USHAURI WA DAKTARI: Si Ukimwi tu, ipo haja kupima magonjwa mengine ya zinaa

Magonjwa ya zinaa ni moja ya magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kwa kasi katika siku za karibuni. Kutotumia kinga katika tendo la ndoa na kuwa na washiriki wengi ni baadhi ya sababu kubwa zinazochangia maambukizi ya magonjwa hayo.

Tunapozungumzia magonjwa ya zinaa jambo ambalo wengi huwajia akilini ni Virusi vya Ukimwi (VVU) japokuwa kuna magonjwa mengine mengi ya zinaa kama kisonono na kaswende.

Magonjwa ya zinaa yana madhara makubwa kuanzia kwenye mfumo wa uzazi na hata afya kwa ujumla kwani huchangia kusababisha ugumba na utasa na hata aina mbalimbali za magonjwa ya saratani bila kusahau matatizo mengine kama vile kusababisha harufu mbaya kwenye via vya uzazi.

Jiulize, je una utamaduni wa kupima magonjwa haya ya ngono mara kwa mara? Kama daktari nakiri bado watu hawatilii maanani kupima magonjwa ya zinaa. Nakushauri ni vyema ukaanza utaratibu huo kwa kuwa kadri unapowahi kugundua magonjwa ya zinaa mapema, ndivyo unapokuwa na nafasi nzuri ya kupona kwa kuwahi matibabu na kuzuia madhara mengine.

Lakini je? Unatakiwa kupima mara ngapi kwa mwaka? Kujua unahitaji kupima mara ngapi kwa mwaka kunategemea unashiriki tendo la ndoa mara ngapi na washirika wangapi tofauti na hasa kama hautumii kinga. Hivyo ushauri wangu ni kuwa na utaratibu wa kujiwekea ratiba ya kupima magonjwa ya zinaa. Kuna kundi la watu wanaodumu na mshirika mmoja tu wa tendo la ndoa kwa muda mrefu, na hii ndiyo inayoshauriwa kiafya na kimaadili. Kuwa na mshirika mmoja kunasaidia kujikinga na hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa, hasa Ukimwi. ingawa pia haimaanishi kuwa haupaswi kuendelea kupima.

Kuwa na mshirika mmoja haina maana hauwezi kuambukizwa magonjwa ya zinaa. Unaweza kuambukizwa ila tu hatari ya kuambukizwa ni ndogo. Hivyo kama una mshirika mmoja unashauriwa kupima angalau mara moja kwa mwaka.

Kuna watu wanaokuwa na mshirika mmoja lakini hawadumu naye, baada ya muda mahusiano yanavunjika na kutafuta mshirika mwingine.

Kundi hili pia halina tofauti sana na mtu mwenye washirika wengi wa tendo la ndoa kwa muda mmoja. Kundi hili lipo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kuliko kundi lingine lolote hasa tukizingatia ukweli kuwa ni vigumu kumkosa mtu mwenye maambukizi kati watu watatu hadi watano unaoshirikiana nao kimapezi.

Ndani ya idadi hii lazima utampata mwenye maambukizi ya magonjwa ya zinaa iwe Ukimwi au mengineyo. Kundi hili linahitaji vipimo vya magonjwa ya zinaa kila baada ya miezi mitatu kutokana na hatari kubwa ya kupata maambukizi na kushiriki tendo la ndoa na idadi kubwa ya watu ndani ya muda mfupi.

Pia bila kuwasahau wanaopenda kufanya ngono kwa njia ya haja kubwa na mdomo. Hawa pia wapo hatarini sana kupata aina nyingi za magonjwa yaambukizwayo kwa njia ya ngono, nao wanahitaji vipimo mara kwa mara. Aidha ningependa kuwashauri watu kuacha kufanya ngono kupitia haja kubwa na mdomo, sehemu hizi ndizo hubeba hatari zaidi ya maambukizi lakini hata wanaoshiriki tendo la ndoa na idadi kubwa ya watu kwa kipindi kifupi ni vyema wawe wanatumia kinga ili kujilinda na hatari hii ya kupata maambukizi.