bendi hii, na kupata sifa ya kujulikana kama ‘Wana Mwambe’ .

Vibao vingine vilivyotolewa na bendi hii ni kama Navanda Ndumba, Ngoya, Sandokan, Engunduka na FC Dragon, kibao kilichokuwa cha kusifu timu ya mpira ya Dragon, viliwezesha kupata wapenzi wengi kwani muziki wa Conga Success ulikuwa unahamasisha kucheza katika staili yao ya Mwambe.

Mwaka 1968 Bokelo alibadili jina la bendi yake na kuiita Conga 68, na kisha akaanzisha label mpya ambayo aliitumia katika kusambaza nyimbo zake. Hili lilileta ugomvi kwenye bendi kwani wenzie walilalamika kuwa hawakuwa wanafaidika na mradi huo mpya wa label, kwani kabla ya hapo nyimbo zao zilikuwa zikitumia label kutoka Ufaransa na walikuwa wakipata chochote kutokana na tungo zao.

Baada ya hapo Bokelo alianza kutumia muda mwingi Bokelo kwenye studio yake kurekodi, hakuwa anafanya tena maonyesho kwenye kumbi. Kiwanda pekee cha kuchapa santuri jijini Kinshasa kikaanza kupata matatizo ya uzalishaji, Bokelo akaanza kutumia viwanda vya Kenya kuchapisha kazi zake. Januari 15, 1995 Johnny Isenge Bokelo alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwanae Johnny Bokelo, aitwae Bokelo Blito ameanza kujaribu kufuata nyayo za baba yake, maana imelazimika mpaka baba yake alipofariki ndipo aanze muziki kwani mzee Bokelo hakutaka kabisa mwanae yoyote afuate nyayo zake.

Advertisement