USHAURI WA DAKTARI: Madhara yatokanayo na vinywaji hivi

Vinywaji nguvu ni vinywaji laini visivyo na kilevi vijulikanavyo zaidi kwa lugha ya Kiingereza kama Energy Drinks ambavyo ndani yake huwa na vitu mbalimbali ikiwamo vichangamsha mwili na akili.

Baadhi ya vinywaji hivyo huwa na maji, sukari, ladha, caffein, mitishamba, tauline (amino acid), protini, vitamini, madini na virutubisho.

Matangazo ya biashara ya vinywaji hivi huwa ni ya kuvutia ikiwamo kuwaonyesha watumiaji wanavyochangamka kiakili, kuwa na nguvu na kasi, jambo linalowavutia wanajamii ikiwamo wanamichezo kuvitumia.

Tafiti za karibuni zinaonyesha vinywaji nguvu ambavyo vinatumiwa na watoto na wakubwa ndani yake huwa na kiambata cha caffeine kikitumika kiholela huwa na madhara.

Usalama wa vinywaji hivi unaulizwa katika jamii hasa kutokana na video za mitandaoni na taarifa zisizo rasmi.

Wanasayansi wa tiba na Lishe wamewahi kutoa machapisho kadhaa ya kisayansi kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) yanayoeleza athari za kutumia vinywaji hivi vyenye caffein kupita kiasi na kila mara.

Wanamichezo, wanafunzi na wafanyakazi ngumu ndiyo wanaotajwa zaidi kutumia vinywaji nguvu wakiamini kuwaondolea usingizi, uchovu na kuwapa nguvu zaidi.

Wapo wanamichezo ambao hutumia ‘Energy Drinks’ saa chache kabla ya kuingia kucheza au mara baada ya kucheza wakiamini itawafanya kupata nguvu za ziada na kucheza kwa kiwango.

Huku wanafunzi na madereva wakivitumia siku za mitihani ili kuuondoa usingizi na wanywaji wa pombe kali aina ya spiriti na whiskey hutumia vinywaji nguvu kuchanganyia.

Ni kweli kiambata cha caffein husisimua mfumo wa fahamu hali inayomfanya mtumiaji kuhisi kuchangamka na kuondoa uchovu.

Vile vile sukari na maji huwa na faida mwilini kwa kuupa mwili nguvu.

Caffein huainishwa kisayansi kama kundi la opiod yaani dawa ya kulevya aina ya kichangamshi (stimulant)kiwango chake katika vinywaji hivi kinakubalika ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Hata mamlaka za dawa na chakula zinakubali kuwa kiwango hicho ni salama, tatizo linakuja kwa watumiaji wanaotumika kupita kiasi bila kufuata maelekezo yaliyobandikwa katika chupa husika.

Imewahi kuripotiwa madhara mbalimbali ya kiafya na vifo pale vinywaji hivi vinapotumiwa kiholela.

Watumiaji wa energy drink kiholela wanapata kiasi kikubwa cha caffein ambayo huambatana na madhara ya kiafya katika mfumo wa fahamu, damu na moyo.

Kiambata hiki ndicho kinahusishwa zaidi na madhara ya kiafya ukilinganisha na vitu vingine.

Madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na degedege, kuumwa kichwa, kizunguzungu, kuzimia, hitilafu ya mapigo moyo, shinikizo la juu la damu, shambulizi la moyo na maumivu ya tumbo.

Pia uwepo wa kiasi kikubwa cha sukari na kiambata cha taurine navyo vinahusishwa na madhara ya kiafya.

Kisayansi ni kweli uwepo wa caffein katika vinywaji hivyo una athari chanya katika mwili na akili.

Faida zake ni pamoja na kuchangamsha misuli, kuongeza wepesi, nguvu na uimara wa misuli lakini bado madhara ya kiafya ya caffein ni makubwa kuliko faida hizi.