USHAURI WA DAKTARI: Hawa wasifanye hivi kipindi cha corona

Vifo vingi vya wagonjwa wa Covid-19 vinavyotokea duniani vinaonyesha kuwapata zaidi watu ambao wana umri mkubwa kati ya miaka 49-60 na wale wanaogua magonjwa mengine.

Magonjwa hayo ambayo huwa ya kudumu au sugu yakiwamo yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, kisukari, kiharusi, figo, saratani, pumu na matatizo sugu ya mkwamo wa hewa.

Vilevile kuna magonjwa mengine ya kuambukiza ikiwamo kifua kikuu, VVU, nimonia na homa ya ini.

Uwepo wa magonjwa hayo na umri mkubwa ni mzigo kwa kinga ya mwili. Hivyo kupata ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona kunaupa mwili mzigo mkubwa na hatimaye kuwa katika hatari ya kuzidiwa na hata kifo.

Udhaifu wa kinga, uwepo wa magonjwa mengine na umri mkubwa ni vihatarishi vya kupata ugonjwa huu.

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wagonjwa 100 wanaougua Covid-19, 80 hawapati dalili kali na kati ya wagonjwa sita mmoja ndiyo hupata corona kali.

Hivyo si kila anayeumwa ugonjwa huu lazima afe au apate makali ya ugonjwa ila ni vizuri kujikinga mapema zaidi kwa akuwa bado mtu huyo huweza kuambukiza wengine.

Mzee au anayeugua magonjwa mengine kuchukua hatua za kujikinga mapema na jaribu kubeba hisia kuwa huu ugonjwa upo kila mahala.

Zingatia maelekezo ikiwamo kunawa mikono na sabuni kwa maji yanayotiririka au kitakasa mikono, kutojishika maeneo ya usoni na kutoshika shika vitu vinavyoshikwa sana katika jamii.

Vilevile kujitenga, kuikaa mbali na wengine angalau mita moja, kutochangamana na mikusanyiko au misongamano na zuia chafya au kikohozi kwa kona ya mbele ya kiwiko.

Mtu mwenye vihatarishi viwili yaani umri mkubwa na magonjwa mengi, anahitajika kuhakikisha kuwa anashikamana na ushauri wa matibabu anayopewa kwa ajili ya matatizo ya kiafya aliyonayo.

Kama mgonjwa ana kliniki ya tiba na anatumia dawa za kila siku shauriana na daktari njia bora za kujihami kipindi hiki ikiwamo kukupa muda zaidi ili kuepuka kwenda mara kwa mara kliniki.

Hii ni kutokana na hatari ya maambukizi ya corona inaweza kuwa juu katika maeneo zinakotolewa huduma za afya kwa sababu ya mikusanyiko na msongamano, ikitokea kwenda basi iwe ni uwepo wa tishio la kiafya la dharura.

Kama una masharti mbalimbali kama vile vyakula au mienendo na mitindo fulani ya kimaisha vema kuzingatia ushauri wa daktari.

Ikumbukwe pia kujitenga ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na hatari ya maambukizi ya corona vizuri kutulia ndani zaidi hata kama huna dalili.

Pale unapokuwa umeyadhibiti magonjwa mengine uliyo nayo ina maana hautakuwa na haja ya kufika katika huduma za afya, hivyo unajipunguzia hatari ya kuchangamana na mikusanyiko.

Ili kujiepushia hofu, woga au wasiwasi isiyo na lazima epuka taarifa za mitandao zisizo rasmi zinazoweza kukupa msongo wa mawazo, ambao unaweza kuteteresha kinga yako ya mwili.

Fanya vitu vinavyokupa faraja na furaha kama vile mazoezi mepesi ya ndani ikiwamo kuruka kamba, kutembea, kupanda ngazi, kucheza na sikiliza muziki au tazama vipindi vya runinga vinavyokupa hisia nzuri.

Fuatilia taarifa za Wizara ya Afya na WHO, vile vile jenga mawasiliano na daktari anayekuhudumia magonjwa mengine uliyonayo.