KUTOKA LONDON: Tunapofiwa na tunaowapenda twajifunza nini?

Sunday May 12 2019Freddy Macha

Freddy Macha 

Kufuatana na takwimu za “tovuti ya mazingira”, watu wanne huzaliwa na wawili kufariki kila sekunde hapa duniani. Wanaokufa ni wachache zaidi ya wanaozaliwa. Mwaka 2011, kiasi cha wanadamu 151, 600 walifariki ilhali 360,000 waliubishia hodi uhai, kwa siku.

Kila mwezi huwa tunawakaribisha wanadamu wapya na kuwapoteza wengine. Mzunguko huu ni sayansi ya ulimwengu.

Juma hili Harry, mjukuu wa malkia Elizabeth, alifurahia kuzaliwa mtoto wake wa kwanza na mkewe - nusu mzungu na mweusi aitwaye Meghan.

Juma lililopita Waafrika tulipoteza watu watatu maarufu. Mwanamuziki Moise Fan Fan alifariki kwa maradhi ya moyo, Nairobi akiwa na miaka 75. Gwiji Fan Fan aliwahi kucharaza gitaa na bendi ya mfalme wa mtindo wa “Soukous” (mzazi wa Ndombolo), Luambo ‘Franco’ Makiadi mwaka 1972.

Juma hilohilo Tanzania iliibiwa ilipoteza mchapakazi aliyeendeleza vyombo vya habari na biashara, Reginald Mengi. Kifo cha Mengi kilishtua hadi ikabidi Rais mstaafu Jakaya Kikwete awasihi wananchi wasisikilize maneno ya mitandaoni. Kati ya mazito yaliyotajwa kuhusu Mzee Mengi ilikuwa maandishi ya mtangazaji wa michezo wa Tanzania Sports aliyepo London, Israel Saria aliyekumbuka namna Mengi alivyoendeleza mashindano ya michezo miaka ya 1980.

“Kwa wakazi wa Moshi, Bonite Cup, ilikuwa kama Olimpiki, kila taasisi ilifaidika na shindano hilo...” aliandika Saria katika akaunti yake ya Facebook, Mei 3.

Advertisement

Hapahapa London tulifiwa na mpiga ngoma na mwanamuziki wa Kinigeria, Baba Adesose Wallace. Si wengi Afrika Mashariki waliomsikia. Wala hakurekodi nyimbo nyingi, lakini aliwahi kupiga na takribani wanamuziki vigogo wote wa Kiafrika mathalani Miriam Makeba, Fela Kuti, Sunny Ade na Hugh Masekela.

Mwanamuziki wa Kitanzania, mkazi Uingereza, Saidi Kanda aliyewahi kufanya naye kazi alisema Ade alikuwa kati ya Waafrika wa kwanza kupiga miziki ya Kiafrika sehemu ambazo Wamatumbi hawakukanyaga. Zamani Kanda alikung’uta ngoma na bendi kabambe ya Super Matimila ya Hayati Remmy Ongala.

Tuelewe maana ya maneno yake ‘Wa Kanda’. Sisi Waafrika tuna muziki wa hali ya juu. Miziki yetu inatofautiana kikabila, kijimbo na kimila.

Midundo ya Kiafrika imezua miziki inayouzwa ya pop katika nchi zilizoendelea. Sisi Waafrika hatuitambui miziki hii. Bado tunajidunisha. Soko la muziki wa dunia liitwalo “World Music” lilipobuniwa miaka ya 1980 na mwanamuziki wa Kizungu, Peter Gabriel, lilijengwa na wanamuziki kama Baba Adesose Wallace.

Baba Ade aliagwa kwa siku mbili.

Mosi ilikuwa wapiga ngoma tuliokusanyika Magharibi ya London.

Siku iliyofuata ikawa ibada katika Kanisa la Paddington Green, ambapo dada yake, Goke Braithwaite alitueleza maisha yake.

Hapa ndipo ilipoonekana namna Baba Ade alivyopendwa. Ikafuata sala ya Kiislamu makaburini. Shehe akatathmini thamani ya kuwa mtu mzuri maishani.

Udongo ulipokuwa ukitupwa jenezani, ngoma na muziki wa jadi ukapigwa kwa nguvu.Hapo ikashuhudiwa Ukristo, Uislamu na jadi ya Mwafrika kwa pamoja. Tulijazana zaidi ya watu 200 makaburini.

Kila mtu huagwa kufuatana na alivyoishi.

Ndugu msomaji hukuwahi kumsikia, Baba Ade. Ila elimu ya makala haya ni kutukumbusha kuishi kwa malengo, nidhamu, na kujaribu kuuendeleza ulimwengu wetu.

Advertisement