USHAURI WA DAKTARI: Je, corona ina athari kwa mjamzito?

Tangu dunia iingie katika janga la ugonjwa wa corona kumekuwa na maswali kadhaa kuhusu ugonjwa huu ambao mpaka sasa hauna tiba wala kinga.

Kabla ya kupata ufahamu wa makala ya leo ni vizuri kujikumbusha kuwa tunahitajika kujikinga na corona kwa kuosha mikono yetu kila mara kwa sabuni na maji yanayotiririka, kutoshika maeneo ya usoni, machoni na puani, kuepuka kukaribiana na walioambukizwa na kuepuka misongamano isiyo na lazima.

Mmoja wa wasomaji wetu aliuliza kama corona ina madhara kwa mjamzito na mtoto.

Kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) hakuna taarifa rasmi kuhusu madhara ya corona kwa wajawazito wala kwa mtoto aliye katika nyumba ya uzazi.

Ingawa taarifa mbalimbali zinazohusu corona kwa wajawazito zilitolewa wiki hii na Kituo cha Utafiti cha Magonjwa ya Binadamu cha Marekani (CDC) na mtandao wa Kaizer Family Foundation (KFF) ziligusa yafuatayo.

Taarifa hizo zilionyesha kuwa tafiti ndogo zilizofanyika jijini Wuhan China, Hazijaonyesha ushahidi kuwa virusi vya corona vinaweza kuvuka na kwenda kumvamia mtoto anayepitia hatua za ukuaji katika nyumba ya uzazi.

Vile vile tafiti hizo zilizotolewa wakati wa mlipuko huu wa ugonjwa bado zinaonyesha kuwepo kwa visa vya wajawazito wenye maambukizi ya corona na kuzaliwa watoto wenye maambukizi ya corona.

Wajawazito wako katika hatari zaidi kupata maambukizi na pia waliopata corona wameonekana kuwa katika hatari ya kupata makali ya ugonjwa zaidi kulinganisha na wasio wajawazito.

Hii ni kwa sababu ujauzito huwa na mabadiliko mbalimbali ikiwamo kinga ya mwili kushuka ili kutoa nafasi kwa mwili kujikita katika hatua za awali za ujauzito.

Ushukaji huu wa kinga kipindi cha ujauzito una faida kwani uwepo wa mtoto ni kitu kigeni hivyo kinga ikiwa juu inaweza kuiharibu mimba.

Ila hasara yake ni ikiwamo kupata uvamizi wa magonjwa madogo kama vile fangasi wa ukeni na maambukizi ya njia ya mkojo mara kwa mara.

Vilevile mabadiliko katika mfumo wa chakula kwa muda fulani yanaweza kumfanya mjamzito kutokula vizuri hivyo ikaathiri uimara wa kinga yake na kuwa hatarini kupata maradhi ikiwamo ya mlipuko kama corona.

Ingawa kwa mjamzito kuugua ugonjwa wowote ule hasa katika muhula wa kwanza wa ujauzito kunamuweka katika hatari ya kupoteza ujauzito kwani ugonjwa wowote ule unamuweka katika shinikizo. Maambukizi ya corona huambatana na homa, kwa mjamzito huenda ikawa zaidi kuliko mtu wa kawaida, hivyo mimba inaweza kuwa katika hatari ya kuharibika.

Mjamzito kama watu wengine anapaswa kuzingatia njia zote za kujikinga na kuhakikisha anafuatilia taarifa mpya za Wizara ya Afya.

Wanasayansi hao wamependekeza ili kuwalinda wajawazito mahudhurio ya kliniki yafanyike kwa njia ya mawasiliano ya Telemedicine yaani kutumia runinga kuwahudumia wakiwa majumbani.

Watafiti bado wanahitaji muda zaidi kupata majibu ya maswali mengi kuhusu corona kwa mjamzito.