UJASIRI: Wanzira mwanamke anayepambana katikati ya mfumo dume

Sunday November 3 2019

 

By Antony Mayunga, Mwananchi

Kadri siku zinavyosogea, idadi ya wanawake wanaoongoza taasisi mbalimbali inaongezeka.

Hilo lilidhihirishwa na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Bunge, Jenista Mhagama mwaka 2018 alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Waajiri (Ate).

Jenista alisema mwaka 2017 idadi ya wanawake katika bodi mbalimbali za taasisi za Serikali iliongezeka na kufikia 117 kutoka 114 kwa mwaka 2014, ikilinganishwa na wanaume ambapo walipungua toka 526 mwaka 2014 hadi 352 mwaka 2017.

Mbali ya hilo, alisema katika miaka hiyo idadi ya wanawake majaji iliongezeka na kufikia 39 kati ya 95, wakati mwaka 2012 majaji wanawake walikuwa 34 kati ya 97.

“Wanawake wameondokana na woga na kuamua kupambana kutimiza ndoto zao,” anasema Wanzira Wambura (38), ambaye ni meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) mkoa wa Mara.

Anasema akiwa chuo (Mwananchi wanalo jina la chuo hicho) kuna mwalimu alimfelisha makusudi kwa sababu alikataa kutoa rushwa ya ngono.

Advertisement

“Mkufunzi mmoja aliamua kwa makusudi kunifelisha,. Roho iliniuma ila nikajiapiza nitapambana kutimiza ndoto zangu,” anasema Wanzira.

Anasema kuanzia hapo alielewa maana ya mfumo dume na kuuchukia.

“Ilibidi nikatishe masomo yangu. Nilikubali kukaa nyumbani kwa sababu moja muhimu kwangu; kuulinda utu wangu,” anasema.

Anasema jambo hilo lilimpa ujasiri wa kupambana ili aonyeshe namna ambavyo wanawake wanaweza kujisimamia bila kujidhalilisha.

Anasema baadaye alijiendeleza kielimu na kufanikiwa kusonga mbele.

“Mwaka 2018 niliona tangazo la nafasi za kazi TTCL. Kwa kujiamini niliandika barua ya kuomba kazi nikiambatanisha na wasifu wangu (CV) niliitwa katika usaili, nikaajiriwa kama meneja msaidizi, kituo changu cha kwanza kikiwa mkoani Mara,” anasema.

Anasema alifanya kazi miezi mitatu ya kupimwa na kuthibitishwa kulikoambatana na kuteuliwa kuwa meneja wa TTCL mkoani Mara.

“Hapa tena nilikutana na changamoto ya kuwa mwanamke, kwa kuwa kuna mfanyakazi mmoja bila aibu aliwahi kusema hawezi kufanya kazi chini ya mwanamke.

“Kwa sababu ni changamoto niliyokwishakutana nayo huko nyuma, hakunisumbua ndiyo kwanza alisisimua ari ya kuwa kiongozi bora anayesimamia misingi ya kazi,” anasema Wanzira.

Anasema silaha kuu anayotumia ni kuwaongoza walio chini yake kwa kufuata sheria na kuchapa kazi pasina shaka.

“Usiposimama imara wanaume wanakuondoa kwenye mstari. Tangu zamani wao ni viongozi, waume zetu, baba zetu. Wanatujua vizuri, inakuwa rahisi kwao kuturudisha nyuma wakisaidiwa na imani zilizopo kwenye jamii zetu.

“Hapa mkoani mimi ndiyo mtendaji wa juu peke yangu. Nasimama imara, nasimamia haki ya kila mmoja, wafanyakazi wenye nia njema wananielewa na shirika linasonga.”

Wanzira anasema kwake mfumo dume ni fursa na anapokutana na watu wenye mtazamo huo, jibu lake ni kufanya kazi kwa bidii matokeo huwa ni majibu kuwa mwanamke anayejitambua anaweza kufanya vizuri zaidi ya mwanaume mnyanyasaji.

Anasema bado jamii inakabiliana na changamoto ya wanawake kutojiamini, kukosa stadi za maisha.

“Wanawake wengi hawatafuti maarifa, hapo ndipo wanaume wanapotushinda. Wapo mbele katika hilo,” anasema.

Meneja huyo anasema kiu yake ni kuiwezesha TTCL kuwa mtandao bora mkoani Mara kuanzia mjini hadi vijijini, kazi ambayo anaifanya kila wilaya kwa kushirikiana na maofisa wenzake baada ya kutambua uwezo wake.

“Shirika linashiriki maonyesho mbalimbali kiwilaya na kimkoa kwa lengo la kuwafikia wananchi, pia kuna michezo ambayo tunaitumia kufikisha ujumbe wa utendaji wetu,’’ anasema.

Advertisement